JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
- Kuongeza idadi ya wakaguzi wa shule
Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema itaendelea kutekeleza mikakati
mbalimbali ya kuimarisha ukgauzi wa shule ili kuhakikisha ufuatiliaji wa
karibu wa maendeleo ya wanafunzi na ufundishaji
shuleni.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Shule Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Marystella Wassena katika mahojiano na kituo cha Redio Uhuru
cha jijini Dar es salaam.
Wassena
amesema chini ya utaratibu na mfumo wa sasa kila shule inatakiwa
kukaguliwa mara moja kila mwaka hatua ambayo imekuwa ikitekelezwa na
wakaguzi wa elimu wa kanda na wa wilaya katika kuhakikisha
maendeleo ya mwanafunzi. Hata hivyo bado kuna changamoto katika
kuzifikia shule zote.
Mkurugenzi
huyo amesema katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa wakati, Wizara
inakusudia kutumia mbinu na mikakati mbalimbali ili kuongeza kiwango
cha ukaguzi shuleni ikiwemo kuongeza idadi
ya wakaguzi.
“Kila
shule inapaswa kukaguliwa mara moja kwa mwaka na tumekuwa tukifanya
hivyo ingawa tumeona kwamba kuna haja ya kuongeza kiwango cha ukaguzi na
kwa sasa kuna mipango inafanyika ili kuwezesha
jambo hili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.”Alisema Wassena.
Amesema
zipo nchi ambazo shule zinakaguliwa zaidi ya mara moja kwa mwaka.
Alitolea mfano wa nchi ya Korea ya Kusini ambapo shule zinakaguliwa mara
moja kila muhula, mfumo ambao amesema unaweza
pia kutekelezwa Tanzania.
Ametaja
baadhi ya juhudi ambazo Serikali inazifanya kwa hivi sasa ni kuimarisha
ukaguzi wa shule kwa kushirikiana na UNICEF kutoa mafunzo kwa Waratibu
Elimu Kata na Wakuu wa Shule ili washiriki
kikamilifu kukagua shule zao ikiwa ni pamoja na ufundishaji na kuona
kuwa mazingira ya shule zao yanafaa katika kutoa Elimu bora.
“Waratibu
Elimu Kata na Wakuu wa Shule watasaidia sana iwapo kila mmoja wao
atakuwa na ujuzi wa kukagua shule zao na kufahamu namna bora ya kuondoa
mapungufu yanayojitokeza kwa kuwa wao wapo
karibu zaidi na shule hizo,” alisema.
Wassena
ameeleza zaidi kuwa kumekuwa na juhudi nyingi za kuboresha ufundishaji
shuleni, juhudi ambazo zimekuwepo hata kabla ya matokeo ya kidato cha
Nne ya mwaka 2012 amabazo ana imani kuwa zitatoa
mafanikio makubwa katika siku zijazo.
Katika
hatua nyengine, Mkurugenzi huyo wa Ukagauzi wa Shule amepiga marufuku
walimu kuwatumia wanafunzi kusahihisha madaftari / mitihani ya wanafunzi
wenzao na amesema kazi hiyo inapaswa kufanywa
na mwalimu mwenyewe ili aweze kujua kikamilifua kama somo lake
limeeleweka na kutoa msaada pale inapobidi.
“Kazi
ya ualimu ni kufundisha na kusahihisha ili kufanya tathmini ya kile
mwalimu alichofundisha na kufahamu kama somo lake limeeleweka au la.
Vilevile mwalimu ataweza kujua mwanafunzi anavyoandika,
anavyoumba herufi na kuweza kutoa maelekezo ipasavyo,” alisema.
Wassena amesema walimu wanaowatumia wanafunzi kusahihisha madaftari/ mitihani ya wanafunzi wenzao wanafanya makosa ya kitaalam.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)