Bibi Amina Mohamed (kulia) mlezi wafamilia ya mwanafunzi Mwenjuma
Magalu akifanya mahojiano na mwanahabari Joachim Mushi, kijijini
Msasa,wilayani Handeni
Mwanafunzi, Mwenjuma Magalu
Bibi Amina Mohamed mlezi wafamilia ya mwanafunzi Mwenjuma Magalu
akifanya mahojiano na mwanahabari Joachim Mushi, kijijini
Msasa,wilayani Handeni
Na Thehabari.com, Handeni
“BAADA ya
kumaliza darasa la saba nilichaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari, lakini
sikufanikiwa kuendelea na elimu hiyo kutokana na uwezo wa mzazi wangu mmoja
(mama) ambaye alishindwa kumudu gharama zilizokuwa zikihitajika kwa
wakati…,”ndivyo anavyoanza kusimulia Mwenjuma Magalu akizungumza Kijijini
Msasa, Wilaya ya Handeni.
Magalu
anasema furaha zote alizokuwa nazo mwaka 2011 baada ya kuchaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Komnyang’anyo, iliyopo kijijini
Msasa Wilaya ya Handeni zilikuwa zikiyeyuka kadri siku zilivyokuwa zikikaribia
kufunguliwa kwa shule za sekondari.
Anasema hadi
shule zinafunguliwa mama yake alikuwa hajakamilisha vitu vilivyokuwa
vikihitajika shuleni ikiwa ni pamoja na fedha ya ada ya kuanzia shule. Kijana
huyo ambaye alikuwa akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake wawili
walitelekezwa na babayao miaka kadhaa iliyopita kijijini hapo baada ya baba
huyo kudai anakwenda kutafuta maisha nje ya kijiji chake.
Hata hivyo kwa kuonesha ana uchu na elimu
kijana Magalu hakumuachia mamayake jukumu la kuitafuta ada peke yake, naye
alifanya vibarua huku na kule kijijini Msasa kwa kuamini huenda angelipata kitu
na kufanikiwa kuingia shuleni. Lakini ilishindikana kwake kutokana na uduni wa
kipato kwa mamayake, kwani fedha ambayo mara nyingine Magalu aliipata kwenye
vibarua ililazimika kununua chakula. Hii ilikuwa ni changamoto nyingine kwa
familia ya kijana huyo mdogo.
Baada ya
ndoto za kujiunga na shule kutoweka bila mafanikio, Magalu aliamua kufanya
vibarua na kampuni ya Kichina iliyokuwa ikitengeneza barabara ipitayo karibu na
kijijini chao. Magalu anasema ndoto yake ya shule ilikuja kurejeshwa na utafiti
wa kihabari uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania
(TAMWA), Machi 2012 kwa kushirikiana na waandishi wa habari.
“Baada ya
kufanya mahojiano na mwandishi wa habari aliyekuja kijijini kwetu Msasa na
kumweleza hali halisi, kilio change kilisikika kwawasamaria na kujitokeza
kuisaidia familia yetu…kwa sasa nimepata ufadhili wa kusomeshwa hadi kidato cha
nne,” anasema Magalu.
Mwenjuma
Magalu ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya
Sekondari Komnyang’anyo muda mfupi baada ya kupata ufadhili wa masomo akiwa
bado na furaha alijikuta anaingia katika mtihani mwingine wa maisha baada ya
mamayake mzazi kufariki dunia.
Hata hivyo
baada ya utafiti wa kihabari kufanyika kijijini Msasa Wilaya ya Handeni na
taarifa za mtoto huyo kushindwa kujiunga na elimu ya sekondari kwa kile mamayake
(kwa sasa marehemu) kutokuwa na uwezo kuripotiwa, alijitokeza mfadhili wa kugharamia
masomo yake ambaye hadi sasa anafanya hivyo.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi juzi akiwa shuleni Komnyang’anyo, mwanafunzi huyo
aliishukuru TAMWA kwa kuibua tatizo la familia yao kwa umma na kupatikana kwa
mfadhili ambaye amemrudisha masomoni licha ya familia yao kutelekezwa.
Kwa upande
wake bibi wa mtoto huyo (Amina Mohamed) ambaye aliachiwa familia hiyo baada ya
kufariki kwa mwanaye, anamshukuru mfadhili wa mjukuu wake. “Binafsi nawashukuru
sana hao (TAMWA) waliopaza sauti hadi mjuu wangu kurudi shuleni…hii kwetu
ilikuwa ni ndoto kwetu maana mtoto mwenyewe alikuwa amekata tamaa kabisa kurudi
shuleni na alikuwa kaanza kufanya vibarua mitaani huku wenzake wakiendelea na
shule,” anasema bibi huyo.
Bibi huyo anafafanua
kuwa kwa sasa bado familia hiyo inahitaji msaada wa huduma hasa baada ya
mwanaye (mama wa familia hiyo) kufariki dunia mwaka jana na kumuachia watoto
wake.
Anasema yeye
ndiye aliyebaki kulea familia hiyo baada ya mtoto wake kufariki. Lakini kwa
sasa hali ya afya yake si nzuri, licha ya uzee alionao amepimwa na kubainika ni
mgonjwa wa TB ambapo ameanza kutumia dawa hivyo kwa hali yake ameshauriwa
kupumzika.
Anasema
baada ya kushauriwa na daktari kupumzika, mzigo wa malezi ya familia sasa umejikuta
ukielekea kwa mjukuu wake Mwenjuma ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili
katika Shule ya Sekondari Komnyang’anyo. Kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa katika uchunguzi
uliofanywa tena juzi na mwandishi wa makala haya bibi huyo anabainisha kuwa mjukuu
wake anamzigo mkubwa.
“Nasema
anamzigo mkubwa kwa kuwa sasa anatakiwa kutekeleza majukumu ya shule na
nyumbani kama yeye ndiye mlezi wa familia…namuhurumia sana lakini sina cha
kufanya. Anaporudi shuleni anatakiwa kutafuta chakula cha familia, yeye pia
ndiye mpishi, mchota maji na ndiye mkulima,” anamzigo mzito kweli ndiyo maana
wakati mwingine nalazimika kuingilia licha ya afya yangu.
Muhingo
Rweyemamu ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni, anasema tatizo la uduni wa maisha kwa
familia katika wilaya hiyo lipo kwa kiasi kikubwa. Anabainisha kuwa kwa sasa Halmashauri
ya Wilaya ya Handeni haina mfumo maalumu kwa ajili ya kusaidia moja kwa moja
familia kama hizo.
Anasema kinachofanyika
ni kuhamasisha ndugu, jamaa na marafiki kuendelea kutoa msaada kwa familia
ambazo zimekuwa katika wakati mgumu kimaisha na kuitaji msaada. “Kwa ujumla tunatoa
elimu ya kuhakikisha wazazi wanazaa watoto ambao wanaweza kuwamudu kimatunzo…wajua
wakati mwingine umasikini katika familia hizi huchangiwa na wanaume kuzaa bila
mpangilio, unakuta mwanaume anakuwa na familia zaidi ya moja wakati hana kipato
cha kumudu familia hizo,” anasema Rweyemamu.
Anasema kwa
kuwa hili limesha jitokeza wamejipanga kuziwezesha shule kufanya uzalishaji wa
kilimo ili wanafunzi waanze kupata chochote wawapo shuleni, halmashauri imepata
vocha takribani 300 ambazo zitasaidia upatikanaji wa pembejeo kwa shule
zitakazokuwa zikizalisha mazao kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi kama chakula
wawapo shuleni mchana.
Halmashauri
pia imejipanga katika uhamasishaji kilimo kwa familia pamoja na uwezeshaji
katika nyanja anuai ili kukabiliana na janga la njaa pamoja na ugumu wa maisha
kiujumla.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TAMWA





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)