Mchambuzi wa Sera kutoka asasi ya TOWSF, Badi Darusi akizungumza leo katika mkutano huo, Kulia ni Marcelina Kibena mkazi wa Morogoro.
............................
............................
MTANDAO
wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na wanaharakati ngazi ya
jamii kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Morogoro, Pwani, Shinyanga
na wadau wengi wa mtandao huo wameichambua bajeti mpya iliyosomwa hivi
karibuni bungeni na kuainisha masuala anuai ndani ya bajeti hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosomwa na Marcelina Kibena mkulima
mkazi wa Morogoro, wanaharakati hao wa ngazi ya jamii kwa upande mmoja
wameridhishwa na kitendo cha Serikali kutambua kasoro zilizokuwepo
maeneo mbalimbali ya ukusanyaji wa mapato na usimamizi wake kama vile
mfumo wa ukusanyaji kodi ambapo kwa sasa imerdhamiria kufanya maboresho
ya sheria anuai za kodi.
Hata hivyo wameainisha mapungufu mengi ambayo yamejitokeza katika
bajeti mpya na kuainisha maoni yao ikiwa ni pamoja na kuitaka Serikali
iunde mfumo shirikishi na endelevu utakaoweza kutengeneza bajeti ya
taifa kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi wote wanawake na wanaume na
makundi mengine yaliyoko pembezoni.
"...Mikakati ya kilimo ilenge kuboresha na kuthamini hali ya
wakulima wadogo. Maendeleo ya kilimo yazingatie kuboresha hali ya
wakulima wadogo ambayo kwa sasa bado ni duni...Kukua kwa uchumi wa nchi
kuende sanjari na kupunguza umaskini kwa wananchi wote wanawake na
wanaume na makundi mengine yaliyoko pembezoni," alisema Kibena
akizungumza na wanahabari kwa niaba ya wanaharakati wote.
Aliongeza katika mapendekezo yao wanashauri sekta ya afya iwe ni
kipaumbele cha bajeti na serikali itenge 15% ya bajeti kufuata azimio
la Abuja, kwani hiyo ni moja ya sekta ya msingi na muhimu kwa ustawi wa
jamii yote, hususan wanawake na nguvukazi ya taifa zima.
Walishauri kuwepo na uwajibikaji zaidi katika ukusanyaji na
usimamizi wa mapato na matumizi ya serikali ikiwemo kuondoa misamaha ya
kodi isiyokuwa na tija na Upunguzaji wa utegemezi wa bajeti ya ili
kupunguza mzigo wa kulipa deni na kuelekeza rasilimali kwa maendeleo ya
watu.
"Bajeti imeainisha mapato ya sh. za Kitanzania trilioni 18.2. Kati
ya hizo matumizi ya kawaida ni sh. trilioni 12.6 wakati sh. trilioni 5.6
ni matumizi ya maendeleo. Tumeshangazwa kuona deni la taifa ambalo ni
sh. za Kitanzania trilioni 23.6, likiongezeka na kuwa kubwa kuliko
bajeti ya taifa. Katika bajeti kiasi cha sh. trilion 6.7, ambayo ni sawa
na asilimia 36.8 ya mapato ya bajeti inategemea mikopo na misaada
kutoka kwa wahisani na wafadhilii mbalimbali."
"Bajeti imeanisha kiasi cha sh. bilioni 383.4 kama mapato kutoka
halmashauri. Hii ina maana kwamba kwa idadi ya halmashauri za wilaya
ambazo ni 152 wastani wa kila halmashauri ni kukusanya sh. bilioni 2.5.
Je, huu ndio uwezo halisi wa halmashauri katika ukusanyaji wa mapato
ukizingatia rasilimali na vyanzo vya mapato vilivyopo katika wilaya
hizo? Tunahoji iko wapi mikakati ya kukusanya kodi kupitia vyanzo vya
halmashauri ili kupunguza utegemezi wa mapato kutoka serikali kuu na pia
halmashauri kuweza kuwahudumia wananchi wao?"
"Ni jambo la kusikitisha kuwa vyanzo vikuu vya mapato ni kodi
zinazowagusa wananchi wa kawaida kama pombe, sigara, mafuta na simu na
ndio tunazotegemea kuendesha maendeleo. Tunashauri serikali kutafuta
vyanzo vya kodi visivyo wakandamiza wananchi wa vipato vya chini na
kuanza kuondoa misamaha ya kodi isiyo na tija k.m kwenye kampuni za
madini na gesi, kampuni za simu (k.m. huduma za milio na miziki ya
simu), mahoteli ya watalii na vitalu vya kuwindia wanyama." Alisema
Kibena
akifafanua zaidi.
Aidha aliongeza kuwa juhudu za kurekebisha
sheria za kodi zinapaswa ziendane na usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa
kodi kutoka makampuni ya simu, mahoteli ya kitalii, bandari, nyumba za
kulala wageni na usafiri wa ndege na treni huku ukiwepo mfumo wa
utumiaji bora wa kodi zinazokusanywa na kuwawajibisha vikali wale
wanaothibitishwa kuwa wamefanya ubadhirifu.
"Kuna ukinzani kati ya bajeti ya maji ambayo imeainisha bajeti nzima
kuwa shilingi bilioni 300 na nyongeza ya shilling bilioni 184.3 ambayo
jumla shilling billion 400, wakati hotuba ya bajeti iliosomwa na wizara
ya fedha iliosomwa na waziri wa fedha ni shilling billion 747.6.
Tunahoji ipi bajeti sahihi ya maji kati ya ile iliyosomwa na Waziri wa
Maji na Umwagiliaji na Waziri wa Fedha?
"Ongezeko la upatikanaji wa maji safi, salama na ya kutosha kutoka
53.74% kufikia 56.57% ya watu waishio vijijini kutoka mwaka 2005 kufikia
mwaka 2012 kama ilivyotamkwa katika mpango wa maendeleo wa 2013/14
(kifungu na. 65) ni ongezeko dogo katika kipindi cha miaka saba.
Linatutia mashaka kuhusu kufikia upatikanaji wa maji kwa umbali wa meta
400 kufuatana na sera ya maji na umwagiliaji ya mwaka 2002. Hali hii
itaendelea kuwafanya wanawake kuendelea kuhangaika kutafuta maji kwa
umbali na muda na kuathiri shughuli za kiuchumi."
"Katika vipaumbele vilivyoainishwa bajeti ya sekta ya afya
haijawekwa kama kipaumbele, wakati moja ya vipaumbele vya mpango wa
maendeleo wa miaka mitano ni pamoja na kuimarisha rasilimali watu. Swali
la kujiuliza ni je afya siyo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi
hii?. Pia bajeti ya afya ni sh. trilioni 1.5 (11%) ya bajeti ya taifa
hailingani na Azimio la Maputo linalotaka kila nchi ilioridhia mkataba
huo itenge asilimia 15% ya bajeti kuu kwa ajili ya afya."
Naye Mchambuzi wa Sera kutoka asasi ya TOWSF, Badi Darusi akifafanua
zaidi juu ya tamko hilo, alisema kwa mtazamo huo wa kimapungufu kadhaa
kwenye bajeti mpya inaendeleza ubaguzi wa kijinsia na kuongeza matabaka
kati ya maskini na matajiri, mijini na vijijini, wanawake na wanaume,
vijana kwa wazee; hivyo, kusisitiza ipo haja kudai bajeti inayozingatia
mahitaji ya wananchi na usawa na kijinsia. Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)