BABU ATOA MASHARTI 4 MAPYA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

BABU ATOA MASHARTI 4 MAPYA

 
WAKATI watu wakizidi kumiminika Loliondo katika Kijiji cha Samunge mkoani Arusha kwa ajili ya kupata tiba kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapile anayedaiwa kutibu magonjwa sugu kimaajabu, kiongozi huyo ametoa masharti manne mapya kwa anaowahudumia.

MASHARTI MAPYA
Akihojiwa na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita, Mchungaji Mwasapile ‘Babu’ alisema masharti hayo yanapaswa kuzingatiwa. Sharti la kwanza ni kutojipendelea, akafafanua kuwa itakuwa mwiko kwa mgonjwa kuvunja foleni ili kuwahi kunywa dawa.
 
Alisema, atakayefanya hivyo hata kama atawahi kumpa dawa, haitamsaidia na badala yake atakuwa kama amekunywa juisi tu.

Aliongeza kuwa, dawa hiyo yenye uwezo wa kuponya magonjwa mbalimbali yakiwemo Ukimwi, saratani, kisukari, shinikizo la damu (presha), vidonda vya tumbo na kadhalika imeonesha mafanikio makubwa.
“Hapa kuna masharti kwamba mtu asipokaa kwenye foleni na kufanya ujanja wa kuwapita wenzake ili awahi, hatapona. Atakunywa dawa kama juisi tu,” alionya mchungaji huyo.

Akitaja sharti la pili, babu huyo alisema katika eneo hilo mtu akimuibia mwenzake kisha kunywa dawa hiyo, pia hatapona maradhi yake.

Sharti la tatu alilolitaja ni kuwa, wagonjwa ambao wametundikiwa dripu hospitalini wasitolewe na kupelekwa kwake kwa sababu huko alipo hakuna huduma hizo (za drip).

Alitahadharisha kuwa, wale wote waliotumia dawa hiyo na kuponywa Ukimwi hawatakiwi kurudia vitendo vinavyoweza kusababisha wakapata maambukizi mapya hasa ya magonjwa ya zinaa.

Akafafanua kuwa, dawa yake si ya kuchunguzwa na vyombo vya kimaabara kama serikali ilivyokuwa inataka kwa kuwa ni ya miujiza na ni neno la Mungu.
 
Kuhusu mrithi wake ikitokea akaaga dunia, Mchungaji Mwasapile alisema wanaweza wasiwe watoto wake kwa sababu haya ni maamuzi ya Mungu.

Wachunguzi wa mambo wanadai kuwa, masharti hayo mapya yatawaumiza zaidi vigogo wa vyama na serikali kutokana na kupendelewa katika foleni kwani wengi hupenyezwa na kuwaacha walalahoi wakitaabika katika mistari.
Aidha, habari zinasema vigogo kadhaa wameonesha kukata tamaa kutokana na masharti hayo mapya aliyoyatoa Babu.

TIBA NYINGINE YA DAWA HIYO
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa eneo hilo waliozungumza na mwandishi wetu walisema kuwa, dawa hiyo imekuwa ikitumika tangu zamani kwa kuwapa akina mama waliojifungua. Dawa hiyo ilikuwa ikichanganywa na supu ya mbuzi na imekuwa ikiwasaidia sana wazazi kuondoa maumivu ya tumbo.
Idadi ya wagonjwa wanaofariki kutokana na kuzidiwa na maradhi na ugumu wa kumwona Mchungaji Mwasapile kutokana na foleni ndefu,  imeongezeka baada ya mtu mwingine, Philip Mbise kufariki mwishoni mwa wiki iliyopita kutokana na maradhi ya pumu kabla ya kumfikia Babu.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, wagonjwa wanaofariki ni wale wanaotolewa mahospitalini wakiwa na hali mbaya na wengine ni wale wenye umri mkubwa ambao hushindwa kuhimili hali ya hewa ya eneo hilo ambayo ni ya joto kali.

“Hapa tunavyoongea, muda mfupi uliopita kuna mtu amefariki. Unajua watu wanawaleta wagonjwa wao wakiwa wamezidiwa bila kujua kuwa huku hakuna huduma ya kwanza na wananchi hawatoi kipaumbele kwa waliozidiwa,” alisema mama mmoja mkazi wa Moshono mkoani Arusha.

Naye Mchungaji Mwasapile amesema kuwa, tangu apate maono ya dawa hiyo mwaka 1991, alianza kumtibu mtu wa kwanza aliyekuwa na Ukimwi mwaka 2009, akapona kabisa.
 
WAGONJWA KUTOROSHWA HOSPITALINI
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Dk. Joselin Mlay alisema kuwa, tangu Mchungaji Mwasapile aanze kutoa tiba hiyo, idadi ya wagonjwa hospitalini kwake imepungua huku sehemu kubwa ya waliolazwa wakitoroka na kutoonekana.

”Tangu huyu mchungaji apate umaarufu wa kutibu, hospitali zetu zimepungukiwa idadi ya wagonjwa, wengi waliokuwa wamelazwa hasa wa magonjwa sugu hawaonekani,” alisema Dk. Mlay.

AJALI ILIYOUA
Wakati huo huo, ajali iliyoua watu watano wiki iliyopita, imezua gumzo kwani wananchi wanadai huenda madereva na wasaidizi wao walikiuka masharti ya Mchungaji Mwasapile kwa kutoza nauli kubwa tofauti na wito alioutoa awali.
“Inawezekana kabisa kuwa onyo lake linatimia, amekataza watu kuwatoza wenzao nauli kubwa, kulangua vyakula na kadhalika. Inawezekana asiyetii onyo lake anadhurika,” alisema John Piwee, mmoja wa watu waliokuwa wakisubiri kunywa dawa hiyo.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa, vumbi lililotanda eneo hilo lilifanya madereva wasione mbele na matokeo yake magari mawili yakagongana uso kwa uso.
Magari hayo ni lenye usajili namba T606 ABU lililokuwa likiendeshwa na Zakayo Laizer na T681 ABX, lililokuwa likiendeshwa na Beatus Kiboa. Madereva wote wawili walifariki dunia pamoja na watu wengine watatu na jumla ya watu 14 walijeruhiwa.

 VIONGOZI WA DINI
Naye Mwinjilisti wa KKKT, Samunge Daniel Mbario wa kanisa lililokuwa likiongozwa na Mchungaji Mwasapile, ameiomba serikali iwe bega kwa bega na mtumishi huyo wa Mungu katika kuboresha mazingira ya barabara ili wagonjwa wafike kwa urahisi.
Kwa Msaada Wa Global Publisher Tanzania

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages