BARAZA KUU LA USALAMA LAIONGEZEA UWEZO MISHENI YA KULINDA AMANI SOMALIA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

BARAZA KUU LA USALAMA LAIONGEZEA UWEZO MISHENI YA KULINDA AMANI SOMALIA

Sehemu ya wanajeshi wanaouhudumu katika Misheni ya Umoja wa Afrika ( AMISOM) wakiwa katika majukumu yao ya kulinda amani nchi Somalia. Misheni hiyo imeongezewa uwezo wa muda na Baraza Kuu la Usalama wa Umoja wa Mataifa, katika mkutano wake uliofanyika siku ya jumanne uwezo huo ni pamoja na kuongeza idadi wa wanajeshi zaidi ya 4,000, upelekezaji wa helkopta pamona na vifaa vingine lengo likiwa kuiwezesha misheni hiyo kukabiliana vilivyo na vitisho vya wapiganaji wa Al-Shabaab

Na Mwandishi maalum

Katika kuhakikisha kwamba Misheni ya Umoja wa Afrika inakabiliana vilivvo na kundi la wapiganaji la Al-Shabaab, Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, jana jumanne ,limepitisha kwa kauli moja Azimio linaiongezea uwezo muda Misheni hiyo.

Kupitia Azimio hilo Misheni ya Umoja wa Afrika katika Somalia kwa kifupi kama AMISOM inaongezwa wanajeshi zaidi ya 4, 000 pamoja na misaada ya vifaa ili iwe na uwezo mkubwa wa kukabiliana vilivyo na ongezeko la vitisho kutoka Al-Shabaab.

Aidha Azimio hilo ambalo lilipitishwa kwa kauli moja na wajumbe 15 wanaounda Baraza Kuu la Usalama, pia limeongeza muda wa mamlaka ya misheni hiyo hadi Octoba 31, 2014. Misheni ya Umoja wa Afrika ya kulinda amani nchini Somalia iliundwa mwaka 2007
Azimio hilo pia linaiomba Umoja wa Afrika kuongeza nguvu ya jeshi hilo kwa maana ya kuongeza wanajeshi Zaidi kutoka 17,731 waliopo sasa hadi kufikia 22, 126, na pia limeazimia kupanua misaada yake ya kilojistiki inayotolewa na Umoja wa Mataifa kwa Misheni hiyo.

Aidha Baraza Kuu la Usalama kupitia azimio hilo, linasisitiza kwamba, uamuzi huo wa kuiongezea nguvu Misheni ya Umoja wa Afrika unalenga katika kuimarisha uwezo wa kijeshi wa AMISOM katika kipindi cha miezi 18 hadi 21 na kwamba baada ya kipindi hicho tathimini itafanyika kuangalia kama kutakuwa na haja ya kupunguza nguvu ya Misheni hiyo.

Taarifa Zaidi zinaeleza kwamba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika hivi karibuni kwa pamoja walipendekeza kuimarishwa kwa Misheni hiyo ya AMISOM ikiwa ni pamoja na kupelekewa helkopta na zana nyinginezo, kwa lengo la kukabiliana na vitisho vya aina yoyote katika pembe ya Afrika.

Vilevile kupitia Azimio hilo Baraza Kuu la Usalama pia limepokea taarifa kuhusu pendekezo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la kutaka kupeleka kikosi maalum cha kulinda majengo yaUmoja wa Mataifa nchini Somalia (UNSOM) ambayo ilianzishwa mweji Juni kwa lengo la kuisaidia Serikali na wananchi wa Somalia katika juhudi zao za kuleta usalama na ustawi.

Baraza pia limetoa wito wa kuongezea ushirikiano kati ya AU, Umoja wa Mataifa na Serikali ya Shirikisho ya Somalia, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mpango mpana wa amani, usalama na maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages