Rais Jakaya Kikwete Kufungua Rasmi Mkutano wa 20 wa Bodi ya Magavana wa Afrika (ACBF) - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Rais Jakaya Kikwete Kufungua Rasmi Mkutano wa 20 wa Bodi ya Magavana wa Afrika (ACBF)


Katibu Mtendaji wa Bodi ya Magavana wa Afrika (ACBF) Dkt .Frannie Leautier(katikati) akiongea na waandishi wa habari leo mjini Arusha kuhusu kuanza kwa Mkutano wa 20 wa Bodi ya Magavana wa Afrika(ACBF) unaotarajiwa kufunguliwa na Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete siku ya Alhamis (8.9.2011). Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano(ACBF) Audrey Mpunzwana na kushoto ni Mtaalamu kutoka ACBF George Kararach.Picha na Tiganya Vincent-MAELEZO-Arusha 
---
Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 20 wa Bodi ya Magavana wa ACBF unaokwenda sanjari na mkutano wa tano wa viongozi waandamizi utakaojadili jinsi ya kujenga uwezo kwa nchi wanachama zitakazoshiriki. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika tarehe 07- 09 Septemba, 2011 katika Hoteli ya Mount Meru mjini Arusha.

Mkutano wa Magavana wa ACBF utafunguliwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzana Dkt Jakaya Mrisho Kikwete siku ya Alhamisi tarehe 8 Septemba 2011 mjini Arusha.
Mkutano utawashirikisha Mawaziri, washirika wa maendeleo na wadau wengine maarufu watakaojadili jinsi ya usimamizi mzuri wa misaada na mikopo barani Afrika na namna wanavyoweza kukabiliana na changamoto za ajira kwa vijana.

Mkutano wa Tano wa viongozi waandamizi utatangulia mkutano wa 20 wa Bodi ya Magavana wa ACBF ambao utaongozwa na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mustafa Haidi Mkulo.

Washiriki wa Mkutano wa Bodi ya Magavana wa ACBF ni Mawaziri wa Fedha, wahisani kutoka nchi wanachama wa Bodi ya Magavana(ACBF), viongozi waandamizi kutoka Benki ya Dunia(WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika(ADB) pamoja na Programu za Maendeleo zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Katika mkutano wa tano wa viongozi waandamizi, wasemaji wakuu wanatarajiwa kuwa Katibu Mtendaji wa ACBF Dkt. Frannie Leautier, Waziri wa maendeleo ya Uchumi, Mipango na Uchambuzi wa Sera Mh. Marcel De Souza kutoka Benin na Waziri Mkuu Mstaafu wa Mauritania Mh. Zeine Ould Zeidane ambao wataongoza mjadala juu ya changamoto za ajira kwa vijana barani Afrika na hatua gani zichukuliwe ili kukabiliana na changamoto hizo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo Afrika (Africa Development Institute) Bw. Victor Murinde kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Sera za Uchumi (SEP) Bi. Sue Szabo, Mshauri wa Utawala bora wa Benki ya Dunia Bw. Deryck Brown pamoja na Bw. George Kararach ambaye ni mtaalamu wa ACBF; wataongoza majadiliano kuhusu taarifa ya viashiria vya uwezo wa Afrika kuelekea mkutano wa Busan, Korea ya Kusini mwezi Novemba, 2011utakaojadili uratibu, usimamizi na ufanisi wa misaada. 

Mojawapo ya mada itakayojadiliwa katika mkutano wa viongozi waandamizi hao ni pamoja na hoja ya kujenga uwezo kwa nchi za Bara la Afrika.

ACBF ni mdau muhimu katika kuimarisha ushirikiano na bara la Afrika ikiwemo Umoja wa Afrika(AU) pamoja na Shirika la Maendeleo la Afrika(NEPAD).

Madhumuni ya ACBF na washirika wa maendeleo, ni kuimarisha nafasi ya Afrika na kuonyesha umuhimu wa kutambua sauti ya Nchi zinazoendelea katika kujenga uwezo.
Vilevile, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ACBF imejiunga na masharika kama vile Taasisi ya Uchumi na Maendeleo ya Jumuiya ya Ulaya (OECD), Mtandao wa Mafunzo ya Kujenga Uwezo (LenCD), Wanaharakati wa Masuala ya Siasa wa Nchi za Kusini, Ushirika wa CD (CD Alliance) ambao hufanya kazi kwa pamoja kwa kuainisha vipaumbe na mada kuhusu kujenga uwezo kwa Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha, Katibu Mkuu wa ACBF Dkt Frannie Leautier alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kujadiliana na kubadilishana taarifa, maarifa, utalaam na uzoefu kuhusu namna ya uratibu na usimamizi mzuri wa misaada. Alisema kuwa mkutano huo utasaidia kuboresha ubunifu na utekelezaji wa sera zitakazosaidia kupata matokeo endelevu.

Dkt. Leautier alisema kuwa hatua ya kuwaleta pamoja wataalam mbalimbali wanaohusika na uratibu na usimamizi wa misaada ya wahisani itawasaidia washiriki kujifunza mambo mbalimbali na kupanua uelewa wa wadau katika eneo hilo kwa lengo la kutaka kuimarisha uwezo wa Afrika na pia kutoa fedha pale panapohitajika.Aliongeza kuwa mifumo ya utendaji wa wahisani inapaswa kuendana na kanuni ya uendelezaji na kujenga uwezo.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages