ZIJUE SABABU ZINAZOWEZA KUSABABISHA SARATANI YA MATITI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

ZIJUE SABABU ZINAZOWEZA KUSABABISHA SARATANI YA MATITI

Na Jumia Travel Tanzania

Saratani ya matiti ni miongoni mwa saratani inayomkumba zaidi mwanamke duniani na ndiyo inayoongoza kwa vifo vinavyotokana na saratani katika nchi zinazoendelea, ambapo watu takribani milioni 1.7 mwaka 2012 waligundulika kuwa na ugonjwa huo (kwa mujibu wa taarifa zilizopo hivi sasa). Viwango vya saratani duniani kwa ujumla vinatarajiwa kuongezeka kutoka milioni 14 mwaka 2012 na kufikia milioni 20 ndani ya miongo miwili ijayo, na kuifanya saratani kuwa ugonjwa unaotakiwa kuchukuliwa tahadhari zaidi.      
Mwezi Oktoba wa kila mwaka dunia huwa imeutenga mahususi katika kukuza uhamasishaji wa kupambana na ugonjwa wa saratani ya matiti duniani. Kampeni hizo huungwa mkono na serikali, taasisi na mashirika mbalimbali duniani kwa kuangazia umuhimu wa kuhamasisha juu ya saratani ya matiti, kutoa elimu na kufanya tafiti. Miongoni mwa shughuli zinazofanywa katika mwezi huu ni pamoja na kukuza hamasa kwa watu wengi kadri iwezekanavyo na kuchangisha fedha kwa ajili ya kufanyia tafiti toauti za ugonjwa huo.

Miongoni mwa mambo ya msingi unayotakiwa kuyafahamu kuhusu saratani ya matiti ni pamoja na: saratani ya matiti huwakumba zaidi wanawake; dalili zake ni pamoja na uvimbe au kuvimba kwa titi, na mabadiliko ya ngozi au chuchu; sababu zinazoweza kupelekea ni pamoja na kurithi, lakini mitindo ya maisha, kama vile unywaji wa pombe, unaweza kusababisha kutokea zaidi; aina mbalimbali za matibabu zinapatikana, zikiwemo upasuaji, tiba ya mionzi na kimotherapi; uvimbe unaotokea kwenye titi sio saratani, lakini mwanamke yeyote ili kuchukua tahadhari kuhusu uvimbe au mabadiliko yoyote inashauriwa kumuona daktari.    


Kwa kuwa mwezi huu umelenga kwenye kujenga hamasa juu ya ugonjwa wa saratani ya matiti duniani, Jumia Travel ingependa kukufahamisha juu ya sababu hatarishi zifuatazo zinazoweza kupelekea ugonjwa huo.  

Umri. Hatari ya kuupata ugonjwa huu huongezeka kadri umri nao unavyoongezeka. Katika umri wa miaka 20, uwezekano wa kupata saratani ya matiti ndani ya muongo mmoja ujao huwa ni 0.6%. Lakini katika umri wa miaka 70, takwimu hiyo huongezeka mpaka kufikia 3.84%. Kesi nyingi za ugonjwa wa saratani zimegundulika baada ya umri wa miaka 50.

Kurithi. Endapo ndugu wa karibu anaugua au aliwahi kuugua, saratani ya matiti, hatari ya kuupata ni kubwa zaidi. Wanawake ambao wanabeba jeni aina ya BRCA1 na BRCA2 wanayo hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti, saratani ya ovari au zote kwa pamoja. Jeni hizi zinaweza kurithiwa. TP53 ni jeni nyingine ambayo inahusishwa zaidi na hatari ya kusababisha saratani ya matiti.      


Historia ya kuugua saratani ya matiti kipindi cha nyuma. Wanawake waliowahi kuugua saratani ya matiti kipindi cha nyuma wanao uwezekano wa kuugua tena, ukilinganisha na wale ambao hawana historia na ugonjwa huo.  


Historia ya saratani ya matiti katika familia. Hatari kwa mwanamke kupata saratani ya matiti ni kubwa zaidi endapo mama yake, dada au bintiye (ndugu wa karibu zaidi) au ndugu wengi aidha wa upande wa mama au baba walikwishawahi kuugua ugonjwa huo. Kuwa na ndugu wa karibu zaidi wa kiume ambaye aliwahi kuugua saratani ya matiti pia kunaongeza hatari ya kuupata ugonjwa huo kwa mwanamke.   

Uzito wa mwili uliopitiliza. Wanawake wenye uzito uliopitiliza au utapiamlo hususani baada ya kukoma kwa hedhi wanaweza kuwa na hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti, pengine kwa sababu ya kiwango kikubwa cha estrojeni (homoni inayohusika na ukuaji na uwepo wa tabia za kike mwilini). Utumiaji wa kiwango kikubwa cha sukari pia unaweza kuwa ni sababu.

Matumizi ya pombe. Matumizi makubwa ya kiwango cha pombe pia huchangia kusababisha ugonjwa huu. Tafiti zimeonyesha kwamba wanawake wanaokunywa zaidi ya mara 3 kwa siku wana hatari ya kupata ugonjwa huo mara 1.5.

Matibabu kwa njia ya mionzi kipindi cha nyuma. Kuwahi kufanya matibabu ya mionzi kwa saratani isiyo saratani ya matiti kunaongeza hatari ya kupata saratani ya matiti siku za usoni maishani mwako.

Kutokufanya mazoezi. Wanawake ambao hawafanyi mazoezi ya mara kwa mara pia wanayo hatari ya kupata saratani ya matiti.     


Majanga yanayoweza kutokea kazini. Tafiti zinashauri kwamba sababu zingine kama vile kuvuta sigara, kufanya kazi mazingira yenye uwepo wa kemikali yanaweza kupelekea saratani, na pia kufanya kazi kwenye zamu za usiku pia kunaweza kupelekea saratani ya matiti. Ingawa baadaye watafiti walikuja kubainisha kwamba kufanya kazi zamu za usiku ni suala ambalo hakuna uwezekano.  

Kwa kuwa kampeni hii hufanyika duniani kote ikiwemo Tanzania, Jumia Travel inaamini kwamba kuna hospitali zinafanya kampeni za uhamasishaji juu ya saratani ya matiti. Ambapo elimu, vipimo na ushauri hutolewa na wataalamu mbalimbali. Hivyo basi ni fursa kwa kukitumia kipindi hiki ipasavyo ili kuweza kuujua ugonjwa huu na namna ya kukabiliana nao.  

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages