TAARIFA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KUFUATIA AJALI YA KUZAMA KWA MELI YA MV SKAGIT ILIYOTOKEA TAREHE 18 JULAI, 2012, CHUMBE, ZANZIBAR - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

TAARIFA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KUFUATIA AJALI YA KUZAMA KWA MELI YA MV SKAGIT ILIYOTOKEA TAREHE 18 JULAI, 2012, CHUMBE, ZANZIBAR



THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425






PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KUFUATIA AJALI YA KUZAMA KWA MELI YA MV SKAGIT ILIYOTOKEA TAREHE 18 JULAI, 2012, CHUMBE, ZANZIBAR

          Jana tarehe 18 Julai, 2012, majira ya alasiri kumetokea ajali ya kuzama kwa meli ya MV SKAGIT katika eneo la Chumbe, Zanzibar.  Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kueleka Zanzibar ilikuwa imebeba watu 290. Kati yao watu wazima 250, watoto 31 na wafanyakazi wa meli 9.  

Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Muungano yaani JWTZ na  Polisi waanze kazi ya uokoaji mara moja.
          Kazi hiyo imefanywa kwa kushirikiana na vyombo vya usalama vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na meli za makampuni binafsi.  Mpaka giza lilipokuwa limeingia na hivyo kazi ya uokoaji kusitishwa mpaka kutakapokucha tarehe 19 Julai, 2012, watu 136 walikuwa wameokolewa na maiti 31 zilikuwa zimepatikana.  Aidha, mali zilizokuwa kwenye meli hiyo hazikuweza kuokolewa. 

          Kufuatia ajali hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano alizungumza na Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.  Alimpa pole kwa ajali iliyotokea hasa kwa vifo na majeraha waliyopata Watanzania wenzetu na watu wasiokuwa raia wa Tanzania.  Alimuomba afikishe salamu za rambirambi kwa ndugu zetu waliopotelewa na jamaa zao na kuwapa pole waliopata majeraha na maumivu maungoni mwao. Rais wa Jamhuri ya Muungano alisema kuwa huu ni msiba wetu sote na kwamba majonzi yao ni majonzi yake na ya Watanzania wote.  Kwa ndugu zetu waliojeruhiwa tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape ahueni na wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kujiletea maendeleo na kulijenga taifa letu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein na viongozi wote wa ngazi mbalimbali kwa uongozi wao thabiti tangu taarifa ya kutokea kwa ajali mpaka sasa.  Aidha, amewapongeza maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama na wafanyakazi wa meli binafsi, kwa juhudi kubwa walizozifanya za uokoaji wa ndugu zetu waliopatwa na maafa haya makubwa na ya aina yake.  Amewataka waendeleze juhudi hizo leo na siku zijazo.

          Rais amewataka wananchi wawe na moyo wa subira na uvumilivu wakati kazi ya uokoaji inaendelea.  Kama ilivyofanyika katika ajali ya MV Spice Islander miezi 10 iliyopita, uchunguzi wa kina utafanyika kubaini chanzo cha ajali.

          Kutokana na ajali hiyo na msiba huu mkubwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ametangaza maombolezo ya taifa ya siku tatu ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo, tarehe 19 Julai, 2012.
          Asanteni sana.


Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19  Julai, 2012

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages