Mtuhumiwa namba mbili Joseph
Ludovick (kulia) wa kesi ya kula njama za kutaka kumteka na kumdhuru
Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Denis Msacky, akitoka nje ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam jana baada ya kuachiwa kwa
dhamana. Kushoto ni rafiki yake, Hamfrey Masawe. (Picha na Venance
Nestory)
NA FLORA MWAKASALA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini
Dar es Salaam, imemwonya mshitakiwa mwenza wa Mkurugenzi wa Ulinzi wa
Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, Ludovick Joseph, kutozungumza na
vyombo vya habari wala mitandao ya kijamii. Hakimu Mkazi Aloyce
Katemana, alitoa onyo hilo jana baada ya Wakili Nyaronyo Kicheere,
kulalamikia kitendo cha mshitakiwa Joseph kuzungumza na waandishi wa
habari na kuchapisha habari za kesi hiyo magazetini.
Kutokana na malalamiko hayo, Hakimu
Katemana alimtaka Joseph kutozungumzia kesi hiyo kwenye vyombo vya
habari, kwa sababu si utaratibu na akiendelea kufanya hivyo atafutiwa
dhamana.Wakati huo huo, Mahakama hiyo imetoa kibali kwa Lwakatare kwenda
kutibiwa mgongo nje ya nchi.
Awali Wakili Kicheere aliiomba Mahakama
itoe kibali kwa Lwakatare, ili aende nje kutibiwa matatizo hayo
yanayomsumbua. Aliwasilisha nyaraka zilizotolewa na Daktari wa Hospitali
ya Taifa Muhimbili, kuonesha kuwa Lwakatare anasumbuliwa na tatizo hilo
na anatakiwa aende nje ya nchi kupata matibabu.
Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya
Katemana, ambapo upande wa mashitaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali
Mkuu, Ponsiano Lukosi huku Lwakatare akiwakilishwa na Wakili Kicheere.
Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, na
washitakiwa hao wanaendelea kuwa nje kwa dhamana, hadi Agosti 21
itakapotajwa tena. Hivi karibuni baada ya kupata dhamana, Ludovick
aliomba kupitia mtandao wa kijamii wa Mabadiliko, ahojiwe na waliotaka
kujua zaidi kuhusu kesi yake.
Baada ya kuhojiwa huku akijibu maswali
ya waliomhoji, gazeti la Mtanzania lilichapisha sehemu ya mahojiano hayo
na kumfanya Kicheere aombe mshitakiwa huyo kuzuiwa kuzungumzia kesi
hiyo nje ya mahakama.
Lwakatare na Ludovick wanakabiliwa na
mashitaka ya kula njama kwa nia ya kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa
gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)