Mhe. Membe akiongozana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Mhe. Hannah Tetteh mara baada ya kuhudhuria Mkutano wa 12 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola.
Habari na picha na Rosemary Malale
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe ameshiriki Mkutano wa 12 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Mjini New York sambamba na Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kujadili masuala mbalimbali muhimu kuhusu Jumuiya hiyo.
Wakati wa Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Mhe. Kamalesh Sharma alitoa taarifa kwa Mawaziri kuhusu kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa miaka minne kuanzia mwaka 2013/2016 ulioandaliwa na Sekretarieti ya Jumuiya hiyo ili kuiwezesha kukidhi mahitaji ya nchi wananchama. Mpango Mkakati huo umezingatia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha nchi wanachama zinafuata utawala wa sheria, zinaimarisha demokrasia, zinaheshimu haki za binadamu pamoja na kuzingatia usawa wa kijinsia.Katika maelezo
yake, Mhe. Sharma alisema kuwa, Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola
inaendeleza jitihada zake kuzisaidia nchi wanachama kuimarisha
demokrasia na maendeleo endelevu ambapo pamoja na mambo mengine
waangalizi katika chaguzi mbalimbali zinazofanyika katika nchi wanachama
wamekuwa wakipelekwa ikiwa ni pamoja chaguzi zilizofanyika hivi
karibuni katika nchi na Ghana, Maldives na Sri Lanka.
Aidha, Mawaziri hao walipata fursa pia ya kupitia utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Jopo la Watu Mashuhuri wa Jumuiya hiyo (EPG) kuhusu mageuzi katika Jumuiya hiyo. Vile vile ilielezwa kuwa, Katika kutekeleza mapendekezo hayo, Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola imeanzisha mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuunda Kikundi cha Wataalam kwa ajili ya kutafuta fedha ili kuiwezesha Sekretarieti kuzisaidia nchi wanachama zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na zile zinazoendelea.
Katika hatua nyingine, Mawaziri hao walipokea taarifa kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali (CHOGM) unaotarajiwa kufanyika mjini Colombo, nchini Sri Lanka mwezi Novemba, 2013.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo wa CHOGM ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sri Lanka, Mhe. G.L. Peiris alisema kuwa, nchi yake imekamilisha maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mkutano huo na kuwahakikishia Mawaziri hao kuwa hali nchini kwake ni ya amani na usalama tofauti na taarifa zinazotolewa na baadhi ya nchi kuwa hali si shwari nchini humo.Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama 54 wa Jumuiya ya Madola ambayo Kiongozi wake Mkuu ni Malkia Elizabeth II wa Uingereza.
|
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)