Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, William Erio akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu mfuko huo kutimiza miaka 10
tangu kuanzishwa kwa Fao la Elimu. Kulia ni Meneja Uhusiano wa PPF, Lulu
Mengele na Meneja Michango wa PPF, Cosmas Sasi.Picha na Francis Dande
----
DAR ES SALAAM, Tanzania
MFUKO wa Pensheni wa PPF, umetambia mafanikio iliyopata
katika kipindi cha miaka 10 ya Fao la Elimu, linalotolewa kwa kuwasomesha
watoto, huku likijumuisha ulipaji wa karo za shule na mahitaji mengine ya
wanafunzi.
Akizungmza na Habari Mseto, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William
Erio, alisema kuwa Fao la Elimu la PPF lilianza kuwasomesha wanafunzi mwaka
2003, ambapo mwaka jana 2012 pekee jumla ya wanafunzi 1,333 walisomeshwa katika
shule tofauti za sekondari.
Erio alibainisha kuwa, PPF ilitumia kiasi cha shilingi
milioni 682, kuwalipia karo na mahitaji mengine wanafunzi inaowasomesha waliopo
katika shule 765 za sekondari kote Tanzania Bara na Visiwani na kufaulisha
wengi miongoni mwao.
Aliongeza kuwa, sherehe za mafanikio yatokanayo na Fao la
Elimu zimeanza katika kanda zote nchini na kwamba zitahitimishwa Jumamosi
Aprili 27 katika sherehe za kitaifa, ambazo mgeni rasmi atakuwa ni mke wa Rais,
Mama Salma Kikwete.
Pamoja na sherehe hiyo itakayoambatana na burudani za aina
mbalimbali, PPF itatoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mitihani
iliyopita, miongoni mwa wale wanaosomeshwa kupitia Fao la Elimu la mfuko wake.
“Lengo la zawadi hizo kwa wanafunzi hao ni kuwahamisha
wengine watumie vema fursa ya kusomeshwa kupitia Fao la Elimu ili wafanye
vizuri katika mitihani yao ijayo na tunawaomba wote wanaosomeshwa na PPF waje
kwenye sherehe hiyo,” alisisitiza Erio.
Aidha, Erio alifichua kwamba, licha ya matokeo mabaya ya
mitihani ya mwaka jana yaliyotokana na ugumu wa mitihani hiyo, watoto waliokuwa
wanasomeshwa na PPF waliweza kufanya vizuri, kiasi cha kuwapo waliofaulu kwa
daraja la kwanza na pili.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)