Na Eeuteri Mangi na Hussein Makame - Maelezo
Rais wa Jamuhuri ya watu wa China Xi Jinping anataraija kuanza ziara ya kihistoria nchini tangu kuapishwa kwake kuitumikia nchi hiyo ambapo katika ziara hiyo atasaini mikataba 17 ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Serikali za Tanzania na nchi hiyo.
Akiongea
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe alisema kuwa ziara hiyo ni ya kwanza barani Afrika kwa Rais huyo mpya wa China baada ya kuchaguliwa kuliongoza taifa hilo Machi 14 mwaka huu.
Lengo la ziara hiyo ambayo itaanza tarehe 24 hadi 25 Machi mwaka huu ni kukuza uwekezaji na
biashara baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Baadhi
ya Mikataba hiyo itahusiana na uboreshaji wa sekta ya viwanda, kilimo
hasa cha tumbaku ikiwemo kuwatafutia soko wakulima kutoka mikoa ya
Tabora na Ruvuma ili waweze kuuza zao hilo katika soko la China.
Waziri
Membe alisema kuwa; “Mikataba mingine ni ya kulipatia Shirika la
Utangazaji Tanzania zana za kufanyia kazi na kuandaa mazingira ya ujenzi
wa bandari ya Bagamoyo itakayounganishwa na reli ya Tanzania na Zambia
(TAZARA), reli ya kati na barabara”.
Rais Xi Jinping pia atazindua na kukabidhi rasmi kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere chenye ghorofa tatu na kumbi nne za mikutano zenye uwezo kupokea
washiriki zaidi ya 1800 kilichogharimu dola za kimarekani milioni 29.7
zilizotolewa na Serikali ya China kwa lengo la kumuenzi Mwalimu
Nyerere.
Waziri
huyo alisema kuwa baada ya kufika nchini Rais Xi Jinping atazungumza na
mwenyeji wake Rais Dk. Jakaya Kikwete pamoja na Viongozi Waandamizi wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadaye atahudhuria dhifa
ya kitaifa Ikulu Jijini Dar es salaam.
Siku ya pili ya ziara yake Rais Jinping atazungumza
rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk
Ali Mohamed Shein pamoja na ujumbe wa viongozi waandamizi kutoka
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Waziri Membe aliongeza kuwa Rais Jinping atatoa hotuba maalumu kwa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla na kuzungumzia
sera ya Serikali mpya ya China kwa bara la Afrika ambayo itahudhuriwa
na watu kutoka kada mbalimbali ikiwemo Viongozi na Maafisa Waandamizi wa
Serikali, Wahadhiri wa Vyuo Vikuu,Wabunge, Viongozi wa Dini na Asasi za
Kiraia na Wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali.
“Hotuba hiyo ya Rais wa China ataitoa kwa lugha ya Kichina na kutafsiriwa kwa
lugha ya Kiingereza na Kiswahili ili iweze kuifika dunia nzima, hivyo
tunaviomba vyombo vya habari nchini vichukue fursa hiyo kuwa vya kwanza
kuutangazia Ulimwengu” alisema Waziri Membe.
Ziara hiyo ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China ni muendelezo wa uhusiano mzuri kati ya nchi hiyo na Tanzania ulioasisiwa na viongozi wa mataifa hayo mawili, yaani Mao Zedong wa China na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania.
Rais
Jinping ataondoka nchini Machi 25 saa 10:40 jioni kuelekea nchini
Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa tano wa Wakuu wa Nchi zinazokuwa kwa
kasi kiuchumi ambazo ni Brazil, Urusi, India, China na Afrika ya Kusini
(BRICS).
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)