Ofisa Elimu Wilaya ya Handeni, Mgaza Muchiwa
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi wa Wilaya ya Handeni, Patrick Maligana
Eliakimu Kapele ni Makamu wa Shule ya Sekondari Kivesa
Na Thehabari.com,
Handeni
“KESI nyingi
za tuhuma za kubaka na mimba kwa wanafunzi zinazotufikia zinashindwa kufikia
hukumu maana mashahidi wanashindwa kuthibitisha pasipo shaka…nyingi zinaharibika
sababu hawataki kusema ukweli, hivi karibuni nililazimika kuwaweka ndani wawili
(mashahidi) kwa kuwa wanadanganya. Unakuta maelezo aliyotoa polisi ni mengine
na akifika huku anageuka,” anasema Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi wa Wilaya
ya Handeni, Patrick Maligana alipofanya mahojiano na mwandishi wa makala haya
hivi karibuni.
Hakimu Maligana
anasema licha ya takwimu zao kuonesha kesi za mimba/kubaka wanafunzi kwa sasa
zinapungua bado suala la kuharibika kwa ushaidi wa kesi za mimba ni changamoto.
Anasema kesi nyingi za wanafunzi zimekuwa zikishindwa kufanikiwa hadi hatua ya hukumu
kutokana na mtindo wa kuvuruga ushahidi.
Anasema
awali kikwazo kikubwa kwa kesi kama hizo ilikuwa ni upande wa wazazi na walimu
kutotoa ushirikiano wa kutosha kwenye mchakato wa kesi. Lakini walimu na wazazi
wameacha usumbufu huo hivyo imebaki kwa wanafunzi pamoja na watuhumiwa ambao
mara kadhaa wanakuwa wapenzi wao. Anaongeza kuwa licha ya matukio hayo kupungua
changamoto bado zipo.
Takwimu za
kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba 2012 zinaonesha mahakama hiyo ilipokea kesi
10 za tuhuma za mimba/kubaka kwa wanafunzi, huku kuanzia mwezi Januari hadi
Machi 2013 ni jumla ya kesi sita tu zimepokelewa katika mahakama hiyo. Anasema
kesi sita za mwisho kupokelewa zipo katika hatua anuai.
Zuber
Chembera ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Handeni (OCD), akizungumza na mwandishi wa
makala haya ofisini kwake, anakiri kupungua kwa matukio ya kesi za
mimba/kubakwa kwa wanafunzi Wilaya ya Handeni kutokana na takwimu zao.
Anasema kwa
mwaka 2012 hadi mwezi Novemba walikuwa na jumla ya matukio ya kesi kama hizo
66, lakini kwa mwaka huu (Machi, 2013) kuna jumla ya matukio ya kesi kama hizo
14 tu yalioripotiwa.
Anasema
elimu inayotolewa na Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto Kituo cha
Handeni imesaidia. “Kesi zinazotufikia hapa huku zikiwa na ushaidi wa kutosha
tunazipeleka mahakamani, zile zinazokuwa hazina ushaidi wa kutosha tunajaribu
kuzifuatilia kiuchunguzi kwa mujibu wa taratibu zetu. Lengo letu kupitia Dawati
la Jinsia na Watoto ni kuhakikisha tunapunguza kama sio kumaliza kabisa vitendo
hivyo.
Anasema
maranyingi ushahidi wa kesi kama hizo pia umekuwa ukiharibiwa na wahusika kabla
ya kufika mahakamani, wanaweza baada ya kesi kufunguliwa wakashawishiana na
kukaa nje bila ya sisi kujua na hivyo kupotea wote.
Kaimu
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Komnyang’anyo, Nadhiru Kinyama anasema idadi
ya matukio ya mimba shuleni hapo inapungua kwa sasa tofauti na ilivyokuwa hapo
awali, lakini si kwamba matukio hayo yamekoma kabisa.
“Matukio ya
mimba kimsingi kwa sasa yanapungua…lakini si kwamba yamekwisha kabisa, tatizo
kubwa ni malezi katika familia pamoja na vishawishi vingine,” anasema mwalimu
huyo akizungumza shuleni Komnyang’anyo.
Napingana
kwa mtazamo mwingine kwamba umbali wa makazi kwa wanafunzi unachangia mimba…nasema
hivyo kwa kuwa kwa mwaka jana mwishoni kuna mfano mzuri, shuleni kwetu yupo
mwanafunzi (wa kidato cha pili ‘C’) ambaye anahudumiwa kila kitu na pia yu-karibu
na shule lakini amejikuta akipewa mimba na kukatishwa masomo.
Mwanafunzi
huyu pia huwezi kumuingiza katika kundi la wanafunzi wenye mazingira magumu ya
maisha katika familia zao, nasema hivyo kwa kuwa huyu analipiwa kila kitu,
anapewa matumizi yote yanayoitajika na shirika moja linalosaidia wanafunzi wa
kike lakini ameshindwa kuendelea baada ya kupewa mimba.
Kesi hii
tayari ipo kwenye Serikali ya kijiji kwa hatua zaidi baada ya sisi kutoa
taarifa. Sasa watu wanachukulia hatua si kama ilivyokuwa hapo nyuma.Tangu amekuwa
huyu Mkuu wa Wilaya mpya (Muhingo Rweyemamu) wananchi wanatoa ushirikiano kwa
kesi kama hizi. Kimsingi ujenzi wa mabweni itakuwa hauweni kwa wanafunzi ambao
kwa sasa wanatokea vijiji vya mbali kuja shuleni, vijiji hivyo ni pamoja na
Bangu, Kwamagome na Kwakonje.
Mazungumzo
ya wanafunzi Hamad Ngomero kidato III, Salome Kalage kidato cha IV, Michael
Richard kidato cha I, Mwajuma Munga
kidato cha II, Mwajabu Fungo kidato I na Farid Iddy kidato cha IV - wote kutoka
Shule ya Sekondari Komnyang’anyo wanakubali kwa pamoja uwepo wa matukio ya
mimba, japokuwa kwa sasa ni kwa kiwango kidogo.
Mwajuma
Munga anasema matukio hayo bado yapo lakini yamepungua si kama ilivyokuwa hapo
nyuma. Naye Salome Kalage anasema mfano kuanzia mwezi Januari 2013 anawajua
wanafunzi watatu ambao wamepata mimba na kuachishwa shule. Anawataja wanafunzi
hao ni pamoja na Kuruthumu Omar (IV), Elizabeth Hamis (IV) na Docas (III).
Kwa upande
wake mwanafunzi Hamad Ngomero anasema tamaa za starehe na hali ngumu ya maisha
katika familia kaadhaa wilayani Handeni ndiyo inayowaponza wanafunzi wa kike na
hata kujikuta wakitiwa mimba na kukatishwa masomo.
Martin
Mwingo ni Mwaliku Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Kileleni; ujio wa Mkuu wa
Mkoa mpya Handeni umeanza kuonesha mafanikio kwa upande wa matukio ya mimba kwa
wanafunzi. “DC (Mkuu wa Wilaya) wasasa anajitahidi sana kupitia kampeni yake ya
“Niache Nisome” anafuatilia kesi za mimba na kuhakikisha wahusika wanapata
adhabu kwa mujibu wa sheria…mfano sasa hivi tuna kesi moja tumeletewa hizi ni
juhudi za Mkuu wa Wilaya,” anasema Mwingo.
Kesi
zinapungua mfano mwaka jana tulikuwa na kesi mbili za mimba lakini mwaka huu
(2013) hadi sasa hatujapata kesi ya mimba…lakini pamoja na hayo malezi ya
watoto kwa wazazi bado ni tatizo, mtoto ananyenyekea kea mzazi wake tu dharau
kwa watu wengine-haya si malezi. Zamani mtoto anaweza kuadhibiwa na mkubwa
yeyote ilimradi awe amekosa, lakini sasa sivyo.
“Mi
nashangaa kila uchao watu wanang’ang’ania haki za watoto wasiadhibiwe uweke
utaratibu wa kutoa adhabu lakini nashangaa kwanini wasitaje na wajibu wa mtoto
hili ni muhimu…tusing’ang’anie haki za mwananafunzi tu tuoneshe na wajibu wake
pia,” anasema Mwalimu Mwingo.
Anasema
pamoja na juhudi hizo bado utandawazi unaathiri nidhamu za wanafunzi, umiliki
wa simu za mkononi matumizi mabaya ya mitandao kama tovuti nayo yanawaharibu
wanafunzi, ipo haja ya Serikali kuingilia na kupiga marufuku wanafunzi kumiliki
simu shuleni maana simu inamambo mengi sasa.
Hussen
Kigoma ni mwanafunzi wa kidato cha III, katika moja ya shule za kata Wilaya ya
Handeni ambazo ndizo zimezokuwa na changamoto anuai. Anasema ipo haja ya kuwa na
utaratibu wa kuwapima vipimo vya ujauzito mara kwa mara wanafunzi wa kike.
“Sasa hivi
wapo ambao wanapata na kutoa mimba hizo bila uongozi wa shule kujua…sasa hivi
tunawajua wanafunzi wawili ambao walipata mimba mwaka huu shuleni kwetu. Mfano
Joyce Gasper na Jesca Paul wote wa kidato cha nne wamepata mimba…huenda mwaka
huu mimba zikaongezeka zaidi,” anasema Hussein Kigoma.
Eliakimu Kapele ni Makamu wa Shule ya
Sekondari Kivesa; anasema linapungu tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma. Mfano
mwaka jana tulikuwa na matukio mengi ya kesi za mimba kwa wanafunzi, lakini
hadi muda huu kwa 2013 tunayo matukio mawili tu. Na hatu zinachukuliwa maana
msukumo unaanzia kutoka kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.
Hii
inatokana na Mkuu wa Wilaya wa sasa Muhingo Rweyemamu ametia mkazo sana masuala
ya mimba kwa wanafunzi, watu wamekuwa makini na wafuatiliaji.
“Mfano sasa
mimba inapotokea kuanzia mzazi wa mtoto aliyetiwa mimba, mtoto mwenyewe na
mtuhumiwa wote wanashikiliwa…mi naamini kama adhabu hizi zitaendelea kutolewa
ipasavyo watu watanyooka tu,” anasema mwalimu Kapele.
Hata hivyo
mwalimu huyo anashauri mabadiliko ya sheria na kanuni za utoro shuleni, anasema
maamuzi yamekuwa na mkanganyiko. Mfano kanuni za shule zinaelekeza kuwa
mwanafunzi asipo hudhuria shule kwa siku 90 afukuzwe shule. Hili kwa sasa
halifanyiki maana limekaa kisiasa zaidi…wanafunzi wanatoroka hatua
zinachukuliwa kwa mujibu wa maelekezo lakini baadaye wanarejeshwa kuja kufanya
mitihani, hili ni tatizo.
“Inatokea
mwanafunzi anabeba mimba na baadaye anarudi shuleni baada ya kujifungua,
mwanafunzi kama huyu ni tatizo hawezi kuwa na vurugu sana kinidhamu na wakati
mwingine anawavuruga hata wenzake maana anakuwa hana maadili.”
Shule yetu
inautaratibu mzuri wa kuhakikisha muda wote unaofaa wanafunzi wanakuwa darasani
kupata kilichowaleta hapa shuleni. Lakini huwezi kuamini kuna baadhi ya wanafunzi
muda wote wapo huku vichochoroni wanajificha hawaji shuleni, utoro umekithiri!
Lakini hawa huenda wakaruhusiwa kuja kufanya mitihani hapo baadaye.
Kanuni za
shule mara kadhaa zimewekwa pembeni na siasa kuingizwa kwenye kanuni hizo, hali
hii inawapa wanafunzi kiburi na uhuru mkubwa-huwenda wanadhani kufanya hivi ni
kuwasaidia lakini ukweli ni kwamba wanawaharibu.
Ofisa Elimu
Wilaya ya Handeni, Mgaza Muchiwa anakiri kuwepo na mabadiliko makubwa ya utoro
wa mimba ukilinganisha na hali ilivyokuwa mwaka jana. “Kimsingi huko nyuma utoro
hasa wa mimba ulikithiri kwa wanafunzi wa Sekondari na Msingi, lakini hali ya
sasa ni tofauti. Kuna mabadiliko kampeni ya ‘Niache Nisome’ imesaidia sana…kwa
sasa wengi wanaohusika na kuwatia mimba wanafunzi wanapelekwa mahakamani,”
anasema Muchiwa.
Anasema
zoezi la kamatakamata lililokwenda sambamba na kampeni ya ‘Niache Nisome’ na
watu hufikishwa kwenye hatua mbalimbali limesaidia hivyo mambo yanabadilika.
Kwa mantiki hiyo waweza kuona kuanzia Januari 2013 hadi sasa (Machi) sijapokea
kesi hata moja ya mimba.
Tunachokifanya
sasa ni kutoa elimu zaidi kwenye mikutanyiko ya jamii kupitia viongozi wa ngazi
mbalimbali za halmashauri, ili kuhakikisha tunafanikiwa zaidi tumeanza mkakati
wa kuwajengea uwezo wananchi na shule. Hii ni kukabiliana na baa la njaa ambalo
limekuwa likijitokeza mara kadhaa.
“Unajua mtu
anapokuwa na njaa kushawishika ni rahisi…na Handeni kuna njaa sasa hali kama
hii yaweza kuathiri pia sekta ya elimu, tumejipanga kuimarisha kilimo cha mazao
kama mahindi na mtama shuleni ili wanafunzi wawe na uhakika wa chakula wawapo
shuleni,” anasema Ofisa Elimu huyo wa Wilaya ya Handeni.
Ofisa Elimu
Taaluma, Basil Mrutu anasema kwa mwaka jana kwa mujibu wa takwimu zao walikuwa
na ripoti za mimba 26 kwa Wilaya nzima, lakini tangu Oktoba 2012 hadi sasa
hawajapata kesi za matukio ya mimba.
Simon Mdaki
ni Mkuu wa Idara ya Sekondari Wilaya ya Handeni; anasema kuwa “Halmashauri
imeandaa matrekta 7 ambayo shule zitapewa kipaumbele cha kuyatumia ili kuweza
kuendesha kilimo kwa ajili ya lishe kwa wanafunzi.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)