Ujumbe kutoka Tanzania na Maofisa wa Kamisheni ya Utalii ya Chaoyang, Beijing katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo hayo. Ujumbe
kutoka Tanzania ukiwa katika mazungumzo na Maofisa wa Kamisheni ya
Utalii kutoka Chaoyang, Beijing yenye lengo la kutangaza utalii wa
Tanzania.
………………………………………………………………
Na Pascal Shelutete, Beijing
Tanzania imehimiza wawekezaji
kutoka China kuwekeza katika sekta ya utalii ambayo ina fursa nyingi
ambazo bado hazijatumiwa ipasavyo. Mkurugenzi wa Utalii kutoka Wizara
ya Maliasili na Utalii Bw. Ibrahim Mussa alisema hayo jana alipokutana
na ujumbe Kamisheni ya Utalii ya Chaoyang jijini Beijing nchini China.
Bw. Mussa ambaye anaongoza ujumbe
kutoka Tanzania unaotembelea China kwa lengo la kutangaza utalii wa nchi
yetu alisema kuwa Tanzania ina matarajio makubwa ya kupata wawekezaji
kutoka China hasa katika maeneo ya uwekezaji wa hoteli ili kuongeza
idadi ya vitanda nchini ili kukidhi mahitaji ya watalii wanaofika nchini
kutalii. Alisema kuwa utaalamu wa mafunzo kwa ajili ya rasilimali watu
katika sekta ya utalii inahitajika ili kuweza kuhudumia watalii
wanaofika nchi katika viwango vinavyokubalika kimataifa na hivyo
kuwataka Wachina kutumia fursa hizi kuisadia Tanzania.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi
Mkuu wa Hifadhi za Taifa Bw. Allan Kijazi alisema kuwa TANAPA
imeshaandaa mwongozo kwa wawekezaji unaobainisha fursa mbalimbali za
uwekezaji katika Hifadhi za Taifa. Alisema kuwa mwongozo huo hivi sasa
umetenga maeneo 25 kwa ajili ya uwekezaji ikiwemo manne katika Hifadhi
ya Serengeti; matatu katika Hifadhi ya Tarangire; sita Hifadhi ya Katavi
na manne Hifadhi ya Saadani ambako wawekezaji wanahimizwa kuwekeza
ikiwemo kutoka China ambayo ukuaji wake kiuchumi unakwenda kwa kasi
kubwa..
Kijazi alisema kuwa hivi sasa
wawekezaji katika maeneo ya hifadhi wanatoka katika mataifa ya Marekani
na Ulaya na kuwa hakuna wawekezaji kutoka China na kuwahimiza sasa
kutumia fursa zilizopo katika hifadhi kwa ajili ya kuwekeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi
ya Utalii nchini Dk. Aloyce Nzuki alihimiza mashirika ya kuratibu
safari za wageni yanayomilikiwa na serikali nchini China kufungua matawi
ya ofisi zao nchini ili kusaidia kuongeza idadi ya wageni kutoka China
kutembelea vivutio vya utalii nchini. Alisema kuwa zipo fursa nzuri za
uwekezaji ikiwemo kuanzisha safari za boti katika Ziwa Tanganyika na
Victoria pamoja na safari za utalii kwa kutumia usafiri wa treni hasa
katika ukanda wa Saadani na Mkomazi.
Pande zote mbili zilikubaliana
kubainisha maeneo halisi ya ushirkiano na uwekezaji na kuandaa Hati ya
Makubaliano ambayo itawekwa saini na pande zote ikiwa ni njia nojawapo
ya kuendeleza uhusiano wa siku nyingi baina ya Tanzania na China ambao
uliasisiwa na marais wa kwanza wa nchi hizi hayati Julius Nyerere na
hayati Mao Zedong.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)