IKULU: RAISI KIKWETE SIO MMILIKI WA DOWANS KAMPUNI YA KUZALISHA UMEME - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

IKULU: RAISI KIKWETE SIO MMILIKI WA DOWANS KAMPUNI YA KUZALISHA UMEME



Rais Jakaya Mrisho Kikwete
 -------------
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Wilboard Slaa,juzi, Jumapili, Januari 2, 2011, amekaririwa na Gazeti la Tanzania Daima, linalomikiwa na chama chake hicho, akidai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ni mmoja wa wamiliki wa Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Dowans.

Huu ni uongo wa mchana,ni uzushi wa karne na propaganda ya hatari.Kwa hakika na kwa namna isiyoweza kuelezeka kwa ufasaha,tumeshtushwa sana na kauli hii ya Dkt. Slaa na hatutaki kuamini kabisa wala kukubali kuwa ni kweli kauli hii imetolewa na mtu ambaye majuzi tu alikuwa akiwania kuwa kiongozi wa juu wa taifa letu,yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na kama kweli Dkt.Slaa ametoa kauli hii na kusema maneno ya namna hii basi sasa Watanzania wanayo kila sababu na haki ya kuamini kuliko wakati mwingine wowote kuwa mzee huyu sasa amechanganyikiwa na ni mtu wa hatari sana kwa utulivu wa nchi hii.Kwa nini?

Sababu ni rahisi sana.Mheshimiwa Rais Kikwete siyo mmiliki wa Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Dowans. Hakupata kuwa mmiliki, siyo mmiliki na wala hatakuwa,hata siku moja, mmiliki wa Kampuni hii.

Kama Dkt.Slaa anataka kweli kujua wamiliki wa Kampuni ya Dowans,basi atafute ukweli huo na aachae tabia ya kutapatapa na udhabinadhabina yenye lengo la kuwapaka watu watope. Tabia ya kuwasingizia na kusema uongo kuhusu viongozi wa taifa letu ni tabia ya hatari.

Mheshimiwa Rais Kikwete hahusiki na Kampuni ya Dowans wala na kampuni nyingine yoyote ya kibiashara. Yeye ni kiongozi wa juu kabisa wa siasa wa nchi yetu na siyo heshima wala haki kumhusisha na jambo la kutunga na kuzua na lisilokuwa la ukweli wowote.

Kiongozi huyo wa upinzani ametoa shutuma zake dhidi ya Rais Kikwete kufuatia Kampuni ya Dowans kulishitaki Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) na Mahakama hiyo ikaamua kuwa Dowans ilipwe kiasi cha sh bilioni 185.

Dkt. Slaa amezomoko na kumshutumu Rais Kikwete eti kwa sababu Mheshimiwa Rais hakuzungumzia suala hilo katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wananchi Ijumaa iliyopita.

Mwaka huu, Dkt Slaa aliwania urais wa Tanzania kupitia CHADEMA na akashindwa vibaya sana. Tokea wakati huo amekuwa mtu wa kutunga na kuzua stori za kila aina ya uongo na umbea kuwachanganya Watanzania kwa sababu ya kinyongo chake cha kushindwa.

Tunapenda kuwataka na kuwaomba Watanzania, kama ambavyo wamekuwa wanapuuza uongo na uzushi mwingine wa mara kwa mara wa Dkt. Slaa, waupuuze uzushi na uongo wa sasa kuhusu miliki ya Dowans. Ni sehemu ya tabia iliyoanza kuzoeleka sasa ya Mzee huyo kutapatapa kisiasa.
Imetolewa na
Salva Rweyemamu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais
  Ikulu

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages