MOROGORO YATOA TASWIRA YA HUJUMA ZA PEMBEJEO ZA KILIMO - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MOROGORO YATOA TASWIRA YA HUJUMA ZA PEMBEJEO ZA KILIMO

 Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mkoa wa Morogoro,Fatma Mwassa(katikati),akipitia vitabu vya vocha za ruzuku ya pembejeo za kilimo ya mbolea na mbegu,vilivyohujumiwa kufuatia wananchi 219 kati ya 225 kusainishwa na kupewa sh 10,000 bila kupewa pembejeo hizo baada ya kurubuniwa na Wakala wa Usambazaji wa vocha katika Kata ya Doma.Tukio hilo lilitokea Desemba 31,mwaka jana.
------


 WIZARA ya Kilimo, Chakula na Ushirika katika mwaka huu wa fedha imetenga Sh bilioni 118 kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa mikoa 20 na wilaya 68 Tanzania Bara.

Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa iliyopewa kipaumbele katika mgawo wa fedha hizo. Ni miongoni mwa mikoa iliyotengewa kiasi kikubwa za fedha ili kutekeleza mpango wa kilimo kwanza kwa ufanisi mkubwa ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliotangulia.


Sababu ya kupewa kipaumbele ni kutokana na mkoa huo kuwa na sifa nzuri ya uzalishaji mazao kiasi cha kuishawishi serikali kuufanya mkoa huo kuwa ghala la taifa la chakula.


Mkoa wa Morogoro katika mwaka huu wa fedha wa 2010/2011 umepata mgawo wa vocha 422,118, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero imepata vocha 87,531, Kilosa (63,333), Morogoro Vijijini (61,497, Mvomero (103,152), Ulanga (74,592) na Manispaa ya Morogoro (32,013).


Mgawo huo ni mkubwa ikilinganishwa na mikoa mingine ambayo haikupewa kipaumbele na serikali kama ilivyo kwa mkoa huo. Mkakati huo wa serikali ulikuwa katika hati hati kufanikiwa iwapo viongozi wa serikali wa mkoa huo wasingekuwa makini katika ufuatiliaji wa mwenendo wa usambazaji wa pembejeo hizo uliokuwa ukifanywa na mawakala kupitia mfumo wa Vocha.


Viongozi wa serikali mkoani humo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Kanali mstaafu Issa Machibya, walibaini kuwa baadhi ya madiwani na viongozi wa serikali kutoka ngazi ya vijiji, kata hadi tarafa walihusika katika uhalifu huo wa kuhujumu utaratibu wa usambazaji wa pembejeo.



Habari hii na  Neophitius Kyaruzi

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages