Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Bi. Mwanamvua Ngocho, akizungumuza na wageni waalikwa, abiria waliosafiri na ndege la shirika hilo, pamoja na maofisa wa uwanja wa ndege la Mtwara (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa safari za ndege za Shirila la Ndege la Tanzania (ATCL) mkoani Mtwara , mara tu baada ya kutua ndege hiyo uwanjani hapo mwishoni mwa wiki.
Meya wa Mtwara Mikindani, Selemani Mtalika Shilingi ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa safari za ndege za Shirila la Ndege la Tanzania (ATCL) mkoani Mtwara, akizungumuza na wageni waalikwa, abiria waliosafiri na ndege la shirika hilo, pamoja na maofisa wa uwanja wa ndege la Mtwara (hawapo pichani) mara tu baada ya kutua ndege hiyo uwanjani hapo mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Bi. Mwanamvua Ngocho na kulia ni Meneja Rasilimali watu na Utawala, Bi. Halima Nabalang’anya. Picha na mwandishi wetu.
Baadhi ya abiria waliopanda dege ya Shirika la ndege la Tanzania (ATCL), wakitembea kuelekea katika chumba cha kupumzikia abirai, wakati wa uzinduzi wa safari za ndege za shirila hilo mkoani Mtwara iliyofanyika mwishoni mwa wiki.
====== ====== ========
Safari za ndege ya ATCL kwenda Mtwara zaanza
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Ndege la Air Tanzania (ATCL) mwishoni mwa wiki lilizindua upya safari zake za moja kwa moja za Dar es Salaam-Mtwara na kuahidi kuongeza idadi ya safari hizo na kutoza nauli nafuu.
Akizungumza baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Mtwara, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Bi. Mwanamvua Ngocho alisema kuwa kurejeshwa kwa huduma za usafiri wa anga na shirika hilo la taifa mjini Mtwara ni chachu ya mapinduzi makubwa katika usafiri wa anga mjini hapo kwa kuhakikisha kuwa abiria wanapata huduma bora na za kiushindani.
"Nataka kuwahakikishia wakazi wa Mtwara kwamba ndege yao ya taifa imekuja kuwahudumia watu wa mkoa huu. Kwa kuanzia, tutaruka Mtwara mara nne katika wiki; ikiwa ni siku za Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili, lakini tutaendelea kufanya marekebisho ya safari kutegemeana na mahitaji. Abiria watarajie ATCL kuwapatia huduma ambazo ni salama na za gharama nafuu, "alisema.
Mwanamvua alieleza kuwa shirika hilo litatoza shilingi 199,000 / - kwa tiketi ya kwenda na kurudi, na kuahidi kuwa shirika hilo litafanyia kazi suala la kupunguza gharama za usafiri zaidi ili kuwawezesha wasafiri wanaoenda na kutoka Mtwara kuona faida za kutumia usafiri wa anga.
Kwa upande wake, Meya wa Mtwara Mikindani, Selemani Mtalika Shilingi ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema baada ya ndege ya taifa kurejesha huduma zake mkoani Mtwara, wakati wa shirika moja la ndege kutawala utoaji huduma mkoani hapo na kulazimisha abiria kulipa nauli za juu, sasa umekwisha.
“Ninafuraha kuona shirika la ndege la taifa likiwa limerejesha huduma zake mkoani Mtwara. Kwa muda mrefu sasa usafiri wa anga hapa Mtwara imekuwa ikitawaliwa na shirika moja tu la ndege. Ukweli ni kwamba, pasikuwepo na ushindani, suala la bei mara nyingi ni changamoto kwa walaji/wateja. Abiria wa kwenda na kutoka Mtwara wamekuwa wakilipa nauli za juu. Ila kwa kuwa tuna ATCL sasa na Kaimu Mgurugenzi wa Biashara ametuakikishia, wakazi wa Mtwara na wageni wetu watapata fursa ya kufurahia usafiri wa anga ulio salama na wa gharama nafuu,” alisema Shilingi.
Meya huyo alisema kuwa idadi ya abiria wanaokwenda Mtwara imekuwa ikiongezeka sana katika siku za karibuni, kwa sababu Mtwara imekuwa na sura ya kibiashara baada ya ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi asilia na kuwa mkoa unaozalishaji zao la korosho kwa wingi hapa nchini.
“Wawekezaji wengi wanaendelea kumiminika katika mkoa wetu, na hivi karibuni Mtwara itakuwa na muonekano tofauti kabisa. Ushawishi huu wa kuwekeza mkoani Mtwara umeongeza idadi ya abiria wanaosafiri na ndege. Nina uhakika ATCL itaona ongezeko la abiria mapema na kulifanya shirika kuongeza idadi ya safari zake mapema,” alisema.
Shirika hilo litatumia ndege yake aina ya Dash 8-300 yenye uwezo wa kubeba abiria 50, wakati huu wa mwanzoni, lakini uongozi umebainisha kuwa pale idadi ya abiria itakapoongezeka kuzidi uwezo wa Dash 8, watatumia ndege yao aina ya Boeing.
Urejeshwaji wa safari za Mtwara umekuja ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya shirika hilo pia kurejesha safari za Kigoma baada ukarabati wa uwanja wa ndege wa Kigoma kumalizika.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)