TAMBWE HIZA: UCHAGUZI WA ARUSHA HAUTARUDIWA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

TAMBWE HIZA: UCHAGUZI WA ARUSHA HAUTARUDIWA

 NAIBU Mkuu wa Kitengo cha Propaganda cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tambwe Hiza(Pichani) amesema chama hicho hakipo tayari kurudia uchaguzi na wataendelea kumtambua Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lymo kwa sababu ameshinda uchaguzi kihalali.

Akizungumza leo, Hiza alisema kuwa msimamizi wa uchaguzi alisimamia uchaguzi huo halali na ni huyo ambaye alimtangaza Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), pamoja na madiwani wanane walioshinda katika uchaguzi mkuu.


Alisema kama msimamizi huyo angekuwa na njama zozote asingewatangaza viongozi wa Chadema walioshinda katika uchaguzi mkuu akiwemo Mbunge wa jimbo hilo.


“CCM ingeshtuka sana kama Meya wetu angejiuzulu maana amechaguliwa kihalali... Chadema wajipange upya maana bado wananchi hawajawataka kwa sasa na ndiyo maana wameipa CCM kura nyingi kwa viti vya madiwani,” alisema.


Alisema CCM haikuwa na njama za kuiba kura kama inavyodaiwa kwa sababu wao walikuwa na viti vingi vya udiwani kuliko Chadema na kusisitiza kwamba uchaguzi huo hauwezi kurudiwa kwa sababu meya alipatikana kihalali.


Kuhusu madai ya Mbunge wa Viti Maalum, Mary Chatanda kwamba ni Mbunge wa Tanga, Hiza alisema kawaida hakuna mbunge wa Viti Maalum mwenye jimbo kwa mujibu wa sheria inavyoelekeza.


Wakati huo huo, Chama cha Tanzania Labour (TLP) kimempongeza aliyekuwa Naibu Meya wa Jiji hilo, Michael Kivuyo (TLP) kwa kujiuzulu wadhifa huo na kumtaka Meya kufuata nyayo hizo ili kuepusha damu isimwagike tena.Habari hii na Picha na Mdau Richard Mwaikenda

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages