Mheshimiwa Freeman Mbowe
-
BARAZA la mawaziri kivuli lililo
na wabunge kutoka Chadema pekee, huenda likavunjwa na kuundwa jipya
litakalojumuisha wabunge wa vyama vingine vya upinzani. Kambi ya
Upinzani bungeni inaongozwa na Freeman Mbowe na Naibu wake, Zitto Kabwe
sasa inafanya mazungumzo na wabunge wa vyama vingine vya upinzani
ikiwa ni hatua ya kutaka kushirikiana. Ikiwa viongozi hao watafikia
mwafaka, Mbowe atalazimika kufumua upya baraza lake la mawaziri ili
kuwajumuisha wabunge wa vyama vingine vya upinzani. Mchakato wa
kuwashirikisha wabunge hao ulianza kwa Mbowe pamoja na Zitto kukutana
na wabunge wa vyama vya NCCR Mageuzi, David Kafulila na TLP, Augustine
Mrema mwishoni mwa wiki iliyopita katika Ofisi za Kambi ya Upinzani,
bungeni, Dodoma. Katika kikao hicho, pia walialikwa Wabunge wengine wa
upinzani, Mohamed Habib Mnyaa (Mkanyageni-CUF) na John Cheyo (Bariadi
Mashariki -UDP), lakini hawakuhudhuria kutokana na kuwa nje ya Mkoa wa
Dodoma kikazi.
Mnyaa alikuwa na safari ya
kibunge nchini Angola na Cheyo alikuwa mkoani Shinyanga ambako alikuwa
na katika shughuli zinazohusiana na masuala ya kilimo cha pamba na
uuzaji wa zao hilo. Mwishoni mwa wiki hii Mbowe alikaririwa akisema kuwa
mazungumzo hayo yameanza na kwamba wazo ni kuunganisha nguvu za
wapinzani na kuwa na mtazamo mmoja wa masuala ya kitaifa kama vile
bajeti ya nchi na mengine. "Niseme tu kwamba kweli tuliwaomba wenzetu
kukutana nao. Kama nilivyoahidi wakati nilipotangaza baraza langu la
mawaziri kivuli kwamba suala la ushirikiano na wapinzani wegine ni la
muda, hivyo tumeona ni vizuri kuanza sasa," alisema Mbowe. "Mrema na
Kafulila tulizungumza nao na tuliwaeleza nia yetu hiyo, sasa
tunachosubiri ni mawazo kutoka kwao kwani sisi tayari tulishaweka hoja
mezani, naweza kusema kwamba hapo ndipo tulipofikia hadi sasa," alisema
Mbowe.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Chadema alisema wanatafuta fursa nyingine ya kukutana na wenzao hao
ili kuendeleza mazungumzo, ikiwa ni pamoja na wale wa UDP na CUF ambao
hawakuweza kushiriki katika kikao cha kwanza. Jitihada za kuwaunganisha
wapinzani wote bungeni, zimekuja wakati kambi hiyo ikitakiwa
kutekeleza jukumu la kutunga kanuni za kuiongoza, suala ambalo Mbowe
alisema linapewa nafasi ya kwanza hivi sasa ili kuweka utaratibu wa
uendeshaji. Kanuni za kambi rasmi ya upinzani bungeni lazima ziwatambue
wabunge wote wa upinzani ikiwa ni pamoja na Kamati tatu za Hesabu za
Serikali zinazoongozwa na wabunge wa kutoka upinzani. Kamati hizo ni
ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ambayo hivi sasa inaongozwa
na Mrema, Hesabu za Serikali Kuu (PAC), ambayo inaongozwa na Cheyo na
ile ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), inayoongozwa na Zitto.
