FemAct YATAKA WAHUSIKA WA MILIPUKO GONGO LA MBOTO WAWAJIBISHWE - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

FemAct YATAKA WAHUSIKA WA MILIPUKO GONGO LA MBOTO WAWAJIBISHWE

Mkurugenzi wa TGNP, Usu Mallya.
Na Walusanga Ndaki
MUUNGANO wa mashirika yapatayo 50 nchini yanayotetea usawa wa kijinsia, haki za binadamu, na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FemAct) umetoa wito kwa serikali kuwawajibisha wote waliohusika katika mlipuko wa mabomu katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) namba 511 Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam uliotokea Februari 16 mwaka huu.

Katika taarifa yake iliyotiwa saini juzi na Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa niaba ya FemAct, Usu Malya, na kusambazwa kwa vyombo vya habari, muungano huo ulieleza masikitiko yake kwamba tukio kama hilo limetokea tena baada ya takribani mwaka mmoja ambapo wahusika waliuahidi umma kwamba lisingetokea tena.

“Tunawataka viongozi wanaohusika na masuala ya usalama wa kijeshi ambao waliahidi kuwa tukio kama hili halitatokea tena na sasa limejirudia wawajibike kwani imeonyesha kuwa wameshindwa kutimiza wajibu wao,” ilisema taarifa hiyo.

Miongoni mwa mambo mengine ambayo muungano huo umesisitiza ni pamoja na serikali kuwatafuta watoto wote waliopotea kutokana na janga hilo, kuwalipa fidia kamili watu wote walioathirika na janga hilo, kuyahamisha makambi ya jeshi kutoka mjini, kuwafidia wenye nyumba wote na wapangaji wao bila ubaguzi kwa hasara walizopata, na taarifa ya tume iliyoundwa kushughulikia janga hilo iwekwe wazi.

“Masikitiko yetu yanatokana na ukweli kuwa takribani mwaka mmoja na miezi kadhaa iliyopita ambapo Watanzania wenzetu eneo la Mbagala walipoteza uhai wao, huku wakazi 18,866 wakiathirika kwa namna moja au nyingine,  na kutokea uharibifu mkubwa wa mali kwa mlipuko wa mabomu na kupelekea wananchi 3,775 kukosa makazi,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza: “Femact imesikitishwa na tukio hilo lililotokea kwani linaonekana ni la kizembe kwa kuwa tayari mwaka 2009 lilikwishatokea na lilikuwa ni funzo kwa wahusika kuchukua hatua mathubuti.”

Kuhusu tukio la Gongo la Mboto, FemAct imesema maafa yake yamekuwa ni makubwa zaidi na kuenea katika eneo kubwa zaidi ambalo limehusisha vifo vya watu zaidi ya 25, majeruhi zaidi ya 300 mbali na kupotea kwa maelfu ya wanafamilia na uharibifu mkubwa wa mali ambao umewaacha watu wengi wakiwa hawana msaada mbali na kuwaathiri kisaiokolojia.

“Tunaitaka serikali kuhamisha maghala yote ya silaha ambayo yamewekwa karibu na makazi ya wananchi na kuyapeleka nje ya mji. Pia, wajenge maghala salama,” ilisema taarifa hiyo na kutoa rai kwa serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama kutoa taarifa sahihi kwa wananchi na si vinginevyo kuhusu milipuko hiyo.

Femact ilitoa takwimu kadhaa za watoto waliopotea, kubakwa, kuzaa kabla ya wakati na ujauzito ulioharibika, na kutaka mamlaka zifanye uchambuzi  wa hali ya juu kuhakikisha majanga kama hayo hayatokei tena, sambamba na kuwapa wananchi elimu ya kujiepusha na matukio kama hayo.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages