Na Anna Nkinda – Maelezo, Sumbawanga
Wanawake nchini wametakiwa kusimamia malezi na maadili ya watoto wao
kwa kuwapa elimu juu ya makuzi na hata kama mila zinazuia kufanya hivyo
wawatafute wazee ili waweze kuongea na vijana hao kwani mama ndiye mlezi mkuu wa familia.
Wito
huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wakati akiongea na
Umoja wa wanawake wa mkoa wa Rukwa (Rukwa Women in Action – RUWA)
katika ukumbi wa mikutano wa manispaa ya Sumbawanga.
Mama
Kikwete ambaye yuko mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu
alisema kuwa mama ni muhimili mkubwa wa familia yeye ndiye anayemlea
baba na watoto, hata kama baba atatoa pesa za kutunzia familia lakini
bado muangalizi mkuu wa familia ni mama.
“Wahimizeni mabinti wasome shule hata kama ninyi hamjasoma naamini mnaelewa umuhimu wa shule, simamieni elimu ya watoto wenu ili waweze kusoma kwa bidii na mkijidhatiti ipasavyo watasoma hadi kufikia ngazi ya chuo kikuu.
Katika suala la elimu mtoto wa kike anakabiliwa na changamoto nyingi zaidi ukilinganisha na wa kiume wakanyeni watoto wenu kwani shule nyingi ni za
mchanganyiko washirikiane na watoto wa kiume katika masomo tu na siyo
mambo mengine kwani binti akipata ujauzito au maambukizi ya Virusi Vya
Ukimwi (VVU) ndoto zake za maisha kwa kipindi kile inapotea. Ni mabinti
wachache walioweza kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua”,
alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA aliwasisitiza wanawake hao kujitokeza kwa wingi kuomba na
kugombea nafasi mbalimbali za uongozi pindi zinapotangazwa katika mkoa
huo na waungane kwa pamoja kumpigania mwanamke mwenzao pale
atakapogombea kwani mwanamke ni kiongozi mzuri ndani ya familia na jamii
pia.
Mama
Kikwete alisisitiza, “Kuna baadhi ya wanaume wanawakataza wake zao
kugombea nafasi za uongozi hii si sawa na hawawatendei haki ya msingi
kwani katiba ya nchi inasema kuwa kila mtu anahaki ya kuchagua na
kuchaguliwa na wanawake wengi waliopewa nafasi ya kuongoza wameweza”.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa huo Injinia Stella Manyanya alisema kuwa
manispaa ya Sumbawanga pekee inawatoto yatima 536 ambao wengi wao
wamepotelewa na mama zao na watoto 17 hawana wazazi wote wawili hivyo
basi kina mama wa kikundi hicho wanakazi kubwa ya kuwalea watoto hao.
Injinia
Manyanya alisema, “Tunaishukuru Taasisi ya WAMA kwa kuendelea
kuwachagua na kuwasomesha watoto yatima na wanaotoka katika mazingira
hatarishi kwa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne ambapo toka mwaka
2010 hadi 2013 vijana wa kike 12 kutoka mkoa huu wamesomeshwa”.
Akisoma
taarifa ya umoja huo Leonora Jairos ambaye ni mwanachama alisema kuwa
malengo waliyonayo ni kuwahamasisha na kuwaelimisha wanawake juu ya
umuhimu wa elimu hasa ya mtoto wa kike, kuelimisha jamii juu ya afya za
uzazi wa mpango salama,kutoa elimu kwa kina mama juu ya maisha halisi
ili kujinasua kutoka hali tegemezi na kuongeza jitihada za kupunguza
maambulizi ya VVU.
“Hadi
sasa tumefanikiwa kuwaunganisha wanawake wapatao 200 ambao ni wakulima,
wajasiriamali na wafanyakazi katika manispaa ya Sumbawanga,
tumewatembelea watoto
yatima na kuwachangia vitu mbalimbali kwa mahitaji yao ya kila siku,
kufanya tamasha na kuwahamasisha wanawake kushiriki katika michezo na
mazoezi ili kuboresha afya zao”, alisema Jairos.
Alizitaja
changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na ukosefu wa mwamko wa
wananchi katika suala la elimu hasa la kuwasomesha watoto wa kike, mila
kandamizi kwa wanawake zilizopo katika mkoa huo na uwezo mdogo wa umoja
wa kuweza kuwafikia wasichana mashuleni ili kuwapa maadili juu ya
umuhimu wa elimu.
Umoja
huo ulianzishwa tarehe 22/09/ 2012 kwa wazo la Mkuu wa mkoa huo Injinia
Manyanya ambaye aliona kuna umuhimu wa kuwaunganisha wanawake wote ili
waweze kujiinua kiuchumi, kujitambua na kujiendeleza kielimu na kiafya
na kubadilisha mtazamo wao ili kila mmoja aweze kupiga hatua mbele ya
kimaendeleo na kuwaamsha walio chini zaidi hasa wale wa vijijini.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)