Misheni ya Kutuliza Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (
MONUSCO) imetangaza kwamba kwa mara ya kwanza itaanza kuitumia Brigedi
Maalum ( Force Intervention Brigade) katika kudhibiti eneo maalum
la usalama ( security zone ) kuzunguka mji wa Goma ulioko Mashariki
ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na imewapa saa 48 waasi
kusalimisha silaha zao.
Taarifa iliyotolewa na MONUSCO na
kusambazwa na Idara ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa jana jumanne,
inaeleza kwamba watu binafsi katika eneo la Kivu ya Magharibi ambalo
linajumisha Goma na Sake na ambao hawahusiki na vyombo vya usalama
watapewa saa 48 kuanzia saa kumi jana kwa saa za Goma ( Jumanne )
kuzisalimisha silaha zao katika Misheni hiyo na kujiunga na mchakato
wa DDR/RR unaoratibu upokonyaji, usambaratishaji, urejeshwaji makwao,
kuwaunganisha na jamii na kuwapatia makazi.
Baada ya saa kumi
jioni ya Alhamisi, Agosti Mosi. Taarifa hiyo inasema. Wale wote ambao
watakuwa hawajasalimisha silaha zao watachukuliwa kama tishio kwa
usalama wa wananchi na MONUSCO itachukua hatua zote muhimu kuwapokonya
silaha hizo ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu kama ilivyoainishwa katika
Mamlaka na sheria za ushiriki za MONOSCO.
Kwa mujibu wa
taarifa hiyo zaidi ya wananchi milioni moja wanaishi katika eneo dogo la
Goma na Sake na kando kando ya barabara ambayo inawaunganisha na
kambi ya wakimbizi ya Mugungu ambayo ni makazi ya muda ya watu karibu
70, 000 ambao wameyakimbia makazi yao kutokana na mapigano.
Kwa
mujibu wa MONUSCO, tangu kati kati ya mwezi Mei eneo hilo limeshuhudia
mapigano ya mara kwa mara kutoka kwa kundi la M23 dhidi ya majeshi ya
Serikali ya FARDC ikiwa ni jaribio la wazi la kutaka kusonga mbele
kuelekea Goma na Sake.
“ Katika mashambulizi hayo, likiwamo la
hivi karibuni la Julai 14, M23 walitumia kiholela silaha zao za moto
zikiwamo silaha nzito ambazo zimesababisha wananchi kujeruhiwa” .
Taarifa hiyo imeongeza kwamba kundi hilo la M23 katika mashambulizi hayo limelenga pia Vituo vya Umoja wa Mataifa.
Aidha taarifa hiyo inabainisha kwamba eneo hilo maalum la usalama ( security zone) litasaidia kudhibiti tishio la moja kwa moja mbali na eneo la nje ya Goma na pengine eneo hilo linaweza kupanuliwa na kurudiwa sehemu nyingine kutakako hitajika.
Tamko hilo la kutoa saa 48 kwa waasi kusalimisha silaha zao linafuatia kuwasili katika eneo la Goma kwa Kamanda Mkuu wa MONUSCO, Luteni Jenerali Carlos Alberto dos Santos Cruz, ambaye alitangaza kwamba Misheni ya MONUSCO itaunga mkono jeshi la Serikali ( FARDC) katika kuanzisha eneo la usalama kuzunguma eneo la Goma na vitongoji vyake.
Taarifa hiyo
inamkariri Kamanda Mkuu wa MONUSCO akiyapongeza majeshi ya serikali
kwa kazi nzuri iliyofanya wiki iliyopita ya kuwadhibiti M23. Ingawa
anasema eneo la Goma na Sake bado limo katika mazingira magumu sana na
kwamba ni wajibu wa wahusika wote kuhakikisha wahalifu wote hawaendelei
kuhatarisha raia wa eneo hilo.
Kwa mwaka uliopitia , kundi la M23 pamoja na makundi mengine yenye silaha yamekuwa yakipambana mara kwa mara na majeshi ya serikali katika Mashariki ya Kongo, huku makundi hayo yenye silaha mwezi Novemba mwaka jana yakiikalia Goma kwa muda.
Aidha
mapingano ya hivi karibuni ambayo safari hii yalihusisha pia kundi
jingine la wanagambo wenye silaha lenye asili yake nchini Uganda,
yamesababisha zaidi ya wananchi 100,000 kuyakimbia makazi yao na hivyo
kuongeza mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo linalohusisha watu
wengine 2.6 milioni ambao wameyakimbia makazi yao huku wengine 6.4
milioni wakihitaji chakula na huduma za dharura.
Wakati huo huo, Kaimu Mkuu wa MONUSCO Bw. Moustapha Soumare katika taarifa yake ametoa wito kwa pande zote kutafuta suluhu ya kisiasa kwa matatizo ya DRC kupitia Mpango Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa kuhusu amani, usalama na ushirikiano wa maendeleo katika DRC na eneo la Maziwa Makuu uliopitisha mwezi wa Februari na viongozi 11 wa Afrika na Taasisi nne za Kikanda na Kimataifa.
Aidha akasema katika kipindi hiki
ambacho suluhu la kisiasa linatafutwa MONUSCO itatumia nguvu iliyonayo
kuwalinda wananchi dhidi ya hatari zitokanazo na makundi ya waasi.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)