Pichani: Dkt. Asha-Rose Migiro, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akizungumza wakati wa majadiliano baina ya jopo la wataalamu na wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, kuhusu maendeleo endelevu, kushoto kwake ni Rais Tarja Halonen wa Finland ambaye ni Mwenyekiti mwenza na Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini, wakiongoza jopo hilo lenye wajumbe 21 na kulia kwa Migiro ni Rais wa Baraza Kuu la 65 la Umoja wa Mataifa, Bw. Joseph Deiss.
NA MWANDISHI MAALUM
NEW YORK
Hatima ya watu bilioni 9 wanaotarajiwa kuwapo duniani ifikapo mwaka 2050 imo mashakani kama hakuta kuwa na mipango madhubuti yenye kuleta maendeleo endelevu ili kuboresha ustawi wa maisha yao.
Angalizo hilo limetolewa na Asha-Rose Migiro, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, alipokuwa akifungua majadiliano baina ya nchi wanachama wa UM na jopo la wataalamu likiongozwa na wenyevitiwenza marais Tarja Halonen wa Finland na Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini. Majadiliano hayo yalihusu maendeleo endelevu.
Naibu Katibu Mkuu anasema kwamba jambo la msingi na ambalo jumuia ya kimataifa inapaswa kujiuliza je ni nini matumaini ya watu hao bilioni tisa.
“ Je watakuwa na matumaini ya kuwa na ustawi na maisha bora au idadi kubwa kati yao wataishia kuhangaika kutafuta mbinu za kujinusuru.
Na pengine kibaya zaidi watashuhudia dunia ikitumbukia katika machafuko. Haya ndiyo masuala ya msingi ya kujiuliza tunapojadilia suala la maendeleo endelevu” anasema Migiro.
Amebainisha kuwa jumuia ya kimataifa inatakiwa kuwa na mfumo mpya wa maendeleo ambao siyo tu utaendana na matakwa ya karne ya 21 lakini pia utakuwa kiunganishi cha mambo ya msingi ya wakati huu.
Anayataja mambo hayo kuwa ni kupunguza umaskini, kuibua nafasi za ajira, tofauti za usawa, mabadiliko ya tabia nchi, uhaba wa maji, na usalama wa chakula.
Akasema kwamba Katibu Mkuu Ban Ki Moon wa UM Agosti mwaka jana aliunda jopo lenye wajumbe 21 ili pamoja na mambo mengine,watafiti, watafakari na kuibua mwelekeo mpya kuhusu mustakabali wa maendeleo endelevu pamoja na mbinu za kufanikisha utekelezaji wake.
Aidha Naibu Katibu Mkuu anasema kuwa changamoto zinazoikabilia dunia hivi sasa zikiwamo za mkwamo wa uchumi, machafuko na majanga ya asili yanayoendelea kutokea katika mataifa mbalimbali duniani yasiwe kikwazo cha kutochukua maamuzi kuhusu maendeleo endelevu.
Bali anasema changamoto hizo ziwe kichocheo na kuongeza nguvu mpya . Na kusisitiza kuwa kubadili mwelekeo kutazua hatari mpya.
Lakini hatari kubwa zaidi anasema ni ile ya kutofanya chochote kwa maana ya kutozikabili changamoto hizo. Na kwamba huu ndio ulikuwa ujumbe wake anaotaka uzingatiwe na serikali zote na watoaji wote wa maamuzi.
Akafafanua kwa kueleza kuwa maendeleo endelevu yanategemea sana mambo matatu ambayo ni uchumi, jamii na mazingira na bali ni ushiriki wa sekta zote za kiserikali, kama vile fedha, nishati, na katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake Bw. Joseph Deiss,Rais wa Baraza Kuu la 65 la Umoja wa Mataifa, yeye alitoa wito wa uwepo kwa utashi wa kisiasa na kujituma ili kukabiliana na changamoto ambazo ni kikwazo kwa maendeleo ya watu.
“wote tunataka kuwa na maisha bora, maisha mazuri, lakini hili halitawezekana kama tutaendelea na mfumo huu tulionao sasa, tunahitaji kuunda mfumo mpya wa kuchagiza maendeleo” anasema Bw. Joseph Deiss
Aidha amewataka wanadamu kubadilika na kuachana na tabia ya zitakazopelekea kujimaliza wenyewe.
Jopo hilo la wataalam linatarajiwa kukabidhi taarifa yake mwisho mwa mwaka huu kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo endelevu unaotarajiwa kufanyia mwaka 2012 huo Rio de Janeiro, Brazil.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)