MAANDALIZI YA AIRTEL RISING STARS CLINIC YAKAMILIKA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MAANDALIZI YA AIRTEL RISING STARS CLINIC YAKAMILIKA

Afisa Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde akizungumza na waandishi wa habari juu ya kuanza kwa kliniki ya mpira wa miguu ya Airtel Rising Stars inayoshirikisha wachezaji nyota 65 waliochaguliwa kutoka katika msimu wa sita wa michuano hiyo, cliniki ya mafunzo inategemea kuanza wiki ijayo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa maendeleo wa soka la vijana Ayoub Nyenzi.

Kocha wa timu chini ya miaka 17 Oscar Milambo akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza kuanza kwa kliniki ya soka ya Airtel Rising Stars inayoshirikisha wachezaji nyota 65 waliochaguliwa kutoka katika msimu wa sita wa michuano hiyo. Kulia ni Mwenyekiti wa maendeleo wa soka la vijana Ayoub Nyenzi, na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Ufundi TFF Salum Madadi na kushoto Afisa Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde.
Mkurugenzi wa Ufundi TFF Salum Madadi akiongea na waandishi wa habari wakati wa kutangaza kuanza kwa kliniki ya Airtel Rising Stars wiki ijayo jijini Dar es Salaam, kliniki hiyo itashirikisha wachezaji nyota 65 waliochaguliwa kutoka katika msimu wa sita wa michuano hiyo. Kulia ni kocha wa timu ya taifa ya vijana Oscar Milambo, wa pili kulia mwenyekiti wa maendeleo wa soka la vijana Ayoub Nyenzi na Afisa Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde.
---
Kliniki ya soka ya Airtel Rising Stars iyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa inatarajiwa kuanza Jumatatu, Januari 16 kwenye uwanja wa Karume huku wavulana 40 na wasichana 25 waliofanya vyema kwenye michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars 2016 wakishiriki. Kufanyika kwa kliniki hiyo kutakuwa ni hitimisho ya michuano ya Airtel Rising Stars msimu wa sita.

Kliniki hiyo itakuwa ya siku sita na itaendeshwa na makocha wa timu ya soka ya taifa Oscar Milambo akisaidiwa na Kim Paulsen kwa wavulana huku wasichana wakifundishwa na kocha mkuu wa Kili Queens Sebastian Nkoma.

Akizungumzia maandalizi ya kliniki hiyo, Mwenyekiti wa Maendeleo ya soka la vijana kutoka Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania (TFF), Nyenzi Ayoub alisema “kliniki hiyo itatoa fursa kwa vijana kujifunza mbinu mpya za mpira, na kupata mafunzo kutoka kwa makocha wazoefu ili kuongezewa vipaji vyao. ‘Sisi TFF tumefanya maandalizi yote ya kliniki na tumeichukua kwa uzito wa hali ya juu kwa kuwa ndio njia sahihi ya kupata wachezaji wa timu zetu za taifa, Serengeti Boys na Taifa Queens’, alisema Ayoub.

Tunaamini ya kwamba kliniki haitakuwa na mafanikio kwa wachezaji tu bali na timu zetu kupata wachezaji walio bora. Tumekuwa tukishuhudia wachezaji wazuri wenye vipaji kwenye kila msimu wa Airtel Rising Stars. Nachukua nafasi hii kuzishauri klabu zetu za mpira wa miguu kujitokeza kuangalia wachezaji wakati wa siku sita za kliniki hii ya Airtel Rising Stars, aliongeza Ayoub.

Kwa upande wake, kocha mkuu wa timu ya Taifa ya vijana chini wa umri wa miaka 17 Oscar Milambo alisema, ‘Wachezaji watafundishwa nidhamu ya mpira, ndani na nje ya uwanja, jinsi kumiliki mpira mbele ya mchezaji wa timu pinzani, kutoa pasi za uhakika pamoja na mafunzo ya nadharia. Sambamba na hayo wachezaji pia watakuwa na fursa ya kukutana na wenzao na hii itakuwa na hamasa kwao kwani wengi wao itakuwa mara ya kwanza kupata mafunzo kutoka kwa makocha. Milambo aliongeza kuwa vijana hao watafundishwa jinsi mchezaji anavyotakiwa kujitunza kwa manufaa ya kuendelea kutunza kipaji chake.

Akizungumza juu ya kliniki hiyo, Afisa Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde alisema michuano ya Airtel Rising Stars 2016 imekuwa na mafanikio makubwa na kuwa kufanyika kwa kliniki kutahitimisha Airtel Rising Stars msimu wa sita na kufungua pazia kwa maandalizi ya Airtel Rising Stars msimu wa saba. Michuano ya Airtel Rising Stars mwaka 2016 tuliunganisha na promosheni ya kampuni ya Airtel ya ‘Airtel Fursa’ ambayo ni maalum kwa kuwawezesha vijana kufanikisha malengo yao.

Matinde aliongeza kuwa Airtel inajivunia kuwa sehemu ya mradi huu wa kukuza vipaji vya soka kwani imesaidia kubadilisha soka la Tanzania. Airtel Rising Stars inalenga kutafuta vipaji chipukuzi kuanzia ngazi ya chini mpaka ngazi ya Taifa, kampeni yetu ya Airtel Fursa inalenga kuwainua vijana na kuwawezesha kufikia ndoto zao inaenda sambamba na program hii ya Airtel Rising Stars na tunajisikia furaha kuendelea kuwafikia vijana katika Nyanja mbalimbali aliongeza Matinde.

Wachezaji zaidi ya 1000 wavulana na wasichana walishiriki kwenye michuano ya Airtel Rising Stars 2016 kutoka mikoa ya Mwanza, Morogoro, Mbeya, Arusha, Kinondoni, Ilala, Temeke,Lindi na Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages