Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akagua huduma ya umeme visiwani - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akagua huduma ya umeme visiwani

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitembelea maendeleo ya uzalishaji wa umeme kupitia miundo mbinu iliyopo hivi sasa kwenye kituo kikuu cha umeme Mtoni. Kulia ya Balozi ni Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Madini Mh. Ramadhan Abdulla Shaaban na kushoto yake ni Kaimu Meneja Mkuu wa Zeco Thabit Salum Khamis.
 Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO} Thabit Salum Khamis akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  mfumo mpya wa huduma za umeme unaotumika katika kituo kikuu cha Umeme kilichopo Mtoni wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya huduma za umeme Nchini.
 Mhandisi  wa Vituo vya Umeme katika shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Mohd Juma Othman akimfafanulia  Balozi Seif mfumo wa ugawaji wa laini za umeme mkubwa kwenda katika vituo vipya vilivyojengwa kwa lengo la kutoa huduma za uhakika za Umeme maeneo tofauti Nchini.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji Nishati na Madini imeombwa kufikiria njia muwafaka ya kuyauza Majanareta yaliyopo katika kituo kikuu cha kupokelea Umeme Mtoni ili kuwepusha hasara endapo yataendelea kuwepo eneo hilo bila ya matumizi. 
Majanareta hayo 30 yalikuwa yakitoa huduma za umeme wa dharura katika kipindi ambacho Zanzibar ilikuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa huduma ya nishati ya umeme kutokana na kinanzio chake ilichokuwa ikikitumia wakati huo kutokidhi mahitaji halisi ya huduma hiyo Nchini.
Mhandisi wa Magenareta katika Kituo Kikuu cha Umeme Mtoni Yussuf Reja alitoa ushauri huo wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuangalia maendeleo ya uzalishaji wa huduma ya umeme Nchini kupitia miundo mbinu iliyopo katika kituo hicho.


Mhandisi Yussuf Reja alimueleza Balozi Seif kwamba Majanareta hayo yako katika kiwango bora lakini tatizo kubwa liliopo ni huduma ya mafuta ambayo ni maalum { IDO } na yana hitaji gharama kubwa za uendeshaji. 
Alisema Shirika la Umeme lilikuwa likipata hasara ya zaidi ya shilingi Milioni 16,000,000/- kwa saa wakati maganareta hayo yalipokuwa yakiwashwa kusaidia huduma za umeme katika kipindi cha mgao wa huduma hiyo muhimu.

Mhandisi Yussuf Reja alifahamisha kwamba shirika la umeme lilikuwa likizalisha umeme kupitia Maganareta hayo kwa uniti moja yenye thamani ya shilingi 500/- ambayo ingelazimika kuwauzia wateja wake uniti moja kwa shilingi 700/- gharama ambayo ni mzigo kwa mwananchi wa kawaida. 
“ Ukweli ulio wazi gharama ya kuyaendesha Maganareta hayo kupitia shirika la Umeme ni kubwa mno na inaweza kuleta maafa kwa shirika hilo endapo yataendelea kutumiwa “. Alitahadharisha Mhandisi Yussuf Reja. 

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Madini Nd.Mustafa Aboud Jumbe alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Wizara hiyo tayari imeshapokea mapendekezo ya Shirika hilo kuhusiana na majanareta hayo ya Kituo cha Umeme Mtoni. 
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Ardhi Mustafa Jumbe alisema Wizara hiyo inajipanga kuyafanyia kazi mapendekezo hayo na baadaye kuyawasilisha Serikali kuu kwa ajili ya kupatia ufumbuzi muwafaka.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages