Njiwa akiwa amedhoofu kwa Baridi akiwa katika choo cha wanaume
Hii ni sehemu alipokutwa Njiwa huyo
Majengo nje ya Ofisi ya Afisa Mwajiri
Baadhi ya wafanyakazi wakielekea eneo la tukio
Afisa Mwajiri (Mwenye shati ya bluu) Na baadhi ya wafanyakazi wakishuhudia tukio
Mashuhuda wakitoka eneo la tukio
Barua iliyoletwa na Njiwa maeneo ya Ofisi ya Mwajiri upande wa mbele na nyuma
Jengo la Ofisi ya Afisa Mwajiri
Stesheni ya TAZARA kituo cha Mbeya
ANGALIZO: UNAPOTUMIA HABARI HIZI USIPOTOSHE UKWELI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0787-490 752 Au 0654-221465
PICHA ZOTE NA MBEYA YETU
*******************************************************
WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya
Reli, kati ya Tanzania na Zambia(TAZARA) jana walijikuta katika wakati mgumu na
baadhi yao kulazimika kuzikimbia ofisi zao, baada ya ndege aina ya njiwa
kukutuwa katika moja ya choo cha ofisi hiyo akiwa amefungwa hirizi shingoni,
huku akiwa na barua yenye ujumbe wa onyo kali.
Tukio hilo la aina yake,
lilitokea mapema leo saa mbili asubuhi katika ofisi za mamlaka hiyo
zilizopo eneo la Iyunga Mkoani hapa, hali ambayo mbali na baadhi ya wafanyakazi
wake kuzikimbia ofisi, ilisababisha kuibuka kwa mjadala mkubwa dhidi ya tukio
hilo.
Mtandao huu ulifanikiwa kushudia njiwa huyo mweusi akiwa nyuma ya choo cha kiume katika
eneo hilo la ofisi ya mwajiri, huku akiwa amefungwa hirizi shingoni
iliyozungushiwa shanga mchanganyiko wa rangi tatu, ambazo ni Nyekundu, Njano na Nyeupe. Mbali ya kuwa na hirizi hiyo,
pia njiwa huyo alikuwa amebeba barua inayodaiwa kuwa ni ya mmoja wa wafanyakazi
wa Mamlaka hiyo (jina limehifadhiwa kwa sababu maalumu) ambaye anadaiwa hivi
karibuni kufukuzwa kazi kwa makosa ya ubadhirifu.
Barua hiyo ilikuwa na
maandishi mekundu yenye ujumbe ulioandikwa kwa lugha mbili za Kiswahili na kiarabu,
ambapo katika maandishi ya Kiswahili yalisomeka “ Naomba majibu haraka kama
mtarudisha binti huyu kazini” ilisema sehemu ya ujumbe huo, huku ikiwa na
orodha ya majina matatu ya viongozi wa shirika hilo.
Mbali na ujumbe huo ukiwa
umeandikwa kwa maandishi ya mkono yaliyokolezwa kwa wino mwekundu upande wa
nyuma, lakini upande wa mbele kulikuwa na maandishi yakiwa ni barua ya
kutaarifiwa kufukuzwa kazi kwa mfanyakazi huyo.
Akizungumzia tukio hilo,
Mwajiri wa mamlaka hiyo kanda ya Mbeya, aliyejitambulisha kwa jina la Mchaba
Mgweno, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba waliobaini ni wahudumu wa
usafi. Aliongeza kuwa baada ya
kupokea taarifa hiyo aliwaarifu na wafanyakazi wenzake ambao walikusanyika na
kumshuhudia Njiwa huyo mweusi akiwa amedhoofika huku akiwa na barua hiyo yenye
vitisho.
Alisema baada ya kushuhudia
hali hiyo waliamua kutoa taarifa kituo cha polisi kilichopo ndani ya shirika
hilo, ambapo waliichukua barua hiyo na baadhi ya wafanyakazi hao wakienda kutoa
maelezo kituoni hapo. “Kwa kweli hali hii si ya
kawaida, ila kwa sasa siwezizungumzia chochote kwa kuwa hata mimi tukio hili
limeniweka katika wakati mgumu na nimeshindwa kuendelea na majukumu yangu ”
alisema Mgweno.
Hata hivyo kuliibuka malumbano
makali kati ya wafanyakazi wa shirika hilo walioshuhudia tukio hilo, ambapo
baadhi yao wakidai kuwa tukio hilo ni la kutengenezwa kwa lengo la kuchafuana. “Hebu angalia hiyo barua
yenyewe mbona ni kivuli (Photocopy), kama ingekuwa ni ya ….wanamtaja mfanyakazi
aliyefukuzwa jina limehifadhiwa ingekuwa ni nakala halisi….haiwezekani mambo
haya ni kutaka kuchafuana tu” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Lakini baadhi yao wakiamini
kweli kuwa barua hiyo ilitumwa ili itoe vitisho kwa viongozi wa shirika hilo. Baadhi ya askari polisi wa
kituo cha Tazara walikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea na
uchunguzi ili kubaini ukweli wake. “Ndugu zangu nyie mnajua
taratibu za utoaji wa taarifa kwa jeshi hili, maana wapo wahusika, lakini kwa
kifupi sisi tulipokea taarifa na tunaendelea kuzifanyia kazi” alisema mmoja wa
askari hao.
Hata hivyo, hadi tunapoondoka
eneo la tukio majira ya saa sita mchana Njiwa huyo alikuwa bado yupo eneo la
tukio.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)