TBL kinara tena tuzo ya Mwajiri Bora mwaka 2016 - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

TBL kinara tena tuzo ya Mwajiri Bora mwaka 2016

 Wafanyakazi wa Tbl Group wakifurahia ushindi wa mshindi wa jumla wa Tuzo ya Mwajiri Bora 2016
 Waziri Mkuu,Mh. Kassim Majaliwa  akimkabidhi tuzo ya ushindi wa jumla kwa mwajiri bora mwaka 2016 Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa TBL Group ,David Magese wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo hizo uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi wa ATE,Dk.Aggrey Mlimuka,akimpongeza Mkurugenzi wa Raslimali Watu wa TBL kwa ushindi
Wafanyakazi wa Tbl Group wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kuibuka washindi wa jumla wa tuzo ya mwajiri Bora 2016

  Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imeibuka kuwa mshindi wa jumla wa tuzo ya mwajiri bora mwaka 2016 inayotolewa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE).Ushindi huu imeupata kwa mara ya pili tena ambapo pia mwaka jana ilikuwa mshindi wa tuzo hii ambayo inatambua taasisi inayotekeleza vigezo vya Raslimali Watu kwa viwango vinavyotakiwa.

 Hivi karibuni pia TBL ilishinda tuzo ya mwajiri bora ngazi ya kimataifa kutoka taasisi ya kimataifa ya The Top Employers’ Institute yenye makao yake makuu nchini Uholanzi ambayo inaanda tuzo bora kwa makampuni yanayotekeleza vigezo vya Raslimali Watu kwa viwango vya juu duniani.
Mbali na kushinda tuzo kubwa za uajiri bora ,TBL pia mwaka huu inashikilia ushindi wa jumla wa tuzo ya Rais ya Mzalishaji bora wa mwaka 2015 (President’s Manufacturer of the Year Award (PMAYA).

Mgeni Rasmi katika hafla  ya utoaji wa tuzo hizi kwa makampuni katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere International Convention Centre alikuwa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh.Kassim Majaliwa Kassim ambaye alisema kuwa serikali itashirikiana na sekta binafsi kwa kuzijengea mazingira bora  ya kufanya biashara ili ziweze kukuza wigo wa ajira kwa wananchi hususani vijana wenye taaluma mbalimbali wanaohitimu masomo yao ya elimu ya juu.

Akiongelea ushindi huo,Mkurugenzi Raslimali Watu wa TBL Group,David Magese amesema kuwa kampuni  inao wafanyakazi wapatao 2,100 wakiwemo wafanyakazi wenye ajira za muda katika biashara zake nchini wakiwa  wameajiriwa kwenye vitengo mbalimbali vikiwemo vitengo vya ufundi,Masoko na Usambazaji.
 
Alisema katika kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi kwa kujituma kampuni inao utaratibu wa kutoa MOTISHA kwa wafanyakazi wake kwa kuthamini mchango wao katika kazi mpango ambao umefanikiwa kuongeza ufanisi na mafanikio makubwa kwa kampuni.

Mbali na kuwapa motisha wafanyakazi wake,Magesse alisema TBL  inatekeleza programu mbalimbali zenye manufaa kwa  wafanyakazi wanapokuwa sehemu za kazi na nje ya kazi mojawapo ikiwa ni  The TBL Women’s Forum ambayo imelenga kuwajengea uwezo wafanyakazi wanawake kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini na kushika nafasi za uongozi kwenye kampuni.

“Tunaendelea kuwekeza kwa kutoa mafunzo ya kila aina ya ndani kwa ajili ya kuwanoa wafanyakazi wetu wazidi kupata maarifa zaidi na kwendana na mabadiliko ya teknolojia.Vile vile tunao mpango wa AFYA KWANZA ambao unahusu kuwapatia wafanyakazi wetu na familia zao elimu ya afya na tangu uanze umeonyesha mafanikio makubwa na wanaendelea kuufurahia.
 
Alimalizia kwa kusema kuwa tuzo hizi ambazo kampuni imekuwa ikishinda katika Nyanja mbalimbali kutoka taasisi kubwa zinazoheshimika zinazidi kuwatia moyo wafanyakazi wote wa kampuni ambao mchango wa kila mmoja ndio unawezesha kupatikana kwa mafanikio haya.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages