Waumini wa dini ya Kiislam wakizozana nje ya Msikiti wa Masjidi Pelapela uliopo eneo la Mtakuja Vingunguti jijini Dar es Salaam katika swala ya Ijumaa leo mchana, baada ya kutokea tafrani ya waumini hao dhidi ya viongozi wao ambao wanatuhumiwa kutafuna fedha zaidi ya sh.milioni 20 walizochanga kwa ajili ya ujenzi wa msikiti mpya.
Muumini wa Msikiti huo, Mbarouk Mohamed Makame (kushoto), akizungumza kuhusu fedha hizo zinazodaiwa kutumiwa vibaya na viongozi wao. Kulia ni mmoja wa wazee wa msikiti huo, Mzee Selasela.
Hapa mzee Selasela akionesha uchakavu wa kapeti.
Hapa akionesha vyoo vilivyo chakaa vya msikiti huo.
Mwonekano wa vyoo vya msikiti huo vinavyotumika.
Waumini wakiwa nje ya msikiti huo wengine wakiswali.
Waumini wakiwa mbele ya vibanda vya biashara vilivyopo nje ya msikiti huo. |
Watoto wa shule ya awali katika msikiti huo wakiwa na mwalimu wao (kulia)
Na Dotto Mwaibale
TAFRANI kubwa imezuka katika Msikiti wa Masjidi Pelapela uliopo eneo la Mtakuja Vingunguti jijini Dar es Salaam baada ya viongozi wa msikiti huo kudaiwa kutafuna zaidi ya sh.milioni 20.
Fedha hizo imeelezwa kuwa zilichangwa na waumini wa msikiti huo kwa ajili ya ujenzi wa msikiti mpya baada ya unaotumika kuchakaa.
Imamu mkuu wa msikiti huo aliyetajwa kwa jina la Hamidu Mitanga alilazimika kutoweka ndani ya msikiti huo baada ya kuendesha swala ya Ijumaa iliyofanyika jana mchana kutokana na waumini kuwa na jaziba kufuatia imamu huyo kutamuka kuwa hakuhitaji kuulizwa maswali yoyote kuhusu upotevu wa fedha hizo na kuwa uongozi uliopo utaendelea kuwepo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi msikitini hapo Dar es Salaam leo mchana wakati wa swala ya Ijumaa mmoja wa waumini wa msikiti huo Mbarouk Mohamed Makame alikiri kuwepo kwa ubadhilifu wa fedha za waumini zilizochangwa kwa ajili ya ujenzi wa msikiti mpya.
"Suala la upotevu wa fedha hizo lipo na limeleta changamoto kubwa kwa waumini na kusababisha kuwepo kwa makundi mawili moja likiwa lile linalolalamikiwa kutafuna fedha hizo na lile linalotaka fedha hizo zitolewe maelezo zilipo" alisema Mzee Makame.
Mzee wa msikiti huo na Mwenyekiti wa Kamati ya watu 10 Saidi Ngubi alisema fedha zinazoshindwa kutolewa maelezo ya matumizi yake na viongozi wa msikiti huo zilitokana na mradi wa maji na michango ya waumini.
"Mimi ndiye niliyeanza kuuliza matumizi ya fedha hizo lakini viongozi hao wakawa hawana majibu na badala yake waliivunja kamati yetu na kuchagua nyingine jambo lililoleta sintofahamu" alisema Ngubi.
Imamu mkuu wa msikiti huo Hamidu Mitanda alisema fedha hizo zilitumika kwa ajili ya mchakato mzima wa kupata umiliki wa kiwanja ulipo msikiti huo na michoro ya ujenzi wa msikiti mpya na kuwa yeye ndiye aliyeanzisha mpango wa kupata msikiti ulio bora na si bora msikiti.
"Binafsi sina shida na cheo hiki cha Uimamu kwani nina shughuli zangu nyingi mkitaka kuniondoa fuateni taratibu kama zili zilizoniweka madarakani na sisi kama viongozi dhamira yetu ni kuwa na msikiti uliobora wa ghorofa na si bora msikiti" alisema Mitanga.
Mitanga alisema chokochoko hizo zilianza tangu mwaka 2007 ambapo tulikubaliana kila muumini kati ya waumini 205 achangie sh.5000 za ujenzi lakini waliochangia walikuwa ni waumini wachache ambapo zilipatikana sh.milioni moja tu.
Imamu huyo alisema uongozi unaoendesha msikiti huo hauko tayari kuachia madaraka kwa tuhuma hizo ambazo hazina ukweli alizodai zinachochewa na baadhi ya waumini.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)