Mjasiriamali kijana na mmiliki wa Nelwa’s Gelato, Mercy Kitomari wakati akizungumza na Meneja Uendeshaji wa mtandao wa Habari wa Modewjiblog, Zainul Mzige (hayupo pichani).
MJASIRIAMALI kijana na mmiliki wa Nelwa’s Gelato, Mercy Kitomari amesema anatamani kukutana na Rais John Pombe Magufuli kumwelezea haja ya kukutana na wanawake wajasiriamali vijana wamweleze matatizo yao.
Amesema Rais baada ya kukutana na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara , inafaa akutane na wajasiriamali wanawake vijana ambao wanapita katika magumu mbalimbali .
Alisema katika mahojiano hivi karibuni ambayo sehemu yake itachapishwa katika mtandao wa Modewjiblog muda wowote kwamba, rais Magufuli akiwa kama ‘Role Model wake’ katika kujituma, anaweza kuwasikiliza wanawake hao vijana na kusaidia kuwasukuma juu zaidi katika kampeni ya kuiweka Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
“Nimekuwa nikikutana na wanawake wenzangu ambao wamekata tamaa na wamekuwa wakiniuliza ninawezaje kuendelea, nikawambia wasi-give up (wasikate tama) na kwamba serikali hii ni ya viwanda na kuchapa kazi “ alisema na kufafanua kwamba wanachohitaji wanawake hao ni mazingira mazuri ya kufanya ujasiriamali.
Mercy ambaye anatengeneza ‘ice cream’ zinazotumia matunda yote ya kitanzania kama vile fenesi, nanasi, bungo, ndizi, embe ana ndoto ya kumiliki kiwanda kikubwa kinachoweza kutengeneza na kufikisha ashkrimu kwa Tanzania na Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2020.
Akiwa ameanza kazi hiyo mwaka 2010 kutoka ‘jiko’ la nyumbani Mercy amefanikiwa kutambua wigo wake wa biashara ambayo amesema ina changamoto nyingi hasa mifumo ya vibali na ulipaji kodi na ushuru.
Muonekano wa nje wa duka la Ice Cream la Nelwa’s Gelato lililopo ndani ya Petrol Station ya SOPCO barabara ya Morogoro-Magomeni Mwembechai karibu na kwa Sheikh Yahya.
Alisema uwapo wa kodi nyingi zenye viwango sawa kati ya anayeanza na aliyekuwepo; anayeingiza kidogo na kikubwa kunaleta athari kubwa kwa wajasiriamali wanaotaka kuchomoza.
“To be honest (nikiwa mkweli) zinavunja moyo… nyingi zinakwamisha kwani sisi waelewe tu kwamba tunatengeneza ajira na tunatengeneza soko kama mimi nanunua matunda natengeneza soko la mkulima.,.. natengeneza ashkrimu (Ice Cream) natengeneza ajira.. ipo haja ya kuangalia mambo mengi na hasa hili la kodi na ushuru” alisema.
Alisema ana mambo mengi ya kumwambia Rais Magufuli kama mjasiriamali mwanamke kijana.
“Atupe nafasi tukutane naye wanawake wajasiriamali vijana kisha tutamweleza mengi yakiwemo ya kodi na mifumo yake, mimi ningemweleza haja ya vyombo vyote vya huduma kutumia mtandao, kutoa huduma ,ningemweleza haja ya halmashauri na taasisi kutoa mafunzo mbalimbali ili kuinua wajasiriamali hawa na kuwasapoti si tu kuchukua kodi na ushuru” anasema Mercy.
Anasema wajasiriamali wengi wadogo hawaendelei kwa kukosa sapoti ya mafunzo na namna ya kufanya biashara zao zikue.
“Wasiwe wanachukua kodi na ushuru tu, halmashauri hizi lazima zianze kufikiria kukuza wajasiriamali kwa kuwapa elimu inayostahili katika biashara zao” anasisisitiza Mercy ambaye amesema angelipenda kumuona Role Model wake (Rais Magufuli) kumweleza mengi yanayohusu wanawake vijana na viwanda vidogo kuelekea viwanda vikubwa na hamu ya wajasiriamali wanawake vijana kuchangia pato la taifa na kulipa heshima.
Anasema anapokutana na wajasiriamali wa Uganda, Rwanda anaona jinsi serikali zao zinavyowasaidia kunyanyuka na anaona serikali ya awamu ya tano inaweza kuwasikia na wao wakanyanyuka.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)