AFYA, POLISI, MAHAKAMA, ARDHI NI VINARA WA RUSHWA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

AFYA, POLISI, MAHAKAMA, ARDHI NI VINARA WA RUSHWA

 
Utafiti uliofanywa na asasi binafsi ya Fordia, umebaini kuwa vitendo vya rushwa vimekithiri kwa kiwango kikubwa katika utoaji wa huduma za afya kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitalini.

Mkurugenzi wa Asasi hiyo, Bubelwa Kaiza (pichani kulia) , alisema hayo jana kwa waandishi wa habari wakati akizungumzia utafiti uliofanywa na asasi yake kwenye mikoa mbalimbali nchini mwaka 2008-2010.

Alisema Jeshi la Polisi, linafuatia malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuwa huduma zake zimetawaliwa na rushwa.

Kaiza alisema Idara ya Mahakama, nayo imelalamikiwa na idadi kubwa ya Watanzania kuwa utoaji wa haki umekuwa mgumu na mara nyingi kumekuwa na vitendo vya rushwa.

Alisema wananchi wengi waliozungumza na watafiti, walisema hulazimika kutoa rushwa ili kupata huduma wanazopaswa kuzipata bila fedha. Kaiza alisema sehemu nyingine iliyotajwa kwamba, rushwa imekithiri ni katika ardhi na upatikanaji wa leseni za biashara.

Alisema hata Shirika la Umeme nchini (Tanesco) limelalamikiwa na wananchi wengi kuwa upatikanaji wa umeme umekuwa mgumu na wakati mwingine wananchi wanalazimika kutoa rushwa ili kupata huduma hiyo.

Kuhusu jitihada za kupambana na rushwa zinazofanywa na serikali, alisema hazitoshi kwani vitendo vya rushwa bado vinaongezeka.

Alisema ingawa serikali ilifanya marekebisho ya Sheria ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), adhabu zinazotolewa na taasisi hiyo kwa watu wanaokutwa na hatia, ni ndogo na hazilingani na makosa yanayofanyika.

“Ukali haupo kwenye adhabu zinazotolewa na hiyo inaweza kusababisha vitendo vya rushwa kuendelea. Mfano kifungo cha miaka mitatu au minne jela ni kidogo sana kwa makosa ya rushwa,” alisema.

Aliongeza: “Mfano ofisa anayesimamia uchaguzi akitangaza kwa makusudi matokeo, ambayo si halali hakuna hatua anazochukuliwa. Huu ni upungufu mkubwa, ambao lazima serikali iufanyie kazi.”

Alisema siku hizi kuna taasisi zimeanzishwa kwa ajili ya kuwa wakala wa kupokea rushwa kwa niaba ya wahusika.

Alisema watu hao wamekuwa wakifanya hivyo ili kuwaficha watoaji na wapokeaji wa rushwa wanaohusika kwenye mashauri mbalimbali.

“Kuna watu, ambao hawahusiki katika shauri. Wanakwenda mfano polisi au mahakamani kuongea na hakimu ili kuhonga kwa niaba ya wale wanaohusika. Na hilo linafanyika ili kuwakinga wahusika wasikamatwe na rushwa,” alisema.
    CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages