TAASISI YA TIBA YA MIFUPA, UPASUAJI WA UBONGO NA MISHIPA YA FAHAMU (MOI) YAPOKEA MILIONI 20 - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

TAASISI YA TIBA YA MIFUPA, UPASUAJI WA UBONGO NA MISHIPA YA FAHAMU (MOI) YAPOKEA MILIONI 20

  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa ,Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI) Dk. Othman Kiloloma akizungumza wakati alipokua akipokea msaada kutoka, Taasisi ya GSM ya Dar es Salaam baada ya kumkabidhi hundi ya mfano ya Milioni 20 kwa ajili ya kununulia vifaa tiba na matibabu kwa watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi ambao unajulikana kama Hydrocephalus & Spinal Bifida. Jijini, Dar es Salaam leo (PICHA NA KHAMISI MUSSA)

NA KHAMISI MUSSA 


Taasisi ya GSM ya Dar es Salaam, imekabidhi msaada wa fedha taslimu shilingi milioni 20, kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) kwa ajili ya kununulia vifaa tiba na matibabu kwa watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi ambao unajulikana kama Hydrocephalus & Spinal Bifida.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mfano wa hundi, mwakilishi wa Kampuni ya GSM, Shannon Kiwamba, alisema wameguswa na changamoto zinazowakabili Watanzania ndiyo maana imeamua kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli ya kuboresha huduma za afya hapa nchini.

Shannon alisema, pamoja na msaada wa fedha ambazo GSM imeipa Moi, vilevile watafadhili kambi za upasuaji (Surgical camps) kwa watoto wenye matatizo ya vichwa kujaa maji na mgongo wazi katika mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dkt Othman Kiloloma, alisema anaishukuru GSM kwa kuguswa na hali za Watanzania hususan watoto wenye matatizo ya vichwa kujaa maji na mgongo wazi ambao kimsingi wanahitaji kufarijiwa.

Dkt kiloloma aliongeza, GSM imefanya uamuzi sahihi wa kuunga mkono jitihada za Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kwa wakati mwafaka.

Alisema, fedha zilizotolewa na GSM zitatumika kama ilivyoelekezwa, vilevile Moi ipo tayari kutoa wataalamu kwenda mikoani kuwafanyia upasuaji watoto katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kuwapunguzia wagonjwa adha ya kusafiri kwenda Dar es Salaam.

Taasisi ya Moi imekuwa ikichukuwa jitihada madhubuti za kuhakikisha Watanzania hususan watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wanapata huduma bora pale walipo, ambapo imekuwa ikipeleka wataalam mikoani kwa ufadhili wa wadau mbalimbali na kuwafanyia upasuaji.
Takwimu zinaonesha hapa Tanzania watoto zaidi ya 5,000 kwa mwaka wanazaliwa na vichwa vikubwa na mgongo wazi ambapo watoto 400 mpaka 500 pekee ndiyo wanapokelewa Moi.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages