TAARIFA YA NDUGU ZITTO KABWE (MB) KUHUSU YANAYOENDELEA
MTWARA NA MRADI WA BOMBA LA GESI ASILIA
Serikali iache kutafuta mchawi, iende Mtwara
Katika kipindi cha wiki nne sasa kumekuwa na maandamamo, malumbano na vurugu kuhusu mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Mradi huu wa kutandaza bomba la urefu wa kilometa 542 ni mkubwa sana hapa nchini, na una thamani kubwa zaidi kuliko miradi mingine yote ya miundombinu iliyopata kutokea hapa nchini. Mradi huu utajengwa kwa mkopo wa dola za Kimarekani 1.2 bilioni kutoka Benki ya Exim ya China.
Wananchi wa Mtwara kupitia maandamano ya tarehe 27 Desemba 2012 wametaka kujua hatma ya maendeleo ya mikoa wa kusini kutokana na mradi huu wa bomba la gesi. Serikali imewajibu wananchi hawa kwa kuwaita wahaini, watu hatari na wasio elewa. Imefika mahali inapotosha madai yao kwamba hawataki gesi itoke Mtwara.
Kimsingi Serikali haijajibu hoja yeyote ya msingi ya wananchi wa Mtwara kuhusu mradi wa kusafirisha gesi. Badala yake imekuwa ikijaribu kupotosha madai ya watu wa Mtwara kupitia mikutano na vyombo vya habari.
Tangu maandamano haya yatokee, na baadaye mikutano ya hadhara na hatimaye matukio ya kusikitisha ya kuharibu mali za watu, mauaji ya watu na majeruhi mbalimbli, Serikali na hasa Wizara yenye dhamana ya mradi huu, imekuwa ikitoa matamko kwenye vyombo vya habari badala ya kwenda Mtwara kuzungumza na wananchi, kusikiliza madai yao na kuona
namna ya kutekeleza madai hayo. Kutokana na Serikali kutofanya hivyo, kusikiliza na kuzungumza na wananchi wa Mtwara, vurugu mbaya sana zimeendelea mkoani humo.
namna ya kutekeleza madai hayo. Kutokana na Serikali kutofanya hivyo, kusikiliza na kuzungumza na wananchi wa Mtwara, vurugu mbaya sana zimeendelea mkoani humo.
Mwezi uliopita, Desemba 2012, tatizo lilionekana kuwa ndogo na lenye kuhusiana zaidi na ukosefu wa kushirikishwa kwa wananchi. Badala ya kushughulikia tatizo likiwa bado ndogo, Serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisemakuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro huu.
Leo hali iliyopo mkoani Mtwara inasikitisha sana, maana mali za wananchi zinaharibiwa, nyumba zinachomwa moto na watu wanapoteza maisha. Tunalaani matukio haya kwa nguvu zetu zote, maana kinachotokea Mtwara si Utanzania. Tusipowasikiliza wananchi na kutatua mgogoro huu kwa kuwashirikisha, hali itazidi kuzorota wakati tukitupiana lawama.
Hivi sasa serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisema kuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro huu.
Kwanza, Serikali imekuwa ikiaminisha umma kwanza suala hili limechukuliwa kisiasa. Pili, Serikali imekuwa ikirudia kusema kuwa baadhi ya makampuni ya uwekezaji nchini na mataifa ya Magharibi yamekuwa yakichochea wananchi wa Mtwara.
Katika mwendelezo wa mtindo wa Serikali wa ‘management by press conferences’ jana Jumamosi Naibu Waziri wa Nishati na Madini ndugu George Simbachawene aliwaambia wahariri kwamba mimi Zitto Kabwe ninachochea wananchi wa Mtwara, ninatumiwa, na si mzalendo. Vile vile alitoa vielelezo kadhaa kuonyesha kuwa mradi wa kujenga bomba la gesi ni gharama sawasawa. Akasisitiza kwamba mimi ni mwongo.
Katika kipindi chote cha mgogoro wa Gesi Mtwara, sijafika Mtwara. Sijafanya mkutano wowote na waandishi zaidi ya kuandika mawazo yangu, kama Mtanzania kuhusu suala hili.
Nimeandika makala nne na zimechapishwa katika magazeti kadhaa hapa nchini na kwenye blogu yangu (www.zittokabwe.com).
Niliandika: Utajiri wa Gesi Asilia: Tuwasikilize Watanzania wa Mtwara na Lindi. Nikaandika tena: Tusipuuzemandamano dhidi ya Bomba la Gesi: Kilio cha Uwajibikaji; Nikaandika tena: Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi; ni baadhi ya makala nilizoandika kuhusiana na suala la Mtwara.
Sitaki kubishana na Naibu Waziri ama Kiongozi yeyote ya Serikali kwa sasa. Hatuwezi kuendelea kulumbana, kuzozana, kuzodoana na kurushiana maneno wakati nchi yetu inaungua. Huu sio wakati wa kutafuta mchawi bali kutafuta majawabu ya changamoto zilizopo mbele yetu.
Yanayotokea Mtwara ni fundisho kwetu kwa Taifa namna ya kukabili changamoto za utajiri wa rasilimali, ili kuweka mkakati, mambo haya yanayotokea Mtwara yasitokee tena Tanzania. Tutaweza kuzuia maafa haya iwapo tutaweka uwazi katika mikataba, tutashirikisha wananchi kwenye unyonyaji wa maliasili za nchi, na iwapo tutaweka uwajibikaji.
Rais Kikwete Kikwete ana majibu; ayatoe sasa kwa wana Mtwara
Kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Umeme nchini (Power System Master Plan), kulikuwa na mradi wa kufua umeme MnaziBay, ambao Rais Jakaya Kikwete aliagiza utekelezwe mara moja. Serikali ieleze umma kuhusu mradi huo wa kujenga kituo cha kufua umeme 300MW MnaziBay Mtwara na kujenga msongo wa umeme wa 300KV mpaka Singida. Umeishia wapi? Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 12 Oktoba 2012, Rais Jakaya Kikwete alipokea ripoti ya ujenzi wa mradi huu kutoka makampuni ya China National Machinery & Equipment Import & Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani, ambayo kwa pamoja yalitarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida. Mradi huu ungegarimu dola za kimarekani milioni 684 na Rais aliagiza utekelezwe haraka sana. Huu mradi uliishia wapi? Kwa nini Serikali ipo kimya kuhusu mradi huu ambao ungejibu kabisa maswali ya watu wa Mtwara? Taarifa ya Ikulu kuhusu mradi huu imeambatanishwa hapa.
Tufanyeje?
Hapa tulipofikia ni lazima kwanza kabisa kusikia kilio cha wananchi wa Mtwara ikiwemo kuelewa madai yao. Swali kubwa kubwa la watu wa Mtwara na Kusini kwa ujumla ni ‘tunanufaikaje’? Jibu la swali hili si ahadi za miradi bali ni vitendo. Hapa ndipo serikali inaposhindwa kushughulikia suala hili, kutoelewa madai ya wananchi na kuyapotosha.Viongozi wa kisiasa wenye ushawishi kutoka pande zote, chama tawala na vyama vya upinzani, waende Mtwara kuzungumza na wananchi, lakini wawasikilize kwanza.
- Lazima viongozi tujenge utamaduni wa kusikiliza wananchi na si kuwahutubia tu. Wananchi wa Mtwara wana madai ambayo lazima viongozi tukae kitako kuwasikiliza kisha kufanya nao majadiliano ambayo yatatoa mwafaka. Rais mstaafu, Ndugu Benjamin Mkapa ameshatoa kauli kuhusu suala hili. Ni wakati mwafaka sasa kwa viogozi wengine kumuunga mkono kwa kwenda Mtwara na kukaa na wananchi wa Wilaya zote za Mtwara, kusikiliza hoja zao na kuona namna ya kupata ufumbuzi wa suala hili. Wakati hatua hii inachukuliwa, wananchi waombwe kutulia na kuacha vurugu za aina yeyote ile, na Serikali isimamishe mradi mpaka hapo suluhu na wananchi itakapopatikana.
- Wakati juhudi hizo zinaendelea Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa bomba, kwani ni dhahiri gharama za mradi huu ni kubwa mno kulingana na uhalisia wa miradi ya namna hii duniani kote. Katika taarifa zote kwa umma Serikali imekuwa ikisema kwamba mradi utagharimu jumla ya dola za kimarekani 1.2 bilioni, lakini katika taarifa ambayo Wizara ya Nishati na Madini imesambaza jana kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini imesema mradi utagharimu dola za kimarekani milioni 875. Usiri katika mkataba huu unaashiria kwamba Serikali inaficha kitu. Hivyo njia pekee ni kutaka mkataba uwe wazi kwa wananchi.
- Wakati tunawataka wananchi wa Mtwara kuruhusu utulivu, ni vema Serikali ijiandae kutoa majawabu ya madai ya wananchi hao. Majawabu ya Serikali yajikite kueleza wananchi wa Mtwara wanafaidikaje na rasilimali ya gesi asilia kwa maendeleo yao. Wananchi wa Mtwara wanataka uwajibikaji wa Serikali kwenye utajiri wa nchi, na wamechoka na porojo za orodha ya miradi isiyotekelezwa.
Viongozi twendeni Mtwara kusikiliza wananchi wetu. Nchi inaungua na hatuwezi kuendelea kuzozana badala ya kuzima moto huu hatari kama vita vya MajiMaji. Mimi nakwenda Mtwara haraka na mara baada ya viongozi wangu wa chama kutoa ridhaa.
ZITTO KABWE
Mbunge, Kigoma Kaskazini (Chadema)
Waziri Kivuli wa Fedha
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)