William
Zelothe Stepehen ni Mtanzania wa Kwanza Mmaasai aliyepewa ithibati ya
kuiongoza ndege aina ya Airbus A319 punde tu baada ya kupokea mafunzo ya
urubani yaliyodhaminiwa na shirika la ndege la fastjet. Alipata mafunzo
hayo nchini Uingereza kwa muda wa takriban miezi miwili na amerudi
nchini Tanzania hivi karibuni. William alikulia Olosipe jijini Arusha
ambapo ni nyumbani kwa wazazi wake.
William
anafananisha anavyojihisi anapoiongoza ndege ya Airbus A319, na wakati
akiwa katika nyumba nzuri ya kifahari na ya kisasa; anaielezea ndege ya
Airbus A319 kama ndege iliyo imara na ambayo imewekewa mifumo mingi ya
usalama. Kwa maneno yake mwenyewe, anasema “Ndege ya Airbus inakulinda
kweli kweli, kama unaifahamu vyema”
William
amewahi kusomea usimamizi wa wanyama pori; alipata mafunzo ya urubani
kwa mara ya kwanza kule Florida Aviation Academy nchini Marekani mwaka
2006 ambapo alipata leseni yake ya usafirishaji kwa ndege. Ingawa ana
umri mdogo, ana uzoefu wa masaa 3,053 ya kuongoza ndege.
Kumwajiri rubani huyu mtanzania mwenye miaka 28, ni mojawapo ya jitihada za fastjet za kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inaajiri watendaji wazawa waliobobea katika fani hiyo hapa nchini. Mikakati yao ya kuajiri pia ni mojawapo ya wajibu wao mpana wa kuwekeza nchini Tanzania. Kwa kila rubani aliyepokea mafunzo, fastjet imetumia gharama inayokadiriwa shilingi 49,546,400 hela za kitanzania ambayo ni sawa na 31,027 dola za kimarekani.
fastjet
ni shirika jipya la ndege la nauli nafuu Afrika ambalo lilipata umiliki
wa FLY540 na kwa mantiki hiyo likazindua kampuni ya kwanza ya usafiri
wa ndege ambalo linazingatia bajeti. Fastjet, ambayo inaungwa mkono na
mwanzilishi wa Lonrho na easyGroup Bwana
Stelios Haji Ioannou, imetambulisha nauli za kiwango cha chini hadi
kiasi cha Tsh32,000 bila kujumlisha kodi ili kuwawezesha mamilioni ya
watu ambao walikuwa wameshindwa kusafiri kwa ndege, kuweza kusafiria
ndege kwa mara ya kwanza na kuendelea kutumia ndege mara kwa mara. Tangu
kuzinduliwa kwake mwezi Novemba 2012, shirika hili la fastjet
limewasafirisha zaidi ya watu 70,000 na asilimia 99.7 ya safari za ndege
zikisafiri katika muda uliopangwa.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)