Baadhi ya mashamba ya wananchi eneo la Rongai, wilayani Rombo ambayo mara kadhaa huvamiwa na tembo waharibifu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Judethadeus Mboya akizungumza na mtandao wa www.thehabari.com hivi karibuni wilayani Rombo.
Pichani ni baadhi ya majengo ya Shule ya Msingi Rongai, wilayani Rombo. Shule hii ni miongoni mwa maeneo yanayoathiriwa na uvamizi wa tembo waharibifu ambao huathiri taaluma shuleni hapo.
====== ===== ====== ========
Na Thehabari.com, Rombo
HALMASHAURI ya Wilaya ya Rombo imeanza mipango ya kutumia ufugaji wa nyuki kukabiliana na tembo waharibifu ambao mara kadhaa huvamia baadhi ya makazi ya wananchi maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na kufanya uharibifu wa mazao pamoja na kuua au kujeruhi wakazi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni wilayani hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Judethadeus Mboya alisema tayari halmashauri hiyo imetengeneza mizinga ya nyuki ambayo imesambazwa maeneo kadhaa ili kukabiliana na tembo waharibifu eneo hilo.
"Unajua nimetembea mbuga mbili za Kenya ikiwemo Tsavo ambazo tumepakana nazo eneo hili sehemu ambayo tembo hutokea huko na kuvamia maeneo yetu, sehemu hizi wao wamedhibiti uvamizi wa tembo...wamefuga nyuki wengi sana na maeneo mengine wametumia hadi teknolojia kuwazuia tembo kuvamia makazi ya raia hivyo hawapati madhara kama yetu," alisema Mboya akifanya mazungumzo na gazeti hili ofisini.
Alisema kwa sasa tayari wametengeneza mizinga 50 ya nyuki na kuifunga ukanda wa chini wa vijiji kama Chala, Ibukoni, Ngoyoni na maeneo mengine ambayo tembo huyatumia kama njia kipindi cha uvamizi na kwa sasa mizinga mingine 100 ya nyuki inaandaliwa kuenezwa maeneo mengine kukabiliana na tembo hao hatari.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)