FEMACT WATEMBELEA WAATHIRIKA WA MILIPUKO YA MABOMU YA GONGO LA MBOTO - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

FEMACT WATEMBELEA WAATHIRIKA WA MILIPUKO YA MABOMU YA GONGO LA MBOTO

 
Baadhi ya Majeruhi wa milipuko ya mabomu iliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania namba 115 Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, wakipata huduma katika Hospitali ya Temeke.
Na Walusanga Ndaki
MASHIRIKA yapatayo 50 yanayotetea usawa wa kijinsia, haki za binadamu, na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FemAct) juzi yalifanya ziara ya ghafla kutembelea waathirika  wa milipuko ya mabomu iliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania namba 115 Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi hiyo kwa vyombo vya habari, msafara huo uliongozwa na wakurugenzi wa mashirikia wanachama wa Femact na wafanyakazi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), kwa lengo la kuwapa pole waathirika, kuwajulia hali wagonjwa, kutoa mkono wa pole kwa familia zilizopoteza ndugu na jamaa zao na kupata taarifa sahihi juu ya tukio hilo kutoka kwa waliokumbwa na janga hilo.

Pamoja na kutembelea nyumba zilizopata madhara ya kudondokewa na mabomu,  uongozi wa Femact ulikutana na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Ilala Bi.

Elizabeth Kasesa, na kupata taarifa juu ya hatua inayoendelea ya kuwahamishia watoto ambao hawajachukuliwa na ndugu zao katika eneo la Shule ya Msingi Mzambarauni, Ukonga.

Femact walitembelea pia majeruhi waliolazwa katika hospitali za Temeke, Amana na kambi ya watoto wadogo iliyoko viwanja vya Saba Saba.

Akizungumzia milipuko hiyo, Mkurugenzi wa TGNP, Usu Mallya, alisema hilo lilikuwa tukio la kusikitisha ambalo Femact imelichukulia kama msiba wa kitaifa na kila Mtanzania anapaswa kuguswa nao kwa namna ya pekee ili kuwafariji kwa kila njia wananchi  waliokumbwa na tatizo hili.
 
“Ukiangalia kwa karibu utagundua kuwa walioathirika kwa kiasi kikubwa ni wanawake, wazee, watoto na walemavu, ambapo akina mama hasa wajawazito wameathirika zaidi.  Ni lazima jamii nzima ilione hili na tuchukue hatua za dhati za kusadiana,” alisema na kuongeza:

“Kazi yetu kubwa sisi wanaharakati ni kutafakari kwa kina juu ya tatizo hili, na sababu za kutokea kwa mara ya pili; lilitokea Mbagala miaka miwili haijaisha na sasa limetokea tena hapa hapa Dar es Salaam, ni lazima tujue chanzo na tuhoji ni kwa nini tusiyadhibiti matukio haya.

Tume iliyoundwa wakati wa Mbagala iliapa kuwa hayatatokea tena lakini yametokea,” alisema kwa masikitiko.

Mallya alisema kutokana na madhara makubwa yaliyotokana na milipuko hiyo, serikali ichukue hatua za haraka kuhakikisha kuwa raia wote waliokimbia makazi wanawezeshwa kurejea  mapema  na kuendelea  na shughuli zao.

“Ambao hawaonekani watafutwe misituni na katika mabonde ya mto Msimbazi ili wapatikane,” alisisitiza.
 Alisema kutokana na hofu na jinsi tukio lilivyotokea, watoto wengi na hata watu wazima wameathirika kisaokolojia kwa hiyo kunahitajika hatua madhubuti za kuwasaidia ili waweze kupona na kurejea katika hali ya kawaida.

Aidha Mallya amesema Femact inafanya uchambuzi yakinifu na tayari imeunda kikosi kazi kitakachofanya uchambuzi huo kutaka kujua ni kwanini masuala hayo yanaendelea na baada ya hapo Femact itatoa tamko kamili kuhusu tukio hili na ikibainika kuna uzembe itadai uwajibikaji kwa viongozi wanaohusika.

Naye Mkurugenzi wa The Leadership Forum, Hebron Mwakagenda, alisema wanaharakati wanashindwa kuelewa ni kwa nini majanga yanapotokea serikali inakimbilia kuunda tume ambazo hata hivyo ripoti zake zinaishia kuwa siri.

Mwakagenda amehoji wapi ilipo ripoti ya milipuko ya Mbagala na kusema kuwa tume zinapoteza muda na fedha za wananchi kwenye vikao badala ya kutafuta dawa ya tatizo.

“Kwenye majanga hatuundi tume tunaunda kikosi kazi, na kinatakiwa kutoa ripoti yake hadharani siyo kuiweka kabatini, vikao vipungue  viongozi wajitokeze kuwasaidia wananchi walioathirika,” alisema Mwakagenda.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wanawake wanaopambana na Ukimwi (WOFATA), Neema Duma, alisema  madhara yamekuwa makubwa kutokana na serikali kukosa mfumo sahihi wa kutoa taarifa za majanga kwa wananchi wake.

Alisisitiza kwamba majanga yanapotokea serikali haichukui jukumu la kuwaeleza wananchi kwa kauli moja na iliyo sahihi  kuhusu ni kitu gani kinaendelea na hatua gani za kuchukua.
Mkurugenzi wa TGNP, Usu Mallya.
“Tukio limetokea usiku, hakuna kauli moja iliyotoka; polisi, jeshi  waziri kila mmoja alitoa kauli na kuzidi kuwachanganya wananchi.  Tunahitaji kuwepo na mfumo wa kueleweka ili kuwaunganisha wananchi na kuepusha madhara zaidi, ” alisema.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages