Pombe za asili zatamba soko la vinywaji nchini - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Pombe za asili zatamba soko la vinywaji nchini

 Wafanyakazi wa DarBrew wakionyesha kinywaji cha Chibuku kwenye chupa ndogo wakati wa kuizindua hivi karibuni
Kikosi kazi cha menejimenti  na wafanyakazi wa DarBrew wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa kusherehekea kupata tuzo ya SABMiller ya kuendeleza vinywaji vya asili nchini hivi karibuni
Licha ya kuwepo na viwanda mbalimbali vya kutengeneza bia na vinywaji vingine vya kisasa ikiwemo uingizwaji wa vinywaji  hivyo kutoka nje ya nchi bado idadi kubwa ya watanzania wanatumia pombe za asili na sababu kubwa inabainishwa kuwa hali hiyo inatokana na vinywaji vya kisasa kuuzwa kwa bei ya juu.

Utafiti uliofanywa na taasisi ya CanBack kuhusiana na matumizi ya  pombe za asili nchini umebainisha kuwa matumizi ya pombe za asili nchini ni asilimia 50% ambapo kati ya asilimia  hizo vinywaji vya asili vinavyototengenezwa kisasa viwandani vinatawala kwa asilimia  8% .

Sababu kubwa ya watumiaji wa vinywaji vya asili ambavyo vingi vinatengenezwa kwenye mazingira yasiyo salama na vinaendelea kuleta athari kwenye jamii ni kutokana  na bei kubwa ya  bia ,wine na vinywaji vinginevyo vya kisasa ambapo idadi kubwa ya wananchi hawana uwezo wa kumudu kuvinunua na kuvitumia.

Akitoa  ripoti ya utendaji wa kampuni katika kipindi cha mwaka 2015 na mikakati yake ya mbele katika kipindi cha mwaka 2016/17 kwa waandishi wa habari hivi karibuni,Mkurugenzi Mkuu wa TBL Group,Roberto Jarrin alisema kuwa kampuni  yake tayari imeanza kutekeleza mkakati wa kuboresha vinywaji vya asili na kuhakikisha vinaingia katika mfumo rasmi unaotambulika kwa kuviwezesha kuchangia pato la taifa kwa njia ya kodi ikiwemo kulinda afya za wananchi.

Jarrin  alibainisha kuwa kampuni ya DarBrew imeweza kuleta mapinduzi ya uuzaji wa pombe za asili nchini kwa kuwawezesha watumiaji kupata kinywaji cha Chibuku na Nzagamba kikiwa kimefungwa kwa viwango mbalimbali na  katika mazingira ya usafi yanayolinda afya za watumiaji na hivi sasa imekuja na mkakati wa kuwainua akina mama kimapato kupitia kuuza bidhaa zake unaojulikana kama Chibuku Mamas ambao hadi kufikia sasa wanawake wapatao 130 wameishajiunga na mpango huu.

Alisema kuwa akina mama wakiendelea kujiunga na mpango huu wataweza kujikwamua kimapato na  kulinda afya zao na wanywaji pia kupunguza uharibifu wa  mazingira kwa  kutumia kuni kwa ajili ya kupikia pombe za asili ambazo zimekuwa zikiuzwa katika vilabu mbalimbali.”Tunawasihi watumiaji wa vinywaji vya asili kujenga mazoea ya kutumia vinywaji vyenye ubora na vilivyotengenezwa kwenye mazingira mazuri kwa ajili ya kulinda afya zao”.Alisema

Katika kuhakikisha  watumiaji wanamudu vinywaji vya asili vya Chibuku na Nzagamba  alisema kampuni imeanza kusambaza vinywaji hivi vikiwa kwenye ujazo wa chupa za ukubwa wa aina mbalimbali ili wanywaji wote waweze kuvipata kulingana na vipato vyao.

Kuhusu mtazamo wake wa hali ya biashara ya kampuni kwa sasa Jarrin alisema sekta ya uuzaji wa vinywaji inakabiliwa na changamoto mbalimbali mojawapo ni bei kubwa ya bia ambayo watumiaji wake wengi wanashindwa kuimudu,kuwepo na vinywaji visivyo katika mfumo rasmi wa ushindani katika soko,kukosekana kwa motisha katika uzalishaji wa malighafi za kutengeneza vinywaji nchini kwa kuwa zinatozwa kodi kubwa ya zuio kuliko malighafi zinazotolewa nje ya nchi.

Alisema baadhi ya mambo yanayostahili kufanyika katika uboreshaji wa sekta ili iendelee kuchangia pato la taifa ni kupunguza  kodi za malighafi zinazozalishwa nchini kama kimea kinachotumika kutengeneza bia pia kulasimisha pombe za asili  ziende sambamba na vinywaji vya sili vinavyolipiwa kodi na kuhakikisha  vinywaji vya asili vinapatikana katika mazingira ya usafi “Pamoja na changamoto nyingi zilizopo katika sekta hii tunaendelea kukabiliana nazo na tumedhihirisha uwezo wetu kwa kuwa na viwanda vyenye ubora wa hali ya juu nchini Tanzania”Alisema Jarrin

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages