ASKOFU wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la
Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo, amesema hafikirii kuwa
Papa. Kauli ya Pengo ameitoa jana nyumbani kwake, alipokuwa akizungumza
na waandishi wa habari waliotaka kujua mtazamo wa Kanisa baada ya Papa
Benedi
ct XVI, kutangaza kujiuzulu ifikapo Februari 28 mwaka huu.
Akijibu swali la mwandishi wa gazeti
hili bila kueleza kwa kina, Pengo alijibu: “Sifikirii kuwa Papa, na hili
halina mjadala.” Akizungumzia alivyochukulia suala la kujiuzulu kwa
Papa Benedict XVI, Pengo alisema wamepokea kwa mshangao na mshituko.
Alifafanua kwamba ingawa jambo hilo si
mara ya kwanza kwa Papa kujiuzulu, lakini hali kama hiyo iliwahi kutokea
karne sita zilizopita. Mwaka 1415, Papa Gregory XII alijiuzulu
katika mpango wa kumaliza mgogoro uliokuwepo wakati huo kati ya
makadinali wa Nchi za Mashariki kugombea kiti hicho.
“Ni wazi kuwa kitu kinatokea baada ya
miaka 600 ni kitu cha kushangaza na kujiuliza na maswali yanapita
vichwani mwa watu, lakini hili si jambo la kwanza kutokea. Papa ameweka
wazi sababu zake kuwa anajisikia kupungukiwa nguvu si za kiakili wala
ugonjwa fulani,” Pengo alisema yeye anaona hatua iliyochukuliwa na
kiongozi huyo wa juu wa Kanisa Katoliki, ni jambo la unyenyekevu
alionao, kwa kuona ukweli ndani ya nafsi yake.
Viongozi ving’ang’anizi “Ni mfano kwa
viongozi wanaong’ang’ania madaraka. Wanakaa madarakani kwa muda mrefu
pamoja na kutokuwa na faida kwa watu wao na wakati mwingine hawatambui
hilo, wanazidi kuona uongozi ni haki yao na kuona bila wao nchi haipo.
Nadhani wanapaswa kujifunza kwa Baba Mtakatifu,” alisema.
Vipi Afrika?
Alipoulizwa kuwa haoni wakati umefika
kwa Afrika kutoa Papa, Pengo alisema hisia hizo ni za kisiasa zaidi ya
imani ya kidini, kwani Papa huchaguliwa kwa msingi wa Roho Mtakatifu
kupitia makadinali na si kwa kujuana.
“Kumchagua Papa ni shughuli inayokwenda
na tafakari nzito, na sala na tunafanya tukiwa mbele za Mungu, ni jambo
linalofanyika mbele ya msalaba na kila mmoja anaweka kura yake kwa
kueleza dhamira yake na Kristo ndiye atahukumu siku ya mwisho,” alisema.
Alisema kutamka kuwa wakati umefika wa
kuwa na Papa kutoka Afrika au Muitaliano, ni kumwekea masharti Roho
Mtakatifu na kuwa nje ya imani ambayo Roho Mtakatifu ndiye anayetenda
kazi.
“Endapo itatokea akachaguliwa Papa kutoa
Afrika, basi Roho Mtakatifu atakuwa ameona kuwa ni wakati wa Afrika,
hiyo kazi tunamwachia Roho Mtakatifu atende kazi,” alisema.
Alisema hatua ya Papa kujiuzulu si jambo
la kutia shaka, bali ni la kujenga imani na kuwa kamwe Kanisa
halitasambaratika kwa sababu misingi ya Kanisa haimtegemei mtu mmoja,
bali anayechaguliwa anaongoza kwa matakwa ya Mungu.
“ Kristo ndio nguzo yetu, yeye
angeliacha kanisa tungesambaratika. Hakuna haja ya watu kuwa na mashaka.
Kristo alipomwambia Petro yule Mgalilaya kuwa ’Petro nakukabidhi Kanisa
langu hata milango ya kuzimu haitalishinda hakumaanisha mtu mmoja,”
alisema.
Matumaini Afrika Nafasi ya Afrika katika
siasa za kumpata Papa, imetajwa kuwa finyu, kutokana na watarajiwa
wengi wa kumrithi Papa Benedict XVI kutoka Ulaya huku wapigakura wengi
pia wakitoka katika Bara hilo. Afrika inamtegemea zaidi Kadinali Peter
Appiah (64) wa Ghana ambaye ni Rais wa Baraza la Haki na Amani la Kanisa
Katoliki Vatican.
Anachukuliwa kama mmoja wa wagombea
wenye nguvu, lakini fursa ya kuchaguliwa ni ndogo. Kadinali Appiah nyota
yake imekuwa iking’ara kutokana na kukubalika kwake na makadinali
wenzake na uwezo wa juu katika lugha mbalimbali. Kiongozi huyo wa
Vatican kutoka Ghana, anazungumza lugha tisa ikiwemo Fante, Kingereza,
Kifaransa, Kiitaliano, Kijerumani, Kiyahudi, Kiaramu, Kiarabu na
Kigiriki. Anatazamwa kama alama ya Kanisa Katoliki
kukubalika ulimwenguni kote kutokana na mtazamo uliopo kwamba mafanikio
ya baadaye ya Kanisa Katoliki si Ulaya tena kama ilivyokuwa desturi,
bali ni katika kujitanua duniani hasa nchi zinazoendelea.
Hata hivyo, kikwazo cha kuchaguliwa
kwake, kinatokana na mtazamo kuwa atabadilisha Kanisa Katoliki na kuwa
tofauti na mtazamo wa makadinali wengi ambao wanatoka Ulaya. Pia kama
Mwafrika, Kanisa Katoliki Afrika, limekuwa na ajenda tofauti na la
Ulaya.
Wakati Ulaya ajenda kubwa imekuwa
unyanyasaji wa kijinsia na migongano ya kitheolojia, Afrika ajenda ni
katika utoaji wa mashetani na hali ya upagani. Pia Papa kutoka Afrika
anaonekana atashughulika zaidi na changamoto ya kukua kwa Uislamu na
upinzani wa sera za kiuchumi za nchi za Magharibi. Watarajiwa wengine Kadinali Angelo
Scola (70) wa Italia Ni Askofu wa Milan na anapewa nafasi ndogo, lakini
kubwa kuliko Kadinali Appiah.
Kuteuliwa kwake kutamaanisha kwamba
Kanisa linalenga katika kuimarisha Ukristo barani Ulaya. Uwezekano wa
kuteuliwa kwake unatokana na kukubalika zaidi na makadinali wenzake wa
Italia na usomi wake katika theolojia ya mambo ya familia, ambayo Kanisa
Katoliki Ulaya, linataka mambo hayo ya familia yapewe kipaumbele. Hata hivyo, anakabiliwa na upinzani wa makadinali wengi, ambao hawapendi muonekano wa Kanisa kuwa taasisi ya Bara la Ulaya.
Kadinali Tarsicio Bertone (77) Ni Waziri
wa Mambo ya Nje wa Vatican, anapewa nafasi kubwa kuliko Kadinali Scola.
Anatajwa kuwa mwanasiasa mwenye mbinu na elimu nzuri na amekuwa
akitamani nafasi ya kuwa Papa kabla ya kufa kwake. Sifa kubwa anayotajwa nayo ni ushiriki wake mkubwa katika ushauri wa uteuzi wa makadinali wa Italia.
Hata hivyo, makadinali wengi ambao si
Wataliano hawampendi na wamekuwa wakimtafsiri kama mtu anayeweza
kusababisha kashfa kama akipewa nafasi hiyo.
Kadinali Jorge Bergoglio (75) Ni
Muargentina anayepewa nafasi zaidi ya Kadinali Bertone. Anatajwa kuwa na
msimamo wa kuhimiza haki katika jamii na msimamo wa kati katika mambo
mengi. Hata hivyo katika mkutano wa 2005 wakati wa uchaguzi wa Papa
Benedict, alipata kura kidogo na kutafsiriwa kuwa muda wake wa kuongoza
umeisha. Kadinali Angelo Bagnasco (69) wa Italia Ni Askofu wa Genoa na
Rais wa Baraza la Maaskofu la Italia.
Anapewa nafasi na anatajwa kuwa na
msimamo wa kutopenda mabadiliko ya Kanisa kutoka katika liturugia ya
zamani na ana umaarufu mkubwa kuliko makadinali wengine wa Italia.
Hata hivyo, msimamo wake mkali katika
kurudisha kanisa katika misimamo na liturugia ya zamani, unatishia
kukubalika kwake kwa makadinali wanaotaka mabadiliko. Kadinali Christoph Schönborn ( 67) wa
Austria Ni Askofu wa Vienna na anapewa nafasi ya juu kuliko Kadinali
Bagnasco na Kadinali Bergoglio.
Anatajwa kuwa mfuasi mkubwa wa Papa John
Paul II. Hata hivyo, uongozi wa Vatican, una mashaka kuhusu imani yake
katika misingi ya Ukatoliki, kwa kuwa aliwahi kuingilia uamuzi wa Kanisa
wa kumtenga muumini anayetetea ndoa ya jinsia moja na kumrejesha
kundini.
Hataki upapa Kadinali Marc Ouellet (67)
wa Canada Alikuwa Askofu wa Quebec na kiongozi wa Baraza la Maaskofu.
Anapewa nafasi sawa na Kadinali Schönborn kwa kuwa amekuwa akishiriki
katika kuteua Maaskofu baada ya kupitia sifa zao na anaaminika kwa kazi
hiyo.
Anaweza kuwa Papa mwenye uwezo wa kuongoza Kanisa Katoliki. Kadinali Ouellet anatajwa kuwa na sifa zilizojitosheleza. Anazungumza vyema lugha sita ikiwemo Kingereza, Kifaransa, Kireno, Kitaliano, Kihispania na Kijerumani.
Amewahi kufanya kazi Amerika ya Kusini.
Hata hivyo anadaiwa haipendi kazi hiyo na kuna uwezekano akiteuliwa,
akakataa uteuzi huo kwa kuwa inaruhusiwa kukataa kuteuliwa.
Amekuwa akisema kazi ya Papa ni ngumu
ambayo hataweza kuitumikia, lakini msimamo huo unamfanya aonekane mmoja
wa wa wagombea wenye mvuto. Kadinali Timothy Dolan (62) wa Marekani Ni
Askofu wa New York.
Naye anapewa nafasi kubwa ya kuwa Papa.
Akiteuliwa atakuwa kiongozi aliyepanda madaraka katika muda mfupi mno.
Anatajwa kuwa na sifa ya kuwasiliana na kukubalika na wenzake na ujana
wake utampa nafasi ya kutumikia nafasi hiyo kwa muda mrefu kama Papa
John Paul II.
Hata hivyo Umarekani wake, mwenye
kupenda misimamo ya kati haonekani kama kiongozi mzuri wa Vatican.
Kadinali Albert Ranjith (64), wa Sri Lanka. Ni Askofu wa Colombo.
Aliwahi kuwa Waziri wa Nidhamu ya Sakramenti na Ibada Vatican.
Anatajwa kuwa kiongozi mwenye uwezo wa
kurejesha liturugia ya zamani ya Kanisa na anapendwa na karibu kila
Kadinali. Hata hivyo, kama dhana itakuwa kumpata Papa kutoka nchi
zinazoendelea, kuna uwezekano asiteuliwe kwa kuwa uwezekano wa Papa
kutoka nchi zinazoendelea, ni kutoka Afrika au Latin Amerika ambako
Kanisa Katoliki lina nguvu. Utaliano shida Kadinali Antonio Llovera (66)
wa Italia.
Amewahi kuwa Askofu wa Toledo. Ni
kiongozi anayeshughulikia Nidhamu ya Sakramenti na Ibada Vatican. Si
maarufu sana. Anajulikana kama ‘Benedict mdogo’ na akiteuliwa,
inaaminika katika kuendeleza utawala wa Papa Benedict kwa kufuata nyayo
zake na malengo ya kurudisha kanisa Katoliki katika asili yake ya zamani
taratibu.
Hata hivyo muonekano wake unatajwa kuwa
si wa ushawishi wa kukabidhiwa wadhifa huo, pamoja na kuwa na mtazamo
usiofurahisha wa mabadiliko ya liturugia yaliyokuwa yakifanywa na Papa
Benedict. Kadinali Norberto Carrera (70) wa Mexico Ni askofu wa Mexico
City.
Anapewa nafasi kubwa kuliko Kadinali
Llovera kutokana na nguvu za Kanisa Katoliki Latini Amerika. Anatajwa
kuwa Kadinali asiye na woga, alikemea rushwa na ufisadi katika Serikali
ya Mexico kiasi cha kusababisha Serikali, kufikiria kuwa na sheria ya
kuzuia viongozi wa dini kuzungumzia siasa hadharani. Hata hivyo,
utendaji wake usio na woga na msimamo wake katika kutetea haki katika
jamii, unakwaza wengi. Kadinali George Pell (70) wa Australia Ni Askofu wa Sydney. Anapewa nafasi kubwa zaidi kuliko Kadinali Carrera.
Anatajwa kuwa mfuasi wa Papa Benedict,
lakini mwenye uwezo wa juu katika masuala ya mawasiliano na vyombo vya
habari. Kama akiteuliwa, anatajwa kuwa na uwezo wa kuendeleza utendaji
wa Papa Benedict, wa kurudisha liturugia ya zamani ya Kanisa Katoliki.
Hata hivyo anasemekana kutaka kurudisha
uhusiano na Shirika la Mtakatifu Pius X, kikundi cha Mapadre
kilichotengwa na Kanisa Katoliki tangu 1998. Kadinali Mauro Piacenza
(67) wa Italia Kiongozi wa Utume katika Kanisa Katoliki Vatican.
Yeye hapewi nafasi sana, lakini anatajwa
kuwa kiongozi anayetaka Kanisa liongeze nguvu katika Bara la Ulaya kwa
kutafuta mapadre waliofuzu kwa viwango vya juu.
Anatajwa kwamba si mtu mwenye
ushirikiano mkubwa na vyombo vya habari, ingawa inatajwa kama moja ya
sifa ya papa wa kisasa. Kadinali Angelo Amato (73) wa Italia.
Ni Kiongozi wa Mkutano wa Makadinali
anayeshughulikia utakatifu na aliwahi kuwa Waziri wa Kanuni za Imani.
Hapewi nafasi pia, lakini mara nyingi Kadinali kutoka Italia mwenye umri
wa kati ya 65-75, anayo nafasi ya kutwaa Upapa. Anatajwa kuwa mfuasi wa
Papa Benedict XVI. Amefanya kazi katika ofisi mbalimbali za
Vatican ingawa Utaliano wake unaweza kumkosesha nafasi hiyo. Kadinali
Crescenzio Sepe (69) wa Italia Ni Askofu wa Naples. Hapewi nafasi kubwa
kutwaa nafasi hiyo.
Hata hivyo anatajwa kuwa mtumishi wa
muda mrefu Vatican. Pia anatajwa kuwa na uzoefu wa kutoa huduma Latini
Amerika. Hata hivyo hajulikani sana kama wenzake
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)