Kwa maana hiyo, taarifa zozote
za kamati hizo lazima zifike kwa kiongozi rasmi wa kambi ya upinzani
bungeni kabla ya kuwasilishwa katika vikao vya Bunge na hilo ni
miongoni mwa mambo ambayo mchakato wa sasa wa kuwaweka pamoja wabunge
wa upinzani unalenga kulitekeleza kwa ufanisi. Mbowe alipotangaza orodha
ya mawaziri kivuli, Februari, 13 mwaka huu alisema mawaziri hao 29
wanatoka Chadema tu kwa kuwa mawasiliano na vyama vingine yalikuwa bado
hayajakamilika. Chadema ni chama cha upinzani pekee kilichotimiza
masharti yatokanayo na kanuni ya 14 fasili ya (4) ya kuchagua kiongozi
wa kambi ya upinzani bungeni, hivyo kumpa Mbowe nafasi ya kuunda Baraza
la Mawaziri Kivuli kutoka Chadema peke yake. “Ni matumaini yangu kuwa
hapo siku za usoni na baada ya kuelewana na kuridhiana na wenzetu,
nitaweza kuunda baraza litakaloweza kushirikisha vyama vingine kutoka
kambi rasmi ya upinzani bungeni,” alisema siku alipotangaza baraza
hilo. Hata hivyo, mmoja wa mawaziri hao, Leticia Nyerere aliyekuwa
akiongoza Wizara Kivuli ya Mazingira alijiuzulu wiki iliyopita, akisema
kuwa anawaachia wengine fursa ya kuongoza badala ya kung'ang'ania
madaraka peke yake.
Kafulila na Mrema Akizungumzia
suala hilo, Kafulila ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kusini alisema:"Naona
ni wazo zuri wala hakuna shida, kweli tumeshiriki katika kikao hicho,
lakini nadhani bado ni mapema mno kusema ni nini
kitakachotokea,"alisema Kafulila ambaye kabla ya kuhamia NCCR Mageuzi
alikuwa mwanachama wa Chadema. Alisema binafsi haoni ubaya wa
kushirikiana na Chadema ikiwa wapinzani wana malengo yanayofanana ya
kuwawakilisha wananchi, lakini pia kuibana Serikali itekeleze wajibu
wake kwa umma. Hata hivyo, alisema ushirikiano huo utawezekana ikiwa
kutakuwa na maridhiano ya pamoja ya jinsi ya kuendesha kambi hiyo ili
kulinda demokrasia na kuheshimu maoni ya pande zote hata pale
kunapokuwa na mitazamo tofauti miongoni mwao. Kwa upande wake, Mrema
alisena: "Siyo jambo baya, ni zuri tu kwani kushirikiana na Chadema
hatujaanzia hapa (bungeni), tumeanzia kule katika Halmashauri ya Moshi,
ile Halmashauri inaogozwa na Chadema kwa kushirikiana na TLP.
" Hata hivyo, alisema Chadema
wamechelewa sana kutoa wazo hilo kwani fursa ilikuwapo tangu mwanzo na
wakashindwa kuitumia kwa maelezo kwamba yeye (Mrema) ni kibaraka wa
CCM. "Jamani hata kama wanaamini kwamba mimi ni kibaraka wa CCM basi
wangewaheshimu wananchi wa Vunjo ambao walinipigia mimi kura na
kunichagua kuwa mbunge, kule Moshi Vijijini mbona tuna ndoa na mambo
yanakwenda vizuri?” Alihoji Mrema na kuongeza: "Kimsingi mimi sina
matatizo, maana ushirikiano ni kitu kizuri sana hasa kwa maendeleo ya
wananchi, sisi sote ni wapinzani kwa hiyo nadhani hakuna tatizo
tukishirikiana na kuheshimiana." Alisema anasubiri vikao vinavyofuata
ili kuona hitimisho la majadiliano yanayoendelea miongoni mwao. Kambi
ya pamoja Wakati Chadema kikianza mchakato wa kuwashirikisha wabunge
wengine wa upinzani katika kuongoza kambi hiyo, kumekuwa na tofauti za
kimtizamo kuhusu masuala mbalimbali yanayojitokeza ndani ya Bunge.
Miongoni mwa masuala hayo ni
hoja inayotaka kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge na watumishi
wengine wa umma. Chadema na NCCR-Mageuzi wanaonekana kuunga mkono suala
hilo, hali CUF wakionyesha kuwa tofauti na msimamo huo. Tofauti hiyo
ilijitokeza juzi wakati Mnyaa alipouliza swali kwa Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda akihoji iwapo Serikali haioni umuhimu wa kuwachukulia hatua za
kisheria watu wanaovunja Katiba kwa kutaka kufutwa kwa posho ambazo
kimsingi zipo kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)