MHASIBU MKUU JAMBO LEO AFARIKI DUNIA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MHASIBU MKUU JAMBO LEO AFARIKI DUNIA

Aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Kampuni ya Jambo Concepts Tanzania Limited, marehemu Vick Mgoyo
---
MHASIBU Mkuu wa Kampuni ya Jambo Concepts (T) Limited inayochapisha gazeti la Jambo Leo, Staa Spoti, Dar Metro na jarida la Jambo Brand Tanzania, Vicky Mgoyo (49), amefariki dunia.

Meneja Mkuu wa Jambo Concepts, Ramadhani Kibanike, alisema marehemu Vicky Mgoyo alifariki dunia leo asubuhi kwenye Hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam alikokimbimbizwa kupatiwa matibabu baada ya kuzidiwa usiku wa kuamkia jana

Alisema kifo cha Vicky zaidi akijulikana kwa jina la Mama Mgoyo kimeacha pengo kubwa si tu kwa familia yake bali pia kwa Kampuni ya Jambo Concepts kutokana na kwamba alikuwa ni mtu mwaminifu kazini, lakini pia uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzake.

"Tumepoteza mfanyakazi ambaye ni mchapa kazi na kipenzi cha wengi, tutamkumbuka kwa hilo. Naomba wafanyakazi tuungane na ndugu na jamaa katika kuomboleza msiba wa kipenzi chetu huku tukiamini kuwa haya ni mapenzi ya Mungu.

"Bado hatujapata taarifa rasmi za maziko, ila taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu kwenda mkoani Kilimanjaro nyumbani kwao zinaendelea kufanyika," alibainisha Kibanike.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Juma Pito alitoa mwito kwa wafanyakazi kuonesha mshikamano katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi kwa kuondokewa na mfanyakazi mwenzao.

Mhariri Mkuu wa Jambo Leo, Anicetus Mwesa, akizungumzia msiba huo alisema Mama Mgoyo ametwaliwa na Mungu ilhali akiwa bado anahitajika na familia pamoja na ofisi yake, hivyo ameacha pengo ambalo litachukua muda kuliziba.

"Mwenzetu ametangulia nasi tupo nyuma yake, zaidi tumwombee ili Mungu ampumzishe katika raha ya milele," alisema Mwesa.

Kwa upande wake Mpiga Picha Mkuu wa gazeti hili, Richard Mwaikenda, alisema atamkumbuka Vicky kwa kuwa ni mwanamke shupavu ambaye alikuwa anazingatia maadili ya kazi yake ya uhasibu.

Pia alisema alikuwa ni mama mjane makini ambaye alihakikisha anasimamia watoto wake katika suala la kuwapa elimu bora, ambapo katika hilo alikuwa akifanya kila anachoweza kuhakikisha anasomesha nje ya nchi tena kwenye shule bora na makini.

Vicky Mgoyo aliyezaliwa Novemba 26, 1964, ameacha watoto watatu huku wawili kati yao ni wanaume.

Alilazwa katika Hospitali ya Kairuki wiki iliyopita ambako alipatiwa matibabu kwa muda wa siku nne na kuruhusiwa.Jumatatu aliripoti kazini na kuendelea na kazi hadi jana jioni, ambapo usiku alizidiwa na hatimaye jana asubuhi Mungu alimchukua. Mungu ailaze pema peponi roho ya Vicky Mgoyo.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages