VUGU VUGU LA AJENDA YA WATOTO NA UCHAGUZI MKUU LAENDELEA KIBAHA MKOANI PWANI. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

VUGU VUGU LA AJENDA YA WATOTO NA UCHAGUZI MKUU LAENDELEA KIBAHA MKOANI PWANI.

Mtoto Loida Goodluck Kutoka shule ya Sekondari ya  Simbani akichangia mada katika Mdahalo huo
Mjumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa mtoto Joyce Michael akizungumza jambo wakati wa Mdahalo  huo
Jastin Moses Mratibu wa mradi wa kuzuia ukatili dhidi ya mtoto kutoka Plan International akichangia mchango wake wakati wa mdahalo huo
 Ombeni Ally Mkuu wa Shule ya Sekondari Simbani akifafanua Jambo katika mdahalo  huo
Ramadhan Lutambi mgombea udiwani kata ya Kibaha maili Moja kupitia Chadema akisisitiza Jambo
 
Rosemary Mkonyi mgombea Ubunge kupitia tiketi ya ACT akizungumza Jambo wakati wa mdahalo huo
Baadhi ya wanafunzi wakiwa wanasikiliza mdahalo huo
Wananchi wakiwa wanafuatilia kwa makini mdahalo huo

Na Mwandishi wetu 

Jamii imetakiwa kuwa karibu zaidi na watoto ili kuhakikisha wanalindwa dhidi  ya ukatili na kuhakikisha wanapata haki zao stahiki. Rai hiyo imetolewa  na wakazi wa Kibaha Mkoani Pwani katika Mdahalo wa Walinde Watoto  uliowaleta pamoja wapiga kura, watoto na wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani.

Kwa upande wake mgombea Ubunge wa Kibaha vijijini kupitia ACT Wazalendo Dk. Rose Mkonyi alisema kuwa  chama chake kinaangalia ni kwa namna gani watazingatia katika Lishe bora ya mtoto pamoja na namna gani mtoto atainuliwa Kielimu. Aidha Mgombea  Udiwani wa kata ya maili moja kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo  ‘CHADEMA’ Ramadhani Lutambi alisema chama chake kitaangalia zaidi afya  ya mtoto na kuhakikisha Bohari ya dawa inakuwa na dawa za kutosha.

Hata hivyo, Watoto waliohudhuria mdahalo huo waliwataka wagombea kutimiza  ahadi wanazotoa wakati wa Kampeni ili na wao waweze kufikia malengo yao.


Watoto walipendekeza serikali ijayo iangalie namna ya kuwalinda hasa
wanapoelekea mashuleni kwani wamekuwa wakitembea mwendo mrefu kwenda na  kurudi shule ambako wamekuwa wakipata madhara na vishawishi vingi  wanapokuwa njiani. 


Aidha watoto pia  waligusia suala la rushwa na kwa namna gani linavyorudisha nyuma  maendeleo yao na kuwaomba wagombea wa ngazi zote katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuwa waadilifu ili watoto wapate haki zao.

Mdahalo huo ulioandaliwa na kampuni ya True Vision production chini ya Wizara  ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto wakishirikiana na UNICEF uligusa  maeneo kumi muhimu ya uwekezaji kwa watoto ikiwemo kuwekeza kuokoa  maisha ya watoto na wanawake, kuwekeza kwenye lishe bora, kuwekeza  kwenye usafi, udhibiti wa miundombinu ya maji taka na ugavi wa maji  katika shule na kwenye huduma za afya pamoja na kuwekeza katika
kumwendeleza mtoto akiwa bado mdogo.


Mengine ni pamoja na kuwekeza kwenye elimu bora kwa watoto wote, kuwekeza  katika kuzifanya shule kuwa mahali pa usalama, kuwekeza katika kuwalinda watoto wachanga na wasichana dhidi ya VVU, kuwekeza katika kupunguza  mimba za utotoni, kuwekeza katika kuwanusuru watoto na vurugu,  udhalilishaji na unyonyaji pamoja na kuwekeza kwa watoto wenye ulemavu. 

Vuguvugu hili la kusambaza ajenda ya watoto kupitia midahalo na wagombea wa  nafasi mbalimbali linaendelea kupita mikoa mbalimbali nchini Tanzania  kwani tunaamini kuwekeza katika maeneo haya ya kipaumbele kunaweza  kupunguza umasikini na kuwezesha kuwepo kwa taifa linalostawi na la  usawa.

Unaweza kusikiliza kipindi cha redio cha Walinde Watoto mahali popote kupitia  redio shiriki 19 ikiwemo TBC inayorusha matangazo hayo siku ya Jumamosi  kuanzia saa nane mchana na pia kupitia tovuti ya www.walindewatoto.org na www.facebook.com/WalindeWatoto

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages