Wanyambo, kabila linalotilia mkazo ustawi wa jamii - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Wanyambo, kabila linalotilia mkazo ustawi wa jamii

Imeandikwa Na Kaanaeli Kaale
.............................
WANYAMBO ni kabila dogo katika jamii ya wabantu linalopatikana Kaskazini Magharibi mwa Tanzania katika wilaya za Karagwe mkoani Kagera.
Lugha yao inaitwa Kinyambo na inamwingiliano na lugha za makabila mengine katika Mkoa wa Kagera, hasa Wahaya.

Kama ilivyo kwa makabila mengine ya Kibantu, Wanyambo wana utajiri wa historia ya utamaduni, mila na desturi ambazo zinaiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yenye urithi mkubwa unaotokana na makabila tofauti Wanyambo wanaishi katika eneo lenye rutuba nzuri inayowawezesha kushiriki katika shughuli za kilimo cha mazao kama ndizi, maharage, mahindi, muhogo, viazi na mtama.

Zao lao kuu la chakula ni ndizi na zao kuu la biashara ni kahawa. Katika ufugaji, Wanyambo wanafuga ng’ombe, mbuzi, kuku na bata. Baada ya kuingia utamaduni wa kigeni Wanyambo walishika elimu na kupata ujuzi wa kufanyakazi katika fani mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Wanyambo ambao hawajapata fursa ya kuendelea na elimu ya juu hujishughulisha pia na useremala, ujenzi, uvuvi na ujasiriamali ili kuongeza kipato katika kaya. Taarifa iliyoandaliwa na Mathias Nzarombi na kuhifadhiwa katika Kijiji cha Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam inasema katika utamaduni wa Kinyambo kulikuwepo na aina mbili za ndoa ambazo ni ndoa ya mke mmoja na ya wake wawili.

Katika ndoa ya mke mmoja mahari na gharama nyingine za harusi zilitolewa na wazazi wa bwana harusi. Hata hivyo, haikuwa lazima kuoa wake wawili hivyo mwanamume aliyetaka kuoa mke wa pili alilazimika kugharimia mwenyewe mahari na taratibu zote za ndoa. Maamuzi ya kuoa mke wa pili yalifanywa na mwanamume pekee au kwa kushirikiana na mke wake wa kwanza ambaye aliridhia kwa kumruhusu mumewe aoe mke mwingine.

Kila mwanamume alipotaka kuoa mke wa pili alipaswa kulipa faini kwa mke wa kwanza. Faini hiyo ilijulikana kama “echihari.” Nzarombina anasema ingawa sheria zinasema ndoa ni kati ya watu wawili; mume na mke, hali ni tofauti katika mila na desturi za jamii ya Wanyambo.

Miaka ya nyuma ndoa ilikuwa mkataba kati ya mke na mume pamoja na familia zote mbili za mke na mume, hivyo ndoa zilikuwa salama zaidi ikilinganishwa na mfumo wa maisha ya kisasa. Ndoa ilikuwa ni alama ya kukomaa na kuwa mtu mzima, ndiyo maana ambaye hajaoa wala kuolewa hakuruhusiwa kushiriki katika maamuzi ya kesi ya ndoa.

Ndoa za Wanyambo ziliandaliwa kwa kutumia hatua mbalimbali kwa kijana kutafuta mchumba, kuchunguza familia ya mchumba, mahari na ndio vyote vilifanyika kwa utaratibu tofauti na kwa muda maalumu.

Kuanzisha uchumba, kitendo ambacho ni maarufu kama “Okupatana” kwa lugha ya Kinyambo ilikuwa hatua ya kwanza ya maandalizi ya ndoa ambapo kijana alitangaza kuanzisha uchumba na msichana wa familia fulani. Wazazi wa pande zote mbili wanapopata taarifa kuhusu uchumba wanaanza upelelezi.

Mambo yanayozingatiwa katika upelelezi huo ni pamoja na uadilifu wa familia, ukaribu, magonjwa ya kurithi na laana katika ukoo. Kila familia inataka kuacha urithi wa kizazi chenye maadili mema hivyo wachumba hutakiwa kuwa makini wakati wa ndoa ili kuepuka kuanzisha uhusiano na kizazi chenye historia na sifa mbaya hasa kuua, uhalifu, chuki na laana.

Baada ya familia zote mbili kuridhika, familia ya mwanamume huingia katika hatua ya tatu ya kutafuta mshenga, maarufu kama Omurangi kwa lugha ya Kinyambo. Mshenga ni mtu muhimu na hutumika kama balozi au daraja la kuunganisha familia ya bwana na bibi harusi.

Shangazi yake bibi harusi hupewa nafasi kubwa kwenye masuala ya kuhakiki posa na hutambulika kama mshenga kwa upande wa familia ya bibi harusi mtarajiwa. Baada ya majadiliano na uchunguzi kukamilika wachumba wanaingia katika hatua ya nne ya kutoa mahari ambayo imegawanyika katika sehemu mbalimbali.

Mahari ya Wanyambo Hatua ya kwanza ya mahari ni wazazi wa mwanamume kwenda kujitambulisha kwa wazazi wa msichana na hutumia pombe (Amarwa agokweranga) yaani pombe ya kujitambulisha.

Baada ya utambulisho ilifuata pombe inayojulikana kama Amarwa Ge’cidgambo ambayo ni mahsusi kwa ukaribisho wa familia ya bwana harusi ili waweze kutajiwa mali na mahari vitakavyotolewa Hatua nyingine muhimu katika mahari ya Wanyambo ni jembe analopatiwa mama mdogo wa msichana.

Jembe hilo linafungwa kwenye khanga au kitenge. Babu (Isenkuru) hupewa pombe na mbuzi yani beberu mwenye ndevu. Pia kuna mahari maarufu kama “Eklbonda bondo cha nyinekuru” au mkongoji kwa lugha ya Kiswahili ambayo ni pombe, blangeti na shuka mahsusi kwa ajili ya bibi yake bibi harusi.

Sehemu ya mahari huenda pia kwa mjomba maarufu kama “Nyinarimi” ambapo hupata pombe na mbuzi jike ambaye hajazaa. Pia kuna sehemu ya mahari huenda kwa “isekanzi”, yaani shangazi ambayo ni mbuzi jike ambaye hajazaa. Baba mdogo yeye hupewa mbuzi jike ambaye hajazaa. Pia kaka wa bibi harusi (banyanya) hupewa pombe na mbuzi jike ambaye hajazaa.

Enkanda wa nyika ni neno la Kinyambo ambalo maana yake ni shuka au kitambaa kikubwa chenye ukubwa wa mita saba. Hiki hutolewa kama sehemu ya mahari ambayo anapatiwa mama mzazi wa bibi harusi. Enkanda wa nyika ambayo ni nguo za asili mahsusi kwa wanawake wa Kinyambo hutolewa ikiwa imefungwa kwenye kitenge kama ishara ya heshima ya kipekee kwa mama mzazi wa bibi harusi.

Mahari kuu ambayo ni maalumu kwa baba mzazi wa bibi harusi wakati mwingine huitwa “okujuga” neno ambalo maana yake ni kuguna. Mguno unatokana na utani kati ya familia mbili ambapo familia ya bibi harusi hutaja kiasi kikubwa cha mahari kitendo kinachomfanya baba wa bwana harusi kuguna. Baada ya mguno huo familia zote huanza majadiliano hadi kufikia muafaka.

Mahari kuu inalipwa kwa kutumia ng’ombe au fedha taslimu. Idadi kamili ya mahari hutokana na majadiliano pamoja na maafikiano. Utani ambao unazua majadiliano ni njia ya kujenga urafiki na kufahamiana zaidi. Pia kuna mahari maarufu kama amahera ga bana ambayo ni fedha taslimu inayotolewa kwa watoto wote wanaomuita bibi harusi mama mdogo.

Pia kuna mahari inayojulikana kama amahera gechitebe ambayo ni ya kununua kiti toka mkwe aliyetangulia. Sehemu hii ya mahari inafanyika ikiwa kuna msichana mwingine ameolewa kabla ya bibi harusi mtarajiwa. Diana Kateka anafafanua kuwa kwa kuwa wakwe wa dada yake bibi harusi hutoa fedha za kukalia kiti basi wakwe wa bibi harusi mtarajiwa hulazimika kutoa fedha za kuwaondoa wakwe wa dada mtu kwenye kiti hicho ili waweze kukikalia.

Diana anasema mila hii ni muhimu kwa ajili ya kutambulisha na kuunganisha familia na koo za wazazi wa watoto wa kike na kule ambako watoto hao huolewa.

“Ikiwa mtu amejaaliwa binti wanne na wote wakaolewa ni lazima familia na koo za walikoolewa binti hao zifahamiane na kushirikiana na ndio maana hata watoto wanaomwita bibi harusi mama ndogo wanapata zawadi ambayo ni sehemu ya mahari,” Diana anaeleza. Hata hivyo, baadhi ya mambo yamebadilika kutokana na mabadi liko ya mfumo wa maisha na ndoa zenye mwingiliano wa makabila tofauti.

Uzazi Salama Mila na desturi za Wanyambo zinazingatia uzazi salama. Mwanamke anapopata ujauzito mumewe anashauriwa kutokutana kimwili na mkewe ili kuepuka kumsumbua mtoto kabla ya kuzaliwa. Miaka ya nyuma wanaume walishauriwa kwenda kufanya vibarua mbali hasa kama ana ndoa ya mke mmoja.

Walitumia falsafa ya amakire (kubemenda) ili kuwakumbusha wanaume athari za kufanya mapenzi nje ya ndoa. Mwanamke mjamzito akichelewa kujifungua ilitafsiriwa kama mkosi au adhabu kwa wanandoa baada ya kuvunja uaminifu na kutoka nje ya ndoa. Hivyo mume na mke walikalishwa pamoja kisha kuulizwa na kushawishiwa kusema ukweli ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Ikiwa mmojawapo atakiri kukosa basi anasamehewa na kupewa onyo kali ili asirudie tena. Hata hivyo, walitumia dawa za asili kumtibu mjamzito na hatimaye mtoto alizaliwa salama. Imani katika Kifo Kifo kilikuwa ni mwisho wa safari ya maisha ya hapa duniani na mwanzo wa maisha mapya ya kwenda kukaa karibu na Mungu.

Baadhi ya Wanyambo walitoa wosia kabla ya kufikwa na mauti na kuelezea jinsi anavyotaka mali yake itakavyogawanywa na ni nani atakuwa mhimili na msimamizi wa familia yake. Katika wosia huo marehemu aliweza kuagiza kwamba hata baada ya kufariki dunia aliyetengwa aweza kusamehewa kama atalipa faini aliyoiagiza vinginevyo angeweza kupata matatizo kutoka kwa marehemu Wanyambo wanasema “kumrumbira.”

Kabla ya maziko tanzia ilitolewa kwa jamaa na marafiki ndipo mazishi yalifanyika. Hata hivyo, maziko yaliweza kuchelewa kwa siku mbili hadi nne kulingana na ukubwa wa familia hususan watu maarufu walipaswa kusubiriwa ili waweze kutoa heshima za mwisho kabla ya marehemu kuzikwa.

Kama ilivyo kwa makabila mengine, Wanyambo wanaamini kuwa mtu hawezi kufa bila kuwepo na sababu hivyo kabla ya kuzika walikuwa na utaratibu wa kukagua mwili wa marehemu na kujaribu kutafuta chanzo cha kifo. Taratibu za maziko zilitumika kujifunza juu ya maisha ya marehemu kwa kuwa kila mtu alizikwa kulingana na haiba yake kwa kuzingatia mchango wake kiuchumi na hususani katika ustawi wa jamii.

Kama aliyekufa ni mtoto mchanga au mtoto aliyezaliwa kabla ya mimba kutimiza umri miezi tisa alizikwa siku hiyo hiyo pasipo kuhusisha watu wengi. Kama marehemu ni mtu mzee mwenye watoto na wajukuu anaweza kuchukua siku nyingi kabla ya kuzikwa ili kutoa nafasi kwa watoto na wajukuu waliombali kufika na kushiriki maziko ya mpendwa wao.

Siku ya matanga inafanyika sherehe kubwa kulingana na uwezo wa familia husika. Kwa kuwa Wanyambo wanathamini sana maendeleo ya ustawi wa jamii hupatwa na hofu anapokufa kijana kabla ya kuoa au kuolewa na kupata watoto. Hivyo akifariki mwanamume ambaye hajaoa alizikwa pamoja na kuti la mgomba maarufu kama Omugogo.

Vilevile mwanamke aliyefariki kabla ya kuolewa alizikwa kwa utaratibu tofauti. Kabla ya kumshusha marehemu kaburini, wazee wa mila walichukua mbegu au kuti la mgomba na kaa kisha kuviweka katika mikono ya marehemu mwanamke aliyekufa kabla ya kuolewa. Mwanamke aliyeolewa lakini akafariki kabla ya kuzaa mtoto alizikwa pamoja na “Omukankabane” wa ndizi.

Matambiko hayo yalikuwa na lengo la kuzindika nafsi zao zisije zikaleta balaa yoyote duniani kwa kuwa iliaminika kuwa ni mkosi mtu kufa kabla ya kuonja maisha ya ndoa na kuzaa ili kutimiza amri Kuu ya Mungu inayosema: “Kazaeni muongezeke muijaze dunia.”

Kwa kawaida matanga yalichukua siku nne hadi saba na wakati mwingine siku 15 ili kuhakikisha wafiwa wanafarijika na kusahaulishwa msiba uliowapata. Hata hivyo, hivi sasa mambo yamebadilika kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha.

Awali ilikuwa nadra kwa kijana au mtoto kufariki lakini maradhi ya watoto na ugonjwa wa Ukimwi umesababisha vifo vya watoto na vijana kuwa kitu cha kawaida katika jamii zote ikiwa ni pamoja na Wanyambo. Mapokeo ya dini, hasa ya Kikristo na ya Kiislamu miongoni mwa jamii ya Wanyambo imeweka kando baadhi ya matendo yakiwemo ya ndoa na namna ya kuzika wafu.

Hivi sasa ni watu wachache hufanya matambiko katika ngazi ya familia kabla ya kuanza ibada rasmi za mazishi kwa kuzingatia dini ya marehemu.


1 comment:

  1. Anonymous6:13 AM

    Na. Furai sana kupata habali kwenye kabila yangu.nilifikiri wanyambo hawajulikani

    ReplyDelete

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages