Waliouawa Darfur: JK atoa tamko kali - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Waliouawa Darfur: JK atoa tamko kali

Ndugu na jamaa wa askari saba wa Tanzania waliokuwa katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa na Afrika (Unamid), waliouawa huko Darfur, Sudan wakiwa na simanzi wakati wa kutoa heshima za mwisho katika Viwanja vya Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dar es Salaam jana.
 Picha na Emmanuel Herman. 

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameutaka Umoja wa Mataifa (UN), kuruhusu kutumika kwa mtutu katika operesheni za kulinda amani zinazoendelea.
Alitoa kauli hiyo jana baada ya kutoa heshima zake kwa wapiganaji saba wa Tanzania waliokuwa Darfur, Sudan katika operesheni ya kulinda amani ya UN na Afrika (Unamid) ambao waliuawa na kundi linalodaiwa la wanamgambo wa Janjaweed wanaoungwa mkono na Serikali ya Sudan inayoongozwa na Rais Omar al-Bashir.

Wapiganaji waliouawa ni Oswald Chaula kutoka 42KJ Chabruma, Songea, Peter Werema (44KJ Mbeya), Fortunatus Msofe (36KJ Msangani, Pwani), Rodney Ndunguru (92KJ Ngerengere), Mohamed Juma (94KJ Mwenge), Mohamed Chukilizo (41KJ Nachingwea) na Shaibu Othman (MMJ- Upanga). “Lazima nikiri kuwa taarifa hiyo ya vifo vya vijana wetu ilinihuzunisha, kunisikitisha na kunikasirisha. Kwa nini watu wa Darfur wawaue wanajeshi wetu ambao wamekwenda kule kuwasaidia wapate utulivu ili kunusuru maisha yao, kuwaondolea wasiwasi na kuwawezesha wafanye shughuli zenye tija kuendesha maisha yao? “Moja kwa moja sikusita kuamini kuwa waliofanya hivyo ni watu wahalifu. Tangu uhuru ni sera ya nchi yetu kutetea wanyonge dhidi ya ukoloni, ubaguzi, uonevu, dhuluma na watu wote walioko katika mazingira hatarishi Afrika na duniani. UN ifanyie marekebisho sheria ili majeshi yanayolinda amani yawe na nguvu za kujihami ili kuzuia maafa yanayoweza kujitokeza.”

Hivi karibuni, Msemaji wa Unamid, Chris Cycmanik alimwambia mwandishi wetu: “Majeshi ya UN mjini Darfur yanaweza kufanya kazi chini ya Kifungu cha VII ambao inaruhusu kutumia nguvu lakini kwa hali iliyopo hawafanyi hivyo,” alisema.

Rais Kikwete alisema eneo hilo ni hatarishi kwa sababu hadi sasa watu 41 kutoka katika nchi mbalimbali wameuawa wakati wakilinda amani huku wengine 55 wakijeruhiwa tangu mpango wa kulinda amani ulipoanza mwaka 2007. “Tumeshawasilisha UN maombi kutaka Kifungu namba Sita cha kulinda amani kibadilishwe na kitumike Kifungu namba Saba ambacho kinawataka askari kujihami pindi wanapovamiwa na maadui,” alisema.
Alisema tayari amewasiliana na Rais al-Bashir akimtaka kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua kali wote waliohusika na tukio hilo huku akiwataka wanajeshi kutokata tamaa kwa tukio hilo na kulichukua kama changamoto katika kujilinda na kuwabaini maadui.
Aliwapa pole wafiwa na kusema Serikali na wananchi wote wapo pamoja katika kipindi hiki kigumu na kuwataka kuwa na subira. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha alisema kitendo cha waasi kuwaua wanajeshi saba wa Tanzania ni mkakati wa vikundi vya waasi kuhakikisha kuwa jitihada za kuleta amani zinagonga mwamba.
Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali Davis Mwamunyange alisema askari hao pamoja na wengine walikuwa wakisindikiza msafara wa walinzi wa amani uliokuwa ukitoka katika kambi yao karibu na Mji wa Nyala. Alisema walipofika kilometa 25, katika eneo la Khor Abeche walivamiwa kwa kushtukizwa na kikundi cha watu wachache na kwa sababu hawakuwa na silaha za kujihami, walishindwa kujitetea na kusababisha vifo hivyo.

CHANZO:MWANANCHI MTANDAONI

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages