SABABU 7 ZINAZOKUFANYA UKOSE MPENZI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

SABABU 7 ZINAZOKUFANYA UKOSE MPENZI

Naamini wapo wapo watu wengi huko mtaani ambao wako ‘singo’ nikimaanisha kwamba hawana wapenzi. Ni jambo linaloumiza sana tena maumivu yake yanaongezeka pale utakapowaona wenzako wakiyafurahia maisha yao ya kimapenzi.

Yawezekana wewe unayesoma makala haya huna mpenzi na umekuwa ukijiuliza sababu bila kupata majibu. Unaweza kwenda mbali zaidi na kuhisi una mkosi.

Huenda Mungu hajapanga kukupatia mpenzi kwa sasa lakini yawezekana wewe mwenyewe unachangia kuwa mpweke. Hapa yapo mambo saba ambayo inawezekana yakawa ndiyo sababu ya kukufanya uwe singo mpaka sasa.

1. Unajifanya matawi ya juu
Ili kumpata mtu wa kuwa nawe maishani, hutakiwi kuwa mchaguzi sana. Wapo wanaume/ wanawake huko mtaani ambao wanajifanya matawi ya juu sana, kila anayewatokea huona hana vigezo, matokeo yake ni muda kusonga huku wakikosa wale ambao wana vigezo wanavyovitaka.

Hivyo basi, ifike wakati anayekuja mbele yako hata kama hana vigezo vyote umkubalie laa sivyo utaendelea kuishi bila mpenzi.

2.Unafikiri walivyoumizwa wenzako
Huenda una rafiki au ndugu yako ambaye ameumizwa sana na mapenzi. Amekuwa ni mtu wa kulia kila siku sababu ya mapenzi.

Kama uko karibu na mtu wa aina hiyo inaweza kukuwia vigumu kukubali kuingia kwenye uhusiano na mtu yoyote atayekuja mbele yako.

Utakuwa ukidhani na wewe utaumizwa, jambo ambalo hutaki likutokee katika maisha yako.
Cha msingi ni kuchukulia kwamba, hayo hayawezi kukutokea. Mpe nafasi mtu unayempenda kisha amini kwamba wewe ni miongoni mwa wale ambao kamwe mapenzi hayawezi kuwaliza.

3. Hujichanganyi
Hii pia yaweza kuwa sababu ya wewe kuendelea kuwa mpweke hadi leo. Huenda unafanya kazi katika mazingira ambayo hakuna mtu anayeweza kuwa mpenzi wako.

Lakini pia unakuwa siyo mtu wa kutoka na kwenda sehemu mbalimbali. Yaani ukitoka kazini ni nyumbani, ukitoka nyumbani ni kazini.

Kama uko katika mazingira haya ni vigumu kupata mpenzi hivyo ni vyema ukaanza kuwa mtu wa kujichanganya, naamini utakutana na watu ambao mioyo yao ni mipweke kama wako na kuungana nao.

4. Tabia zako
Yawezekana wewe ni mkali au huna tabia nzuri. Watu watakukwepa na hakuna atakayekuwa tayari kuwa na wewe.

Jichunguze vizuri tabia zako na kama unaona ni chanzo cha wewe kutopata mpenzi, badilika. Maisha bila mpenzi hayawezi kuwa ya furaha kwako.

5. Siyo mcheshi
Unajua nini? Moja ya sababu inayowafanya watu kuwavutia wengine ni ucheshi wao. Yawezekana wewe ni mtu wa kuwa siriasi kila wakati, utampata nani wa kuwa na wewe?

Nani anapenda kuwa na mtu ambaye inapita nusu saa hajamfanya atabasamu? Tambua kwamba kama si mcheshi, kupata mpenzi itakuwa ngumu sana.

6. Uko rafu sana
Ni kweli mapenzi hayachagui lakini wakati mwingine kuna vitu vinaweza kukukosesha mpenzi hivi hivi. Huenda wewe ni mtu rafu sana, umeamua kuwa hivyo lakini je, wanawake/wanaume wanaokuzunguka wanavutiwa na muonekano wako?

Kama siyo unadhani nani atakukubali utakapomtokea na kumtaka kimapenzi au nani utamfuata na kumtaka awe mpenzi wako na akakukubalia? Itakuwa ngumu kwa kweli, jiangalie upya!

7.Hujaamua tu
Kwa maisha ya sasa na ulimwengu unavyokwenda, kupata mpenzi kama unadhamiria siyo kazi ngumu na ndiyo maana nikasema yawezekana hujaamua kuchagua.

Hebu leo amua kwamba nataka mtu wa kunipa furaha halafu uone kama utamkosa. Ukimkosa nipigie simu mimi nitakusaida kumpata mtu atakayekuwa mpenzi wako.
Kwa Msaada Wa GLOBAL PUBLISHER  TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages