Yanga yatangaza milioni 40 motisha kuiua Simba - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Yanga yatangaza milioni 40 motisha kuiua Simba

KAMATI ya mashindano ya klabu ya Yanga imetenga Shilingi  40 milioni kwa timu yao endapo itaifunga  Simba katika mchezo wao utakaofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Mwenyekiti wa klabu hiyo , LIoyd Nchunga aliiambia Mwananchi jana kuwa kamati hiyo imeamua kutenga fedha hizo kwa ajili ya kuwahamasisha wachezaji  na benchi la ufundi kutokana na ushindani mkubwa ulioko katika mchezo huo.

Alisema kuwa katika kiasi hicho cha fedha, kila mchezaji atazawadiwa  milioni moja huku benchi la ufundi wakipata zaidi ya Sh700,000 na kocha wao, Kostadin Papic  akiahidiwa Sh 1.5m na tiketi ya ndege ya kwenda na kurudi Serbia kwa ajili ya sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Alisema kuwa timu yao inaondoka Dar es Salaam Jumamosi asubuhi kwa ndege ya kukodi na baada ya mchezo huo kumalizika itarudi Dar es Salaam.

Pia, Nchunga aliongeza kuwa  kamati hiyo itawawezesha baadhi ya wazee wa klabu hiyo kwenda Mwanza kwa ajili ya kuiombea dua timu yao ili iweze kufanya vizuri.

Naye ofisa  habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema jana kuwa wao hawana presha na mechi hiyo na kocha wao Papic amekuwa na kazi kubwa ya kuwaondolea presha wachezaji wake  ili wauone mchezo huo kama  ilivyo dhidi ya Manyema, Majimaji au Toto African.

'' Mechi hiyo ni ya kawaida kwani Simba siyo timu ya kutisha kihivyo , tumeiona kwenye ligi, hakuna timu mechi hata moja waliyoshinda bao zaidi ya mabao mawili, hivyo uwezo wa kuifunga tunao,'' alieleza Sendeu.

Alisema kuwa timu yao iko fiti na wanamshukuru Mungu kuona kuwa haina majeruhi  na wachezaji wake wote wako katika hali nzuri na wana ari kubwa ya mchezo huo.

Kwa upande wao, Simba wametamba kuwa wataifunga Yanga keshokutwa mjini Mwanza kutokana na kuzijua  njia  zote wanazofanya wapinzani wao.

Kauli hiyo imetolewa wakati Yanga  ikiwafuata watani zao Simba Jumamosi tayari kwa mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Ofisa habari wa Simba, Clifford Ndimbo alisema jana kuwa wao wako tayari kwa mechi hiyo na wamejiandaa vizuri kuwakabili Yanga kwani hawatafanya makosa kama waliyofanya katika michuano ya Tusker.

Alisema kuwa watani wao wamekuwa wakifanya njia za ujanja ujanja ili waweze kushinda mchezo huu, lakini wao wamezijua njia zote wanazofanya  wapinzani wao Dar es Salaam na Mwanza.

"Watambue kuwa Simba inao mtandao mkubwa na kama watataka kutumia njia hizo kuifunga wajue wameshindwa kwani tumejua kila kitu kinachoendelea na sisi tunawasubiri uwanjani," alisema Ndimbo.

Alisema mchezaji wao  mahiri, Mussa Hassan  Mgosi huenda akakosa  mechi hiyo kutokana na hali yake kwani mpaka sasa bado haijawa nzuri.

Kocha wao, Patrick Phiri alisema kuwa ameshamaliza kazi na anasubiri mechi hiyo na kukiri kuwa itakuwa ngumu mno  hasakutokana na maandalizi ya pande zote.

Hata hivyo, viongozi wao wakijinadi kuwa watashinda mchezo huo baadhi ya wachezaji wa  klabu hizo mbili, wameeleza kuwa mechi hiyo ni ngumu japo ni lazima mmoja aibuke mshindi.

Nao ni  Jerryson Tegete (Yanga ) na Emmanuel Okwi (Simba) ambao kwa nyakati tofauti  jana kila mmoja alijigamba kuwa atazitikisa nyavu za mpinzani wake  Jumamosi.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages