Naibu Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya akilia wakati wa ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Dk William Mgimwa katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam jana. (Picha na Fadhili Akida).
MAANDALIZI ya maziko ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa,
yameendelea katika hatua za mwisho, ambapo jana Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, aliwasili mjini Iringa asubuhi kukagua maandalizi hayo. Baada ya kuwasili, Pinda alikwenda moja kwa moja katika Kijiji cha
Magunga Tarafa ya Kiponzelo wilayani Iringa, kukagua maandalizi ya
maziko hayo yatakayofanyika leo, nyumbani kwake katika makaburi ya
familia kilometa 66 kutoka Iringa mjini.
Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Nduli na kupokewa na viongozi
wa Mkoa wa CCM na Serikali na kufika nyumbani hapo, Pinda aliwapa pole
mama mzazi wa Dk Mgimwa, Consolata Semgovano, wajomba zake na wafiwa
wengine. Pia alikagua ujenzi wa kaburi atakamozikwa leo, uwekaji wa mahema,
eneo la kufanyia ibada ya maziko na mahali mwili wa marehemu
utakapolazwa.
Alipomaliza ukaguzi, Waziri Mkuu alirejea mjini Iringa kuusubiri
mwili wa Dk Mgimwa ambao ulitarajiwa kuwasili Uwanja wa Ndege wa Nduli
jana jioni na kwenda kuagwa na wakazi wa Iringa kwenye ukumbi wa ‘Siasa
ni Kilimo’ na baadaye kupelekwa Magunga ambako utalala nyumbani kwake.
Dar es Salaam wamuaga Wakati huo huo, jana mamia ya wakazi wa Dar es Salaam, viongozi wa
Serikali, wabunge, mabalozi wa nchi mbalimbali wakiongozwa na Rais
Jakaya Kikwete, jana walijitokeza kuuaga mwili wa Dk Mgimwa katika
Viwanja vya Karimjee.
Dk Mgimwa alizaliwa mwaka 1950 Magunga na kufariki Januari mosi katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic nchini Afrika Kusini baada ya
kusumbuliwa na ugonjwa wa figo. Miongoni mwa waliojitokeza kumuaga mbali na Rais Kikwete ni Makamu wa
Rais, Dk Mohamed Ghalib Bilal, mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere, Mama Maria na Spika wa Bunge Anne Makinda.
Wengine ni mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, makatibu wakuu wa wizara
mbalimbali na manaibu wao, viongozi wa vyama vya siasa pamoja na Waziri
wa Fedha wa Uganda, Aston Kajala aliyewakilisha mawaziri wa fedha kutoka
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Akizungumzia utendaji wa Dk Mgimwa, Spika Makinda alisema alikuwa
kielelezo kikubwa cha uongozi ndani ya Bunge na Serikali kwa utendaji
wake wa kujituma bila kuchoka huku akifanikisha kikamilifu mabadiliko ya
mfumo wa bajeti.
Alisema kifo cha Dk Mgimwa ni mtihani mzito kwa Rais, hasa katika
kumpata kiongozi mwingine atakayefaa ‘kuvaa viatu vyake’ katika Wizara
hiyo nyeti hapa nchini huku akisisitiza kuendelezwa kwa mbegu bora
zilizopandwa na kiongozi huyo enzi za uhai wake. “Wallah kama tungekuwa tunaambiwa tubadilishe mtu wa kwenda huko,
Mgimwa tungesema abaki tungechagua mtu mwingine wa kwenda lakini kwa
sababu ni mapenzi ya Mungu aende na akapumzike kwa amani,” alirudia
usemi wake Makinda.
Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Saada Mkuya alimsifu Dk Mgimwa kwa
uchapakazi na ushirikiano aliokuwa nao kwa wafanyakazi wote wa wizara
hiyo. Alisema bila kujali nafasi ya kila mmoja ndani ya wizara hiyo, Dk Mgimwa alijali na kusikiliza mawazo ya kila mtu.
Kwao alikuwa mtumishi shupavu aliyeamini katika nguvu za hoja na
mawazo ya kila mtu huku akisisitiza kuwa ingawa pengo lake ni gumu
kuzibika, lakini watafanya kazi kwa kufuata matendo mema waliyojifunza
kupitia kwake. Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema Dk
Mgimwa ni kiongozi aliyekuwa na ushirikiano kwa wabunge wote bila kujali
itikadi za vyama wanavyotokea, jambo alilosema halionekani kwa viongozi
wengine.
Katibu wa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jenister Muhagama
alisema Dk Mgimwa ameacha pengo lisilozibika ndani ya Serikali na chama
kutokana na umakini na busara aliyokuwa nayo wakati wote wa uongozi na
uhai wake. Chanzo Habari Leo

No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)