Mwendeshaji (MC) wa majadiliano, Dk. Vicensia Shule (kulia) akiwezesha majadiliano kati ya fanani na hadhira.
|
Na Joachim Mushi, Dar es Salaam
MAPROFESA Ruth Meena pamoja na Marjorie Mbilinyi ambao ni wanachama wa TGNP Mtandao wametoa simulizi za maisha yao huku wakibainisha kukabiliana cha changamoto mbalimbali katika maisha yao.
Akiwasilisha simulizi ya maisha yake kwa baadhi ya vijana wa kike kutoka baadhi ya vyuo jijini Dar es Salaam kwenye Kilinge cha Simulizi kilichoandaliwa na TGNP Mtandao, Prof. Mbilinyi aliwataka vijana hao kupambana bila kujali vikwazo vyovyote.
Alisema yeye amekulia katika moja ya familia za kipato cha kati nchi za ulaya lakini vitendo vya ukatili wa kijinsia za mfumo dume vilikuwepo ndani ya familia yao, ambavyo viligharimu uhai wa mama yake mzazi.
Alisema tofauti na baadhi ya watu nchini Tanzania kudhani kuwa mfumo dume haupo katika nchi zilizoendele si kweli kwani katika familia yao vitendo vya unyanyasaji wa jinsia na mfumo dume vilisababisha mamayake mzazi kujiua.
Alisema mamayake alikuwa msomi wa elimu ya juu na akifanya kazi lakini baada ya kuolewa mumewe alimwachisha kazi na kubaki nyumbani akimtegemea mume, jambo ambalo lilimfanya anyanyasike kwa utegemezi.
Aliwashauri vijana wa kike walio katika elimu ya juu kupambana kikamilifu na kusimamia malengo waliojewekea bila kujali changamoto zilizopo.
Kwa upande wake, Prof. Ruth Meena akisimulia aliwashauri vijana hao kutokatishwa moyo na vikwazo vilivyopo kwani wao pia walikumbana navyo, lakini ujasiri ndio siri ya mafanikio.
“Nilisoma kwa shida, nilianza kupinga vitendo vya unyanyasaji tangu nikiwa shuleni na wakati mwingine ujasiri wangu uliwaponza wenzangu…kinachotakiwa ni kupambana kufikia malengo ama ndoto za kila mmoja bila kujali vikwazo,” alisema Prof. Meena.
Alisema vitendo vya unyanyasaji wa kingono kwa wakinadada vimeanza tangu zamani lakini jitihada binafsi za kukabiliana nazo na kushirikishana ndio siri pekee ya mafanikio.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Bi. Lilian Liundi akiwakaribisha washiriki wa Kilinge cha Simulizi hizo alibainisha kuwa kilikuwa na lengo la kuwatia moyo vijana katika kusimamia ndoto na malengo yao kwenye maisha licha ya changamoto wanazokumbana nazo.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)