MBUNGE MSIGWA NA WENZAKE 70 WAACHIWA KWA DHAMANA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MBUNGE MSIGWA NA WENZAKE 70 WAACHIWA KWA DHAMANA

Na Francis Godwin wa Matukio Daima Blog,Iringa

SAKATA la vurugu  za machinga na polisi mjini Iringa limechukua  sura  mpya  baada  ya  jeshi la  polisi mkoa wa Iringa  kumfikisha mahakamani mbunge  wa jimbo la Iringa mjini mchungaji Peter Msigwa pamoja na  watuhumiwa wengine zaidi ya 70

Huku mahakama   hiyo  ikitoa masharti nafuu ya dhamana kwa  watuhumiwa hao na  kuwaonya  kutofanya  kosa kwa  kipindi  chote  cha kesi  hiyo inapoendelea  kusikilizwa .


Watuhumiwa hao  walifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi wa wilaya ya Iringa Mheshimiwa Godfrey Isaya  leo  majira ya saa 8 mchana  huku wakiwa  chini ya ulinzi mkali  wa askari  wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) waliokuwa na msafara  wa magari zaidi ya matatu  likiwemo  gari ya maji ya  kuwasha .

Mbali ya mbunge Msigwa  kupanda gari ndogo  ya  wazi ya  polisi pamoja na  watuhumiwa  wawili wanawake  waliokamatwa katika  vurugu  hizo bado  watuhumiwa  wengine zaidi ya 70  walitumia usafiri wa karandinga la polisi.

 Mbele  ya mahakama  hiyo  wakili  wa serikali  Adolph Maganda alisema  kuwa  watuhumiwa hao kwa pamoja  wanatuhumiwa kwa makosa matatu  likiwemo la kushiriki  mkutano na kufanya   vurugu ,uchochezi na kuharibu mali kinyume na sheria .

Huku mbunge  akisomewa mashitaka mawili likiwemo  kushawishi   na kufanya mkutano bila  kibali  .

Watuhumiwa  wote  wamekana  mashitaka  dhidi yao  huku  wakili  wa  serikali akidai  kuwa hana pingamizi na dhamana kwa  watuhumiwa hao wote ,hata  hivyo wote   wamekana  mashitaka  yote yaliyotolewa  dhidi  yao.

Hata  hivyo makimu anayesikiliza kesi  hiyo alisema kuwa dhamana kwa  washitakiwa  wote  ipo  wazi  kwa kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika pamoja na kusaini hati ya dhamana  ya Tsh milioni moja .

 Hadi majira ya  saa 10 jioni mahakama  hiyo  ilikuwa ikiendelea na mchakato  wa  kupitia barua  za dhamana kwa  wadhamini  huku  mbunge akiwa  wa kwanza kudhaminiwa ,mbali ya  mbunge  watuhumiwa kati ya 74  waliokuwa  bado kupata  wadhamnini  ni  watuhumiwa  sita pekee.

 Katibu  wa chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) wilaya ya Iringa mjini Suzana Mgonakulima alisema  kuwa  mchakato  wa  kuwadhamini  watuhumiwa  wote  waliosalia unaendelea kufanyika na kuwa wana uhakika wa  watuhumiwa  wote kudhaminiwa .

Hadi  majira  haya  ya saa 10 .40  jioni  wakati habari  hii inakwenda  mitamboni bado  mahakama  ilikuwa ikiendelea na umati wa wafuasi  wa Chadema  ukiwa nje  ya mahakama hiyo kusubiri watuhumiwa  hao kudhaminiwa .
Wakati  huo  huo  wananachi  waliofika  mahakamani hapo  kushuhudia mbunge  wao akifikishwa mahakamani  wamempongeza mkuu  wa  kikosi cha kutuliza ghasia mkoa  wa Iringa (FFU) Said Abdulah Mnunka  kwa kusimamia amani na utulivu katika  eneo hilo la mahakama na jinsi ambavyo alivyoweza  kupambana na machinga  pasipo kumwaga damu kwa  siku ya  jana wakati  wa vurugu  hizo

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages