Na Mhe. Zitto Zuberi Kabwe
1)
Kutokana na kutokuwepo na taarifa sahihi kuhusu deni la Taifa kuna
umuhimu wa kukutanisha wadau wakuu wanaohusika hususani BOT, HAZINA,
Kamati za Bunge na CAG ili kuweza kujua kwa usahihi zaidi ukubwa wa deni
hilo. Vile vile imeamuliwa kuwa Serikali ishauriwe kuunda chombo huru
kitakachosimamia deni la taifa.
2)
Baada ya kuanzisha mfumo mpya wa bajeti ya Serikali mwaka huu kuna
umuhimu wa kuandaa mkutano wa kutathimini mafanikio na changamoto za
mfumo huu na kujadili mambo ya kuboresha zaidi mfumo mzuri wa bajeti ya
Serikali.
3)
Kamati za Bunge zinazoshughulikia usimamizi wa fedha na rasilimali za
taifa zishughulikie zaidi Maafisa Masuuli hatarishi (risk based) ili
kuleta thamani ya fedha katika utendaji wao. Kamati zishirikiane na CAG
katika kuamua ni Afisa Masuuli yupi aitwe kukutana na Kamati.
4)
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge na
TAMISEMI waanzishe utaratibu wa kuratibu mikutano na mafunzo ya
Wakurugenzi wa Halmashauri kwa pamoja kuliko kila Wizara kuwaita
watendaji hao katika sehemu mbalimbali kwa muda tofauti na kuwafanya
kutokuwepo ofisini kwa kipindi kirefu.
5)
Mfumo wa kutunza kumbukumbu za hesabu na nyaraka mbalimbali katika
Serikali Kuu na Halmashauri uboreshwe ili zinapohitajika zipatikane kwa
wakati muafaka bila kisingizio cha aina yoyote.
6)
Kuhusu ukaguzi wa ufanisi CAG asisubiri mpaka asikie malalamiko kutoka
kwa wananchi au kwenye magazeti bali akague mara kwa mara sehemu zote
zenye matatizo.
7)
Taarifa za mwaka za Kamati za Bunge ziwe na kipengele cha kiwango cha
utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati yaliyotolewa awali. Kamati
ziwezeshwe kifedha ili ziweze kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yao.
Kanuni za Bunge zieleze utaratibu wa ufuatiliaji wa Maazimio ya Bunge
na namna utekelezaji wake utavyowasilishwa Bungeni. Vile vile Bunge
litenge siku ya kujadili Serikali ilivyoshughulikia hoja za Kamati za
Bunge. Spika ashauriwe kuhusu umuhimu wa kuunda Kamati ya Bunge ya
kufuatilia ahadi za Serikali.
8) Mikataba katika ngazi ya Serikali za Mitaa iandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
9)
Serikali inatakiwa kufanya jitihada za ziada kuzalisha wataalam wa fani
ya manunuzi. Kuna umuhimu wa PPRA kuongezewa nguvu za ziada za
kiutendaji ikiwa ni pamoja na fedha na wafanyakazi.
10) Bajeti ya Bunge iongezwe kupitia Mfuko wa Bunge na iwasilishwe Bungeni na Naibu Spika na sio Ofisi ya Waziri Mkuu.
11)
Serikali iandae mjadala wa kitaifa wa kutafuta ufumbuzi wa kukabiliana
na vitendo vya rushwa na mmomonyoko wa maadili vinavyoongezeka kwa kasi
hapa nchini. Vilevile viongozi wa umma na watendaji waongoze kwa mfano
kwa kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza majukumu yao.
12)
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma haiweki uwazi wa kutangaza umiliki
wa mali za viongozi. Hii inapelekea viongozi kutoweka wazi mali
wanazomiliki na ni rahisi mtu kuzushiwa umiliki usio wa ukweli. Ni
vyema Sekretarieti wakafanya utafiti wa umiliki wa mali kwa viongozi wa
Umma na kuweka taarifa hizo katika tovuti ya Sekretariati ili
kuwawezesha wananchi kuweza kuona mali zinazomilikiwa na viongozi wao;
na pale ambapo kiongozi hatakuwa ametoa taarifa ya umiliki huo basi
taarifa hiyo itolewe kwa Tume.
13)
Kwa kuwa leseni za udereva za sasa zinaweza kuweka kumbukumbu za makosa
ya usalama barabarani, basi TRA ikishirikiana na Wizara ya Mambo ya
Ndani zihakikishe ya kuwa Askari wa Usalama Barabarani wanatumia
utaratibu huu wa kisasa wa kutoa “notification” na kutoa risiti za
malipo za elektroniki.
14)
Maduhuli ya Serikali sasa yakusanywe kwa kutumia risiti za elektroniki.
Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma yaanze kutumia
risiti za eletroniki mara moja ili kudhibiti upotevu wa mapato ya
serikali yanayotokea hivi sasa katika kutumia risiti zinazoandikwa kwa
mkono. Pia ofisi za serikali zifanye manunuzi yake kwa wafanyabiashara
wanaotumia mashine za kielektroniki.
15)
TRA ihamasishe wananchi na wafanya biashara umuhimu wa matumizi ya
risiti za elektroniki, wafanyabiashara waelimishwe umuhimu wa kutoa
risiti hizo na wananchi waelimishwe umuhimu wa kudai risiti kila
wanapofanya manunuzi. Elimu na uhamasishaji huo unaweza kufanywa kwa
kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo sanaa, timu za michezo, bendi za
muziki, redio, TV, mbao za matangazo n.k.
16) Serikali idhibiti makampuni ya uwakala wa kupakia na kupakua mizigo (clearing and forwarding) yaliyopo Bandarini ili kudhibiti mapato ya forodha.
17) Sheria ya “Anti Money Laundering”
ya 2006 irekebishwe ili iweke viwango vya fedha ambazo mtu anaweza
kuingia au kutoka nazo nchini bila kuzitaja (declare). Kuna umuhimu wa
Waziri wa Fedha kutengeneza kanuni za kutekeleza Sheria hiyo.
18)
Benki Kuu iandae mfumo thabiti wa usimamizi wa Maduka ya Fedha (Foreign
Bureau de Change), na kuhakikisha kutungwa kwa sheria inayozuia matumizi
ya fedha za kigeni katika shughuli za kibiashara hapa nchini.
19) “The Proceeds of Crime Act, 1991”
ifanyiwe marekebisho na kuweka kifungu kinachomwezesha AG/DPP kuwa na
mamlaka ya kuomba mahakama kufungua kesi ya madai (Civil Forfeiture) kwa
watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
20) Imesisitizwa kwamba CAG akague misamaha ya kodi na kuweka taarifa hiyo kwenye taarifa za kila mwaka.
21)
Serikali iimarishe Taasisi zinazoshughulikia maadili utawala bora na
uwajibikaji kama vile Sekretariati ya Maadili ya Viongozi, Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora, Takukuru, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Kamati ya Maadili ya Bunge
ili ziweze kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na kanuni
zilizoanzisha Taasisi hizo.
22)
PCCB na vyombo vingine vinavyohusiana na kushughulikia masuala ya jinai
wawe waalikwa kwenye vikao vya Kamati za Bunge ili waweze kutoa ushauri
kwenye kamati hizo.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)