CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar kimemtuhumu Mwenyekiti wa
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, kuwa anaendesha
kampeni za uchochezi wa kidini.
Uchochezi huo umedaiwa kuhatarisha amani ya nchi, hivyo kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kumchukulia hatua za kisheria.
Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu (NEC) Zanzibar, Itikadi na
Uenezi, Waride Bakari Jabu, alisema jana kuwa ni wiki moja sasa tangu
Ponda afanye mihadhara kwenye misikiti ya Mbuyuni, Kwarara na Nungwi
kisiwani Unguja. Waride alisema kuwa hotuba za Sheikh Ponda alizozitoa kwa nyakati
tofauti kwenye misikiti hiyo zinapandikiza mbegu ya chuki, kuondosha
upendo na kuhatarisha amani.
Alisema matamshi yake ni hatarishi kwa amani na utulivu uliopo, kwani
anawataka Waislamu kupigana vita ya dini (Jihad) na kushiriki harakati
za kuikomboa Zanzibar, kwa madai kuwa serikali iliyoko madarakani
inawakandamiza na kuwanyanyasa wananchi. “Sheikh Ponda ni hatari, anapanda shari na chuki miongoni mwa wananchi,
anahamasisha wananchi wafanye uasi, kulipiza visiasi na kutaka waingie
barabarani kwa maanadano ya kutetea haki kama inavyotokea Misri,”
alisema.
Aidha, alisema CCM imeshangazwa na ukimya wa vyombo vya ulinzi na
usalama wa raia kumtazama kiongozi huyo bila ya kumchukulia hatua za
kisheria wakati akiwatukana matusi ya nguoni viongozi wa serikali na
chama tawala.
Aliongeza kuwa Sheikh Ponda huenda anatumiwa na mtandao wa vurugu ili
kuharibu na kuvuruga amani ambapo hamu yake ni kuona damu ya wananchi
ikimwagika na nchi ikiingia kwenye machafuko.
Kwa mujibu wa Waride, kitendo cha Ponda kulitumia jukwaa la dini na
kufanya siasa misikitini hakikubaliki na kwamba kikiachiwa kiendelee
kinaweza kuleta madhara na mgawanyiko.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema jeshi hilo
limeanza kumtafuta Sheikh Ponda tangu walipopokea taarifa za kuendesha
mihadhara ya uchochezi katika baadhi ya misikiti, ikiwa na lengo la
kuibua chuki.
Mussa alisema kitendo anachokifanya kinakwenda kinyume cha sheria, hivyo kumtaka popote alipo ajisalimishe kwa hiari yake. Tangu kuingia visiwani Zanzibar, Sheikh Ponda amekuwa akifungamana na
viongozi wa Jumuiya ya Uamsho wakipinga kitendo cha viongozi wa jumuiya
hiyo kuendelea kubakia mahabusu baada ya kukamatwa na kufunguliwa
mashtaka ya uharibifu wa mali na kuhatarisha usalama wa taifa.
Viongozi hao wa Uamsho wako mahabusu baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka
Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim, kuwasilisha ombi la kufunga dhamana yao
kwa kutumia sheria ya Usalama wa Taifa na marekebisho yake ya mwaka 2002
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)