WAGE AKIRI KUMPA RUSHWA JERRY MURRO - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

WAGE AKIRI KUMPA RUSHWA JERRY MURRO

Jerry MURO
---
Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa watatu upande wa Jamhuri katika kesi ya kuomba rushwa ya sh milioni 10 inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la (TBC1) Jerry Murro, na wenzake Michael Wage amekiri kutoa rushwa ya sh milioni moja baada ya kutishiwa bastola na pingu.

Wage alitoa maelezo hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe wakati akiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Boniface Stanslaus.

Alidai kuwa alilazimika kutoa rushwa hiyo kwa sababu alitishwa na Murro na mshtakiwa wa pili Kapama aliyejitambulisha kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa PCCB na mshtakiwa wa tatu Deo Mgassa alijitambulisha kuwa ni msaidizi wa mkurugenzi huyo.

Shahidi huyo ambaye alikuwa mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kabla ya hajasimamishwa kazi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Januari mwaka jana, alidai kuwa washtakiwa hao wote watatu Januari 31 mwaka jana, katika Hoteli ya Sea Cliff walimtaka awapatie sh milioni 10 ama sivyo wangembambikia kesi kama alivyobambikiwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, kwa kumwambukiza maradhi mpenzi wa rafiki wa Kapama ndiyo maana akabambikiziwa kesi iliyomfanya ahukumiwe kwenda jela miaka miwili.

Wage aliieleza Mahakama kuwa Januari 28 mwaka jana akiwa nyumbani kwake Bagamoyo alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa mtangazaji wa TBC1 na hakuwa hakimfahamu, akimtaka kesho yake aje Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kwani amepata taarifa kuwa anakabiliwa na tuhuma za ufisadi katika Halmashauri ya Bagamoyo.

Katika hilo Wage alieleza kuwa alikubaliana na ombi hilo na Januari 29 mwaka jana, saa tano asubuhi alifikia katika mgahawa wa Califonia ulioko jijini hapa akiwa na dereva wake.

Alisema akiwa njiani alimpigia simu Murro ili aje aungane naye na baada ya dakika chache Murro aliwasili katika mgahawa huo akiwa na gari ndogo na akamweleza watafute meza nyingine ili wakae mbali na dereva wake na walipohamia kwenye meza nyingine ndipo Murro alipoanza kumueleza tuhuma za ufisadi zinazomkabili na kwamba anataka kuzitangaza kwenye kipindi cha Usiku wa Habari kinachorushwa na TBC1.

“Baada ya Murro kunieleza tuhuma hizo akaniambia mahojiano kamili yangefanyika katika Hoteli ya Sea Cliff kwani huko ndiko walikokuwa mabosi wake na kunitaka nimwache dereva wangu kwenye mgahawa huo nikapande gari lake twende nae Sea Cliff na nilifanya kama alivyonielekeza nikapanda na tulipokuwa njiani akampigia simu mtu akawa anazungumza naye na akanitaja jina langu… alivyokata simu nikamuuliza ni kwa nini alikuwa akitaja jina langu akasema alikuwa akizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa PCCB (Kapama) naye pia atanihoji.

“Kitu kingine wakati nilipokuwa ndani ya gari hilo tukielekea Sea Cliff, Murro aliniambia yeye ni ofisa wa jeshi na ana nyota tatu na amechukua mafunzo nchini Marekani na Afrika Kusini na ana madaraka ya kunikamata… na baada ya hapo alifungua dashibodi ya gari lake akatoa pingu akaniambia nikimletea vurugu atanifunga na pingu na kisha akanionyeshea bastola pia akaniambia nikifanya vurugu atanifyatulia risasi ili kunidhibiti,” alieleza.

Wage aliendelea kueleza kuwa walipofika tu Hoteli ya Sea Cliff walipokelewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa PCCB, anaitwa Mussa ambapo hata hivyo Wage alimtambua mtu huyo mahakamani kuwa ni Mugassa na akaongeza mtu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Dokta ambaye Wage jana alimtambua mahakamani kuwa ni Kapama na kuongeza kuwa baada ya hapo mahojiano yakaanza na Dokta akaanza kumueleza kuwa yeye ni fisadi mkubwa na kwamba kama alihitaji msaada wao angesema mapema ili mahojiano yao yasiweze kurushwa kwenye kipindi cha Usiku wa Habari cha TBC1.

“Niliwajibu mimi siyo fisadi; ndipo yule Dokta (mshtakiwa wa pili) akaniambia kuwa hata Liyumba alifungwa jela kwa kuonewa kwani ile kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma, alibambikiziwa kwa kuwa alikuwa akitembea na mpenzi wa rafiki yake anayefanya kazi BoT akamwambukiza maradhi… nilipokea taarifa hiyo kwa mshtuko mkubwa na nikaona wanaweza kunibambika kesi watu hao na siku hiyo nilikuwa na sh milioni moja mfukoni ikabidi nimpatie kiasi hicho cha fedha Kaimu Mkurugenzi wa PCCB (Kapama), mshtakiwa wa pili, ndani ya gari na Murro alikuwa nje ya gari na kuwaahidi kesho yake Januari 31 mwaka jana ningewaletea sh milioni tisa zilizokuwa zimebaki.

“Baada ya kumaliza kuwapatia sh milioni moja, niliingia kwenye gari la Murro akaenda kunishusha mgahawa wa Best Bite na tutakubaliana kesho yake tukutane kwenye mgahawa wa City Garden ulioko mtaa wa Mkwepu… Nikapanda kwenye gari langu nikaenda nyumbani kwangu Bagamoyo nikawaeleza ndugu zangu kuhusu tukio la mimi kutishiwa bastora na kuombwa rushwa; wakaniambia nikatoe taarifa polisi….na kweli Januari 31 mwaka jana, nilivyokuja Dar es Salaam nilifikia moja kwa moja kituo kikuu cha Polisi Kati huku mfukoni nikiwa na sh milioni tisa,” alidai Wage.

Alisema mara baada ya kutoa taarifa hizo polisi wakamtaka ampigie simu Murro na amweleze kuwa tayari ameishafika kwenye mgahawa wa City Garden.

Wage alieleza kuwa alifanya hivyo na baada ya dakika chache Murro aliwasili kwenye mgahawa huo lakini alivyomuona Wage ameambatana na watu wengine watatu alishtuka na polisi waliwahi kuzuia gari lake lisitoke katika viwanja vya mgahawa huo na askari kanzu hao walimwamuru aendeshe gari lake na kulipeleka kituo cha polisi Kati na Murro alitii amri hiyo na wote walifika kituoni hapo.

Alisema Murro alipoulizwa kama alikuwa akimfahamu Wage alikana kumfahamu na polisi hao walipopekuwa gari la Murro walikuta bastola, pingu na miwani ya kusomea ambayo Wage alidai ni yake na aliisahau jana yake wakati alipopanda katika gari hilo wakati anapelekwa Sea Cliff.
Vitu hivyo vyote pingu, bastola na miwani ilipokelewa mahakamani hapo kama utambulisho.

Kwa upande wake wakili wa Murro, Richard Rweyongeza, na Majura Magafu, anayemtetea Kapama na Muggasa akimhoji shahidi huyo alidai kuwa shahidi huyo haoni kwamba Murro alikuwa akitangaza habari za hatari hatari za kuligusa jeshi la polisi na alikuwa akitaka kurusha tuhuma za ufisadi zinazomkabili Wage ndiyo maana alishirikiana na polisi kumbambikizia kesi mteja wake, hoja hiyo ilipingwa vikali na shahidi huyo. Leo shahidi wa nne ataanza kutoa ushahidi wake.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages