MAGGID MJENGWA USO KWA USO NA DR SLAA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MAGGID MJENGWA USO KWA USO NA DR SLAA

 Maggid Mjengwa  akiwa na Dk Wilbrod Slaa(Chadema) jana Mikumi
 Maggid Mjengwa akiwa na Yusuph Makamba(CCM)
--------
Tukiwa Kikoboga Camp, Mikumi, jana na leo nimepata bahati ya kuongea kwa karibu na Dr Willibrod Slaa, Katibu Mkuu ( CHADEMA). Leo kabla ya mlo wa mchana tuliongea kwa kirefu. Mazungumzo yalikuwa ni ya kirafiki sana. Tulikumbushana tulipokutana mara ya kwanza, mwaka 2004 mwezi Julai. Wakati huo, rafiki yangu Zitto Kabwe ndiye aliyenitambulisha kwa Dr Slaa pale zilipo ofisi za CHADEMA, Kinondoni.

Dr Slaa: " Maggid, umetuchukia CHADEMA, tangu nikuone wakati ule hujaja tena kwetu!"

Mimi: " Hapana Dr, naishi Iringa, ni mbali na Dar. Ningependa nionane mara kwa mara na wanasiasa, lakini nashindwa. Hata Mzee Makamba nimeonana nae mara moja mwaka 2007. Mpaka hii leo hatujakutana tena. Nimemwona leo hapa mbugani akiwa kwenye gari, nimempungia mkono tu".

Wakati nikimpa majibu hayo Dr Slaa, kichwani nafikiria, hata Profesa Lipumba nimeonana nae mara moja tu, mwaka 2005, tangu wakati huo hatujatiana machoni. Na James Mbatia namsoma tu magazetini, ningependa nikutane nae siku moja.

Kisha Dr Slaa na mimi tunajikita kwenye mazungumzo ya siasa. Namweleza Dr Slaa;

" Dr, naamini tumefanya kosa kubwa kama nchi mara ile tulipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi bila kuifanyia marekebisho katiba ya nchi yetu. Tuliwaamini wanasiasa wetu, lakini sasa tunaona, kuwa wanatuangusha. Ufisadi umetamalaki, baadhi yao ndio wenye kushiriki ufisadi huo, na Katiba inawalinda. Tunahitaji marekebisho makubwa ya Katiba yetu".

Dr Slaa: " Ni kweli kabisa".

Kisha Dr Slaa anachambua kwa undani kwa kutoa mifano. Mazungumzo yamepamba moto. Iko siku nitarejea mazungumzo yangu na Dr Slaa kuhusu hili la Katiba na mengineyo.

Na

Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